Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazanzibar wawili wakaipa TFF Sh4 milioni

Fei X Mudathir Wazanzibar wawili wakaipa TFF Sh4 milioni

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Watoto wawili wa Kizanzibari wakaamua kutimiza masharti ya kuchelewa kuingia uwanjani katika muda wa kusalimiana kwenye mechi ya Yanga dhidi ya Azam, Oktoba 29 pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ni nani na nani? Ni viungo Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ wa Azam na Mudathir Yahaya Abbas wa Yanga ambao wakati wenzao wanapeana mikono wao kila mmoja alikuwa anamsubiria mwenzake aingie uwanjani kisha naye aingie.

Hadi walipomaliza kusubiriana kwao na kuamua kuingia, tayari muda wa kusalimiana ulikuwa umekwisha hivyo ambacho kingefuata kwao ni kanuni za ligi kufuata mkondo wake kwa Fei Toto na Mudathir kupewa adhabu na kamati ya usimamizi na uendeshaji wa Ligi Kuu kwa kupigwa faini ya milioni mbili kila mmoja.

Hakukuwa na chochote cha maana kilichosababisha wategeane kuingia uwanjani ambacho ukiwauliza wawili hao leo watakutajia zaidi ya imani za kishirikina tu ambazo zinabakia juu yao kama walitumwa na timu zao au wao wenyewe waliamua.

Baada ya hapo, wengi tulikaa mkao wa kula kusubiria ni uamuzi gani ambao ungechukuliwa na kamati ya usimamizi ambayo kwa jina ililozoeleka ni kamati ya saa 72 hasa ukizingatia baada ya mechi hiyo, Yanga ilipaswa kucheza mechi moja tu ya ligi kabla ya kuivaa Simba.

Kwa vile tukio kama hilo lilitokea msimu uliopita tena kwenye mechi ya dabi na wahusika Clatous Chama na Stephane Aziz Ki wakafungiwa mechi tatu zilizofuata na faini ya Shilingi 500,000 kwa kila mmoja, basi tukajua yatatokea pia kwa Mudathir na Fei Toto.

Lakini mambo yakaja kinyume na kamati ikawatoza faini ya fedha, shilingi 2 milioni kila mmoja lakini haikuwapa adhabu ya kuwafungia.

Kwa tuliosoma Cuba, tukaelewa kwamba kamati ingawa ilifuata kanuni, ilitumia busara tu kwa kuamua kuwatoza faini tu ili yule Mudathir asije kukosa dabi ikaonekana ikawapa cha kulalamika watu wa timu yake hasa ukizingatia upande wa pili hakukuwa na mchezaji aliyefanya kosa la kusababisha afungiwe na kukosa mechi hiyo hivyo hakukuwa na uwezekano wa kuifanya ngoma kuwa droo.

Sisi hatuna tatizo na kamati baada ya uamuzi wake na tunaipongeza kuwa wameshatupa cha kuhoji kesho ikiwa itatokea kosa kama hilo halafu wakatoa adhabu ya kufungia mtu au watu. Hapo tutawakumbusha risiti zao na tutawaambia ukweli kuwa hawatoi maamuzi ya haki na usawa.

Chanzo: Mwanaspoti