Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamejipanga kukwepa hujuma zozote wanazoweza kukutana nazo ugenini baada ya kutuma mashushushu nchini Algeria kuweka mambo sawa kabla ya kikosi cha timu hiyo hakijaenda.
Wakati kikosi cha Young Africans kikitarajia kuondoka nchini kesho Alhamis (Juni Mosi), tayari uongozi wa timu hyo umeshawatuma viongozi wawili ambao tayari wapo Algeria wakiweka mambo sawa na kufuatilia nyendo za wapinzani wao hao.
Inaelezwa maamuzi ya kutuma mashushushu hao Algeria ni mapendekezo ya kocha Nasreddine Nabi ambaye alipendekeza mratibu wa timu hiyo Hafidh Saleh na mtaalamu wa uchambuzi wa video wa timu hiyo Mtunisia Khalil Ben Youssef kutangulia kuweka mambo sawa.
Mratibu wa timu hiyo, Hafidh amesema kuwa wamewasili nchini Algeria na tayari wameanza majukumu waliyotumwa.
Amesema moja ya majukumu yao ni kuhakikisha wanapata hoteli watakayofikia wachezaji na viongozi lakini pia kufahamu mapema uwanja watakaoutumia kwa mazoezi kuelekea kwenye mechi hiyo ya Juni 3.
“Hii mechi ni kubwa, nimekuja kuweka mazingira sawa kuhakikisha wachezaji hawapati shida wakifika, hali ya hewa ni ya kawaida iliyozoeleka kama ilivyo Dar es salaam,” amesema Mratibu huyo na kuongeza,
“Mpira wa Afrika una mambo mengi na hii ni fainali, kuja kwetu pia ni kuangalia namna ya kukwepa mitego yoyote ambayo wapinzani wetu wanaweza kutuwekea, lengo letu kwenye mchezo huu ni ushindi tu, tunataka wachezaji wetu akili yao iwe kwenye mchezo huu,” amesema Hafidh.
Kwa upande waKocha Nabi amesema amelazimika kutanguliza baadhi ya watu wake muhimu kwa kuwa anataka kuona wanafanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo huo ambao una umuhimu mkubwa kwao baada ya kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Mei 28).
“Nadhani kubwa kwetu kwa sasa ni mchezo huu, nataka wachezaji wangu waelekeza akili zao kwenye huu mchezo, tunaendelea na maandalizi kwa sababu kila mmoja anatambua na kujua tumekosea wapi hivyo tunahitaji kurekebisha kabla ya kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano, lakini kingine nataka timu ikifika Algeria isipate tabu yoyote, akili iwe kwenye mchezo, naamini tuliowatanguliza Algeria wataweka mambo sawa,” amesema Nabi.
Nabi, amesema bado hawajakata tamaa ya kuukosa ubingwa kwa kuwa wana dakika nyingine 90 za kurekebisha mambo. “Kufungwa kwetu nyumbani kumetusikitisha lakini bado hatujakata tamaa, tuna nafasi ya kufanya vizuri na kwenye mpira hakuna kinachoshindikana, tunaenda Algeria kwa lengo la kupambana na kubadilisha matokeo, hili linawezekana.” amesema Nabi