Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazir Jr amtibulia Benchikha

Waziri Kmc Vbs Wazir Jr amtibulia Benchikha

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabao mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Wazir Junior wa KMC, moja kila kipindi jana yalimtibulia Kocha Abdelhak Benchikha aliyekuwa akiiongoza Simba kwa mara ya pili katika mechi za Ligi Kuu Bara baada ya timu hizo kutoka sare kwenye pambano kali lililopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Benchikha aliyeajiriwa hivi karibuni, aliongoza Simba kushinda mechi ya kwanza akiwa benchi kwenye ligi dhidi Kagera Sugar na kushinda mabao 3-0 na jana alirudi kwenye ligi hiyo bila ya kiungo mshambuliaji Clatous Chama na kulazimishwa sare hiyo iliyoifanya timu hiyo kufikisha pointi 23 baada ya mechi 10.

Chama na Nassor Kapama wamesimamishwa Simba kwa utovu wa nidhamu wakisubiri kupelekewa Kamati ya Nidhamu ya klabu kwa maamuzi zaidi ya kinidhamu.

Hiyo ilikuwa ni sare ya pili kwa KMC dhidi ya Simba katika mechi 11 walizokutana katika ligi tangu timu hiyo ya Kinondoni, ilipopanda daraja mwaka 2018 na ilikuwa ni ya pili pia kwa Simba msimu huu ya kwanza ilikiuwa dhidi ya Namungo. Ligi hiyo inasimama hadi Februari mwakani kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na Afcon inayoanza Januari.

Wazir alifunga bao la kwanza dakika ya 31 baada ya kiungo na nahodha Awesu Awesu kuchezewa madhambi na kuanzisha mpira kwa haraka uliomkuta nyota huyo wa zamani wa Yanga na Toto Africans aliyewapiga chenga mabeki wa Simba kabla ya kumhadaa kipa Ayoub Lakred na kuutia mpira kambani.

Bao jingine la Wazir lililomfanya afikishe mabao saba kwa sasa akilingana na Maxi Nzengeli wa Yanga alilifunga dakika mbili kabla ya pambano kumalizika baada ya kipa Ayoub kushindwa kudaka shuti la Tepsie Evans uliomkuta nyota huyo aliyeutupia wavuni kuisawazishia KMC iliyochupa kwa nafasi moja hadi ya nne ikifikisha pointi 21.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Katika mchezo huo Benchikha alifanya mabadiliko machache ya kikosini kilichoanza kulinganisha na kile kilichoifunga Kagera kwa kumuanzisha John Bocco, Willy Onana na Kibu Denis kuchukua nafasi za Moses Phiri, Mzamiru Yassin na Clatous Chama na kipindi ha kwanza kiliisha kwa Simba kuwa nyuma ya bao 1-0.

Dakika 20 za mwanzo Simba ilianza kwa kasi ikitafuta bao la kusawazisha, huku KMC ikapata nguvu ya kujiamini na kutawala mchezo, baada ya kufunga bao la kuongoza, huku timu hiyo ikipoteza nafasi nyingi za wazi za kupata mabao kutokana na kukosa umakini kila walipokaribia lango la Wekundu wa Msimbazi.

Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Bocco na Onana na kuwaingiza Jean Baleke na Mzamiru ambao waliibadilisha kasi ya mashambulizi ya Simba na katika ya 57, timu hiyo ilipata penalti baada Abdikarim Mohammed kuunawa mpira wakati akiokoa na Mwamuzi Thabit Maniamba kuamuru tuta.

Saido Ntibazonkiza alikwamisha mpira huo akiisawazishia Simba, lilikiwa ni bao lake la nne msimu huu na penalti ya tatu kufunga hadi sasa akiwa ndiye kinara wa mipira hiyo katika ligi na dakika mbili baadaye Baleke alipiga chuma cha pili, likiwa ni bao lake la nane akilingana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.

Baleke alifunga bao hilo akimalizia pasi tamu ya Shomary Kapombe iliyokuwa ya tatu kwake msimu huu akipenyeza mpira pembeni kwa kipa Wilbol Maseke aliyetoka kizembe na Baleke kuukwamisha mpira wavuni.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa Simba wakiamini timu yao imeibuka na ushindi, Wazir Junior akawatibulia kwa kufunga bao la pili baada ya Ayoub kuutema mpira wa shuti la mtokea benchi, Tepsie Evans na mshambuliaji huyo kuuwahi mpira kuisawazishia KMC.

LAKRED NA MALONE

Pamoja na kosa la Ayoub kuruhsu bao hilo la pili la KMC baada ya kuonekana kama kateleza wakati anataka kuukada mpira wa Tepsie, lakini kipa huyo alichezea kwa nidhamu akishirikiana kuwasiliana na mabeki wa kati, Che Malone Fondoh na Henock Inonga na kumfanya aepuka kufanya makosa.

Kila alipokuwa akitaka kuanzisha mpira kwa haraka, Che Malone alionekana kumtuliza na kuituliza timu hiyo ambayo sasa inajiandaa kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 ambapo itaanza kuvaana na Jamhuri ya Pemba siku ya Mwaka Mpya.

Katika mchezo huo wachezaji watatu wa KMC, Ibrahim Elias, George Makang’a na Awesu Awesu walioneshwa kadi za njano.

Wakati beki wa Simba Che Malone alikuwa mchezaji pekee wa upande huo kupewa kadi ya njano .

Chanzo: Mwanaspoti