Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili Mbeya City kuikosa Coastal, Chipo aja na mbinu mpya

Watatu Wawili Mbeya City kuikosa Coastal, Chipo aja na mbinu mpya

Sat, 12 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji wa Mbeya City Eliud Ambokile na Joseph Ssemuju wataikosa mechi ya kesho Novemba 13 dhidi ya Coastal Union itakayopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa huku makocha wa timu hizo wakieleza mbinu za kushinda mchezo huo.

Mbeya City na Coastal Union zitakuwa uwanjani kesho Jumapili kumaliza kiporo chao, mechi itakayopigwa saa 8 mchana huku kila upande ukiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mechi iliyopita uwanjani hapo.

City ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Namungo, huku Wagosi wakiifumua Tanzania Prisons mabao 2-0 na kesho Jumapili wababe hao wataumana kuwania alama tatu muhimu na kujiweka pazuri zaidi kwenye msimamo.

Hadi sasa Mbeya City wamekusanya pointi 15 na kukaa nafasi ya tano baada ya mechi tisa, huku wapinzani hao wa jijini Tanga wakivuna pointi 11 na kuwa nafasi ya 11 baada ya mechi nane.

Kocha Msaidizi wa City, Anthony Mwamlima amesema timu hiyo itawakosa wachezaji Ambokile na Ssemuju wenye majeraha baada ya mechi iliyopita.

"Ligi ni ngumu kila timu inaweza kushinda popote nyumbani au ugenini, Coastal tumewaona ubora wao ila tumejipanga kushinda na kuendelea kuwa nafasi za juu" amesema Mwamlima.

Naye Nahodha wa timu hiyo, Paul Nonga amesema licha ya wapinzani kuonesha ubora katika mechi yao iliyopita, lakini wanaweza kufungwa akieleza kuwa benchi la ufundi limewanoa vyema na kesho watafanya kweli.

",Wanafungika, kimsingi ni sisi wenyewe wachezaji kutekeleza vyema maelekezo ya benchi la ufundi na tunaamini tutashinda," amesema Nonga.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Yusuph Chipo amesema kesho ni mechi ya mbinu kutokana na City kuwa tinu bora ambayo imefululiza matokeo mazuri hivyo lazima wajiandae vyema zaidi ya mchezo uliopita.

"Na sisi tunakuja na mbinu mpya, kwa sababu tunaona wapinzani walivyo mechi itakuwa ngumu sana ila mashabiki wetu watarajie mazuri na watusapoti, ushindi wetu ni ushindi wao" amesema Chipo.

Chanzo: Mwanaspoti