Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazir Jr: Nyota aliyejitafuta akajipata

Waziri Jr Kk Wazir Jr: Nyota aliyejitafuta akajipata

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Unapozumgumzia ‘King of Kirumba stadium’ ni dhahiri unamzungumzia mshambuliaji wa KMC, Waziri Junior Shentembo ambaye kwa sasa amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu katika Ligi Kuu Bara na kikosi hicho licha ya kutozungumzwa na wengi kama mastaa wengine.

Nyota huyo amekuwa na msimu bora hadi sasa akiwa na timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa ndiye kinara kwa kufunga mabao manane akiwaacha Ibrahim Elias, Daruweshi Saliboko na Rashid Chambo wenye mawili kila mmoja.

Mbali na kuongoza katika kikosi hicho, lakini nyota huyo anashika nafasi ya tatu msimu huu kwenye msimamo wa ufungaji bora nyuma ya kiungo mshambuliaji Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 10 na kinara Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC mwenye 11.

Idadi hiyo ya mabao ni kubwa zaidi tofauti na ya msimu uliopita kwani alimaliza na bao moja alilofunga wakati KMC ilipotoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Geita Gold katika mechi iliyopigwa Novemba 11, 2022 kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita.

Shentembo ni wazi anajitafuta upya na kwa kiasi kikubwa anaanza kujipata kutokana na uwezo anaoendelea kuuonyesha akifufua matumaini kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Abdihamid Moallin kuamini huenda akamaliza katika nne bora msimu huu.

Nyota huyo alianza kung’ara zaidi wakati akiichezea timu ya Toto African ya Mwanza msimu wa 2016-2017 alipofunga mabao 10.

Kiwango hicho kiliwavutia mabosi wa Azam FC waliomsajili msimu wa 2017-2018 ambapo hata hivyo mambo yalikuwa magumu kwake kwani aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara kisha akapelekwa kwa mkopo Biashara United ya mkoani Musoma.

Hata aliporudi baada ya mkataba wake wa mkopo kwisha bado alishindwa kuendana na kasi ya kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam kwani ilifikia hatua akapelekwa hadi timu ya vijana iliyokuwa chini ya Kocha Abdul Mingange.

Changamoto hizo hazikumfanya kukata tamaa kwani msimu wa 2019-2020 alijiunga na Mbao ya Mwanza na kufunga mabao 13 na kuanza kuzivutia timu mbalimbali zilizohitaji saini yake ingawa ilikuwa ni Yanga iliyomnasa msimu wa 2020-2021.

Maisha ya Yanga hayakuwa mazuri kwake ila bado aliendelea kujitafuta na huenda msimu huu ukawa bora zaidi kwake tofauti na mingine.

BADO TISA TU

Katika timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu ni tisa tu ambazo mshambuliaji huyo hajazifunga hadi sasa zikiwemo Tabora United, Yanga, Azam FC, Coastal Union, Singida Fountain Gate, Namungo FC, Dodoma Jiji, Ihefu na Mtibwa Sugar.

Mbali na hayo ila timu mbili amezifunga kuanzia mabao mawili akianza na Geita Gold aliyoifunga katika mchezo wa Septemba 30, mwaka jana wakati kikosi hicho kikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita.

Machi 2, mwaka huu akairudia tena Geita Gold baada ya kufunga bao dakika 56 kufuatia Yusufu Mhilu kuwatanguliza wenyeji dakika ya 45 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na kumalizika kwa timu hizo kufungana 1-1.

Timu nyingine aliyoifunga mabao mawili nyota huyo msimu huu ni Simba wakati zilipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Desemba 23, mwaka jana na kufungana 2-2, huku yale ya wageni yakifungwa na Saidi Ntibazonkiza na Jean Baleke.

Kitu cha kufurahisha kwa nyota huyo, hana hata bao moja la penalti jambo linalomuweka kwenye mazingira mazuri endapo tu itatokea hadi mwisho mwa msimu watafungana idadi sawa ya mabao na wengine kutokana na mabadiliko yaliyofanywa ya kanuni.

Kanuni ya 13 ya Ligi Kuu Bara kuhusu tuzo ya ufungaji bora inaeleza endapo itatokea wachezaji zaidi ya mmoja kufungana kigezo kitakachotumika ni kuangalia mabao yaliyofungwa kawaida yatakuwa na alama mbili huku ya penalti yakipewa moja tu.

Kutokana na kigezo hicho, hadi sasa katika mabao yote manane aliyoyafunga mshambuliaji huyo tayari ana uhakika wa alama 16 jambo linaloweza kumpa faida zaidi endapo watafungana na wenzake kwa sababu ya kutokuwa na bao lolote la penalti.

KAULI YA MOALLIN Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin anasema moja ya jambo kubwa analolipenda kwa nyota huyo ni jinsi anavyofanya kazi na wachezaji vijana.

“Licha ya sifa yake ya kufunga ila amekuwa mfano bora kwa wachezaji wengi vijana waliopo hapa hivyo sisi kama benchi la ufundi tunajivunia, naamini akiendelea na kiwango hiki alichokuwa nacho atafanya vizuri kwa kushirikiana na wenzake."

Chanzo: Mwanaspoti