Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wayne Rooney kutua ulingoni

Rooney Boxer Wayne Rooney kutua ulingoni

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuona mambo hayaendi kwenye mpira wa miguu, mchezaji wa zamani wa Manchester United na England, Wayne Rooney anadaiwa kuwa kwenye mpango wa kutaka kubadilisha kazi na kugeukia ndondi.

Roooney mwenye umri wa miaka 38, amejaribu kufanya kazi ya ukocha kwenye timu kadhaa tangu astaafu lakini mambo yanaonekana kuwa sio mambo.

Hivi karibuni alifungashiwa virago na mabosi wa Birmingham aliyokuwa akiinoa baada ya timu hiyo kupata matokeo mabaya kwenye mechi 15.

Staa huyu anataka kugeukia mchezo wa ngumi aina ya Misfits Boxing ambao unaruhusu watu wa fani mbalimbali kushiriki na sio lazima mtu awe bondia rasmi,

Kwa mujibu wa tovuti ya Mirror, Rooney amefanya mazungumzo na promota wa kampuni ya KSI’s influencer boxing series, Kalle Sauerland ambao ndio waandaji wa mapambano ya aina hiyo.

Inadaiwa kuwa Rooney amefanya uamuzi huo lakini hataondoka moja kwa moja kwenye soka hivyo anafanya hivyo huku akisubiria kuona ikiwa atapata ofa ya kufundisha timu.

Rooney amekuwa shabiki mkubwa wa mchezo wa ngumi kwa muda mrefu. Mwaka 2015 tovuti ya The Sun iliripoti kwamba Rooney alipigana na mchezaji mwenzake wa Man United, Phil Bardsley, nyumbani kwake kabla ya Phil kudondoka baada ya Rooney kuachia mashambulizi makali.

Tukio hili lilionyeshwa kwenye moja ya video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii. Baada ya hapo Rooney alishangilia kwa staili ya kupiga ngumi kisha akadondoka baada ya kufunga bao kwenye mchezo dhidi Tottenham.

Mwaka 2007 Rooney alionekana akiongozana na mpiganaji Ricky Hatton nchini Marekani ambako Hatton alikuwa akienda kupigana na Jose Luis Castillo kwenye jimbo la Las Vegas.

Hii sio mara ya kwanza kwa Rooney kuhusishwa na masumbwi, anadaiwa kuwa aliwahi kumtumia ujumbe promota wa ngumi Eddie Hearn akimtaka amuandalie pambano.

KSI kwa sasa ina mwanachama mmoja ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa soka, Wayne Bridge ambaye mchezaji mwenzake wa zamani na Peter Crouch aliwahi kukiri kwamba Bridge ni mnyama anapokuwa uwanjani.

Masumbwi haya ya Misfits yamekuwa na watazamaji na wafuatiliaji wengi tangu kuanzishwa kwake kutokana na majina makubwa ya watu wanaopigana ikiwa pamoja na KSI na Logan Paul.

Ingawa kuingia kwa Rooney, kunaweza kuwapa umaarufu zaidi kutokana na ukubwa wa jina lake kwenye anga la mpira wa miguu.

Tangu afukuzwe na Birmingham, Rooney amerejea jijini Manchester na familia yake na tetesi zikadai kwamba anafikiria kutimkia nchini Saudi Arabia kufundisha ingawa hadi sasa hakuna kilichoendelea baada ya hapo.

Mbali ya Birmingham, Rooney aliwahi kuzifundisha DC United na Derby County.Rooney alipata kusema klabu yake ya utotoni ya Everton haikuwahi kumpigia simu kutaka awe kocha wake ndio maana hajawahi kuifundisha.

Chanzo: Mwanaspoti