USAJILI wa Neymar Jr kutoka Barcelona kwenda PSG, Kylian Mbappe kutoka Monaco kujiunga na PSG, Phipippe Coutinho kuhama Liverpool kwenda Barcelona na Antoine Greizman kutoka Atletico Madrid hadi Barcelona ni sajili zinazoshika rekodi ya usajili wa bei mbaya duniani hadi sasa.
Sahau kuhusu hao, Ligi Kuu Bara inakaribia ukingoni na kuna wachezaji ambao wameuwasha moto na huenda katika dirisha kubwa la usajili wakaziingiza timu vitani zikitaka kunasa saini zao ili wakazitumikie.
Mwanaspoti linakuletea wachezaji wazawa wanaofanya vizuri msimu huu na huenda wakawa lulu wakati wa usajili unaotarajiwa kufunguliwa baada ya ligi kumalizika.
ABDULMAJID MANGALO
Msimu uliopita jina hili lilihusishwa kutakiwa na vigogo wa Kariakoo Simba na Yanga, lakini hadi dirisha la usajili lilipofungwa hakuna hata moja iliyonasa saini yake.
Beki huyu kisiki na nahodha wa Biashara United, msimu huu ameanzia alipoishia msimu uliopita kwani ameimarika na kuwa bora maradufu akiliongoza vyema chama la wanajeshi hao wa mpakani mkoani Mara.
Ubora wake katika kucheza mipira ya juu, mbio, nguvu na uwezo wa kuwapanga vyema mabeki wenzake ndizo sifa zake kuu zinazomfanya kuhitajika na timu nyingi msimu ujao na kuwa ghali sokoni.
DICKSON AMBUNDO
Ni winga tereza wa Dodoma Jiji ambaye hadi sasa moto wake ni wa kuotea mbali. Ambundo alijiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya alikowika kwa misimu miwili aliyoitumikia akitokea Alliance FC ya Mwanza.
Ambundo amekuwa miongoni mwa wachezaji tengemeo wa Dodoma Jiji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
Utulivu, ufungaji na utoaji pasi za mwisho umekuwa chachu ya kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mbwana Makata, jambo lililoifanya kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku ikifukuzia kimyakimya nafasi nne za juu.
YUSUPH MHILU
Kwenye kikosi cha Kagera Sugar utakutana na majina mawili ya Mhilu; mmoja ni Dickson Mhilu anayecheza eneo la ulinzi na mwingine Yusuph Mhilu anayeupiga kama mshambuliaji.
Hawa ni ndugu, lakini m-simu huu Yusuph ameonekana kuendelea kuonyesha makali ya kusakata vyema kambumbu kamaalivyokuwa akifanya msimu uliopita.
Hadi sasa Mhilu ameifungia Kagera Sugar mabao manane kwenye Ligi Kuu, jambo linalomuongezea thamani na kumuweka
katika orodha hii.
SEIF KARIHE
Huyu ni kinara wa upachikaji mabao Dodoma Jiji msimu huu akiwa na mabao manane hadi sasa.
Licha ya kuwa na ubora wa kupachika mabao, Karihe pia ameendelea kuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi hicho kwani hata asipofunga yeye hutoa mchango katika mabao mengine.
Nyota huyu ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar, alikulia kwenye akademi ya Azam FC na baada ya hapo alizitumikia Ruvu Shooting na Lipuli FC ambako hakung’ara kama ilivyo sasa akiwa Dodoma Jiji.
RAPHAEL DAUD
Mwanzoni mwa ligi msimu huu, Ihefu SC ilipambana kupata matokeo chanya pasipo mafanikio kutokana na wachezaji wengi iliokuwa nao kukosa uzoefu kwenye ligi.
Katika dirisha dogo la usajili, mabosi wa timu hiyo walifungua pochi na kuongeza wachezaji wapya akiwemo Raphael Daud Loth.
Kiungo huyu kabla ya kujiunga Ihefu aliwahi kupita Mbeya City na Yanga ambako pia alicheza kwa mafanikio.
Tangu ajiunge na Ihefu ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na amechangamsha dimba la kati na kuisaidia timu hiyo kupata matokeo chanya.
Haipingiki kuwa Loth ni miongoni mwa wachezaji bora ambao huenda majina yao yakatajwa sana kipindi kijacho cha usajili.
GUSTAPHA SIMON
Huyu ni mchezaji kiraka anayekitumikia kikosi cha Gwambina FC pale Misungwi mkoani Mwanza. Gustapha kabla ya kwenda Gwambina alikuwa timu ya vijana ya Yanga ambapo mara kadhaa alikuwa akicheza timu ya wakubwa na kutumika kama kiungo mkabaji akicheza vyema.
Mara nyingi Gwambina ameonekana akicheza eneo la beki wa kushoto anakouwasha moto kinoma. Ubora wake wa kubadilika na kuwa na uwezo wa kucheza mechi zaidi ya moja ndivyo vinamuongezea sifa ya kuwa mchezaji bora kwani timu nyingi siku hizi zinahitaji mchezaji anayeweza kubadilika kimbinu.
LUSAJO MWAIKENDA
Moja ya timu zenye safu ya ulinzi bora zaidi kwenye ligi ni pamoja na KMC ambayo eneo la beki wa kati amekuwa akicheza Lusajo Mwaikenda na Andrew Vicent ‘Dante’.
Lusajo alijiunga KMC mwanzoni mwa msimu huu kwa mkopo akitokea Azam FC ambako nafasi yake ya kucheza ilionekana kuwa finyu.
Tangu ajiunge na watoza ushuru hao wa Kinondoni, Lusajo ameimarika na kuonekana kuwa bora zaidi eneo la ulinzi.
Huenda dirisha la usajili, KMC na timu nyingine zikagongana vikumbo kwa matajiri wa Azam zikihitaji saini yake kwa msimu ujao.
Wachezaji wengine waliong’ara msimu huu na ambao dirisha la usajili litakapofunguliwa watakuwa midomoni mwa wadau wa soka ni Kibu Denis wa Mbeya City, Aaron Kalambo wa Dodoma Jiji, Erick Mwijage wa Kagera Sugar, Fuluzulu Maganga wa Ruvu Shooting, Deogratius Mafie wa Biashara United, Hasan Kapalata wa KMC na Miza Kristom wa Namungo FC.