Mshambuliaji wa KMC, Wazir Junior amesema ana mambo mawili ya kufanya kwenye mechi kumi zilizobaki ili kuweza kufikia malengo ya msimu huu.
Junior ambaye ametupia mabao 11 hadi sasa akiwa nafasi ya tatu kwa wachezaji waliopachika mabao mengi wakiongozwa na Stephane Aziz Ki (13), ameliambia Mwanaspoti kuwa anataka kuvunja rekodi yake baada ya miaka mitatu na kuibuka kinara wa kupachikaji mabao.
"2019/20 nikiwa na Mbao FC nilitupia mabao 13 rekodi binafsi ambayo sijaivunja kwa zaidi ya miaka miwili. Msimu huu nimebakiza mabao mawili kuifikia rekodi yangu mwenyewe ambayo matarajio yangu ni kuivunja," alisema na kuongeza;
"Sio rahisi, lakini naamini kwenye mechi 10 zilizobaki kwakuwa nia ninayo na uwezo pia upo nitahakikisha nafikia malengo ikiwa ni pamoja na kuonyesha ushindani dhidi ya walio mbele yangu kwenye harakati za kuwania kiatu," alisema.
Junior alisema anawaheshimu Aziz Ki na Feisal Salum 'Fei Toto' na ili kushindana nao ni kuhakikisha anafunga bao kwenye kila mchezo ili kutokuacha pengo kubwa kwenye ushindani.
"Wenzangu kwenye kila mchezo wanatumia nafasi wanazotengenezewa na mimi natakiwa kufanya hivyo na kinachonipa jeuri ni namna ambavyo napata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na misimu miwili nyuma ambayo nafasi kwangu ilikuwa changamoto," alisema na kuongeza;
"Kuaminiwa na kocha na kunipa nafasi ya kucheza nahitaji kuwa bora ili kumuaminisha kuwa hajakosea kunipa nafasi, nafikiri ili niweze kufikia malengo yangu natakiwa kufunga bila kumuangalia mshindani anafanya nini kupunguza presha," alisema.
Wazir ambaye anashindana na viungo kwenye ushindani wa kuwania kiatu cha ufungaji bora alisema anatoa nafasi kwa kila mchezaji kupata kiatu hicho kulingana na namna kila mchezaji anavyopambana huku akiweka wazi kuwa hata yeye ana uwezo huo.
Mshambuliaji huyo anashindana na Aziz Ki ambaye amefunga mabao (13) na Feisal Salum 'Fei Toto' (12) huku yeye mwenyewe akipachika mabao 11 na timu mbili hizo zikibakiza mechi 10 isipokuwa Yanga ambayo ina michezo 11.