Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawa achora tatoo ya Sh1 milioni

Wawa Na Ndemla 1080x640 Pascal Wawa akiwa mazoezini na Kikosi cha Singida Big Stars

Wed, 26 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukisema cha nini wenzako wanasema watakipata lini na ndivyo ilivyokuwa kwa aliyekuwa beki wa Simba, Pascal Wawa kwani wakati timu hiyo ikiwa inamchukulia poa basi Singida Big Stars ilikuwa na hesabu zao.

Wawa kwa sasa yupo katika kikosi cha Singida na ameendelea kupewa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza huku akiiwezesha timu hiyo kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Mwanaspoti lilifanya nae mazungumzo kwa kina juu ya maisha yake ya Simba hadi kufikia kusiani mkataba wa kucheza katika kikosi cha Singida Bs licha ya mashabiki wengi wakitarajia kusikia ameondoka nchini.

ATENGENEZA REKODI SIMBA

Wawa anasema kitu ambacho anajivunia katika soka la Tanzania ni kutengeneza rekodi akiwa na Simba ya kuifanya timu hiyo kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wawa anasema anajivunia na rekodi hiyo kwa sababu ni takribani miaka 15 klabu hiyo haikuweza kufika kwenye hatua ya robo fainali kwahiyo akiwa sehemu ya wachezaji ni fahari kwake.

“Kama mchezaji najivunia sana rekodi ya kufanya Simba icheze robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita miaka mingi, rekodi nzuri kwangu na kwao;

“Nikiwa pale pia kwenye miaka minne nimebeba kila kitu kwa hiyo ni jambo zuri kwangu kwa sababu makombe yote ya ndani nilichukua nikiwa na Simba.”

3-0 ZA GALAXY ZILIMPA CHAMOTO

Wawa anasema katika miaka yake minne akiwa na Simba kitu ambacho hawezi kusahau ni mechi ya marudiano kati yao na LA Galaxy mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa.

Beki huyu anasema matokeo hayo yalimfanya atukanwe sana katika akaunti yake ya Instagram jambo ambalo lilimfanya alie takribani siku tatu huku akiwa hatoki nje.

“Nakumbuka kule Afrika Kusini tulishinda 2-0, nyumbani hapa tukafungwa 3-0, wengi walidai lile bao la kwanza nimefungisha lakini haikuwa hivyo basi mashabiki walinitukana sana;

“Kwenye ukurasa wangu wa Instagram walinitukania mama yangu, nilibaki nalia tu ndani, Mkude (Jonas) na Erasto (Nyoni) ndio walikuwa wananipigia simu na kunipa pole na muda mwingine walitamani tuwe wote lakini mimi nilikuwa nakataa sitaki kutoka nje.”

DABI KWAKE HAIMUUMIZI KICHWA

Wawa ndani ya miaka minne ni miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza dabi nyingi wakiwa na kikosi cha Simba lakini yeye mwenyewe anakiri mchezo huo hauwi mgumu kama mechi zingine.

Anasema mechi za dabi siku zote huwa hazichukulii kwa ukubwa sana kwa sababu anajua timu zote zinaenda kucheza mpira mzuri na wa ushindani tofauti na wanapokutana na timu nyingine.

“Mimi upande wangu dabi huwa naona mechi nzuri na ya kawaida kwa sababu wote tunaenda kucheza mpira, hakuna timu ambayo inakuwa inajilinda kwenye huu mchezo;

“Ukicheza na timu ndogo kiukweli mechi inakuwa ngumu kwa sababu huwa wanakamia sana na kila mmoja anataka kuonekana ili aweze kusajiliwa.”

Wawa anaongeza;”Kwangu kwa hiyo dabi ni kitu cha kawaida kwa sababu wote tunacheza mpira na sio kukamiana kupitiliza kama ukicheza na timu ndogo.”

“Nakumbuka niliwahi kucheza dabi huku nimeumia lakini bado nilifanya vizuri, hakukuwa na mtu yeyote nje ya Simba ambaye alikuwa anajua hilo.”

TUKIO LA PABLO AMUACHIA MUNGU, UCHEBE SAFI

Wawa anasema makocha wote ambao wamemfundisha akiwa Simba ni wazuri lakini kamwe hawezi kusahau tukio ambalo alifanyiwa na kocha Pablo Franco la kusukumizwa huku akiwa anajiandaa kuingia uwanjani.

Beki huyo anasema tukio lilehakufurahishwa kama baba ambaye ana watoto na huwa wanamuangalia akiwa anacheza lakini alimuachia Mungu.

“Nakumbuka Matola (Seleman) aliongea na kocha mkuu wakaninyanyua niende nikapashe misuli na wao wenyewe ndio waliniita ili niingie;

“Jina langu lishapelekwa na meneja ili niingie, nafika pale kocha anageuka nyuma ananiangalia halafu ananisukuma kama mtoto, kama unakumbuka nilishangaa kwa kumuangalia kisha niliinama na kuondoka,”anasema Wawa huku akisikitika.

Beki huyo anaongeza akisema;” Baada ya tukio lile hakukuwa na kiongozi mwingine zaidi ya Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye alimpigia simu na kumuuliza nini kilitokea ndani ya uwanja.”

Wawa anasema kwake yeye kocha wake bora ni Patrick Aussems kwa sababu alikuwa anazungumza na wachezaji mara kwa mara na kubwa zaidi ni kutaka kazi yake iende vizuri.

“Tulipenda kumuita Uchebe, alikuwa rafiki na anasikiliza wachezaji lakini kwake kubwa zaidi ni umfanyie kazi yake vizuri ndani ya uwanja, hanaga shida na mtu.”

ATAKA KUCHOMOKA SIMBA

Wawa anasema licha ya kuwa na wakati mzuri alipojiunga na Simba, ghafla mambo yalibadilika na akawa anataka kutoka kwenye timu hiyo ili aende sehemu nyingine.

Wawa anakiri hakuwa kwenye wakati mzuri na kocha hata baadhi ya viongozi hivyo hali hiyo ilimfanya asiwe na Amani hadi kufikia kusugua benchi kabisa.

“Huwezi kuamini baadhi ya viongozi nikiwa namalizia msimu walikuwa wanataka niongeze hata mwaka mmoja lakini mimi moyo wangu ulikuwa mgumu;

“Niliwaambia marafiki zangu, Erasto (Nyoni) na Mkude (Jonas) kwamba mimi siwezi kubaki Simba tena kwa namna ambavyo maisha yalivyobadilika.”

MISSED CALL 20 ZAMPELEKA SINGIDA BS

Wawa akiwa hana amani kwenye kikosi cha Simba, anasema kwenye mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City baada ya kumalizika alikuta simu yake imepigwa mara 20.

Wawa anasema alikuwa anatakiwa kuondoka baada ya mchezo huo kumalizika hivyo aliwasha gari lake na kutaka kuipotezea kabisa simu hiyo lakini ikatumwa meseji kwamba ni muhimu akikuta simu hizo apige.

“Baada ya kuona meseji ile nilipiga simu kiukweli na kumbe alikuwa ni bosi wa Singida, aliniambia yupo maeneo karibu na uwanja wa Mkapa hivyo anataka tuonane, nilikataa kwa sababu ndege yangu ilikuwa inaondoka usiku ule ule ila aliniambia ni muhimu kuonana;

“Niligeuza gari na kwenda kuonana naye, nilivyofika aliniambia ananihitaji kwenye timu yake akanipa na mkataba na mimi nikautuma kwa wakala wangu alivyoangalia aliniambia nisaini na nilisaini miaka miwili kisha nikasafiri.”

SINGIDA MTEGO KWAKE, ATOBOA

Wawa anasema uwepo wake Singida ni kama mtego kwake kwa sababu anajua kabisa watu wengi wakati anaondka Simba walikuwa wanamuona kama amechoka lakini kwa sasa hawazungumzi tena hayo.

“Hapa ni pagumu kuliko Simba kwa sababu hii timu imetoka Championship kwa hiyo inataka kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu na nashukuru kwa kiasi chake tumefanikiwa kuifanya iwe vizuri;

“Kufanya kwake vizuri watu hawazungumzi kabisa lakini kama ingefanya vibaya halafu na mimi nipo hapa ungesikia si unaona ndio maana Simba ilimuacha Wawa.”

Wawa anasema hayupo kwenye kikosi cha Singida kwa ajili ya kushindana kwa sababu tayari alishapita katika nyakati hizo bali kwa sasa anacheza ili aisaidie timu.

“Nisipocheza basi najua kabisa sipo kwenye mipango ya timu na hilo tayari liliwahi kutokea nilikuwa sichezi wakawa wanacheza wengine, kawaida kwenye maisha ya mpira.

AMVUTA KAGERE SINGIDA BS

Kama ulikuwa unajua Meddie Kagere ni kama vile imekuwa ghafla kwake kwenda Singida ni uongo bali ni pande tu ambalo alipigiwa na Wawa baada ya kuwa na nyakati nzuri walipokuwa Simba.

Wawa anasema awali Kagere alimuambia hali ambayo anaipitia Simba ikiwemo kwenda kwenye maandalizi ya msimu mpya huku akiwa hana mkataba hivyo ilipotokea nafasi alifanya wepesi kwa mwenzake.

“Kwa hiyo katika yote hayo nilipoambiwa kuhusu mshambuliaji kuhitajika hapa moja kwa moja niliwapa jina la Kagere, haikuwa rahisi kwao kuamini kama angekuja;

“Nilimpa namba meneja Nizar (Khalfan) akaongea naye kila kitu baada ya hapo yeye (Kagere) aliniuliza mimi mazingira ya hapa nikamwambia aje tufanye kazi na ndio maana yupo hapa.”

Wawa anaongeza akisema;” Mimi na yeye sio washikaji sana lakini huwa tunapigiana simu, huku Singida pia tunaishi karibu kwa hiyo nisipomuona lazima nimpigie na yeye asiponiona ni hivyo hivyo.”

BONASI MZUKA

Wawa anasema suala zima la bonasi kwenye timu ni huwa inaongeza hali ya wachezaji kupambana hivyo jambo zuri kwake ni kuona suala hilo likiendelea kwa timu nyingi ndani ya ligi.

Beki huyo anasema wakati akiwa Simba bonasi ilikuwa inachangia kwa kiasi kikubwa wachezaji kupambana kwa sababu wanajua kuna kitu ambacho wanakipigania.

“Kule bonasi zilikuwa ni kubwa sana kwa sababu ukweli Simba ni timu kubwa, hapa ni Singida na timu ndogo ambayo imepanda msimu huu kwahiyo nakubaliana na ninachokipata;

“Simba kulikuwa na bonasi ya timu lakini bado kiongozi anaweza kukupigia simu na kukuambia ukipambana ili timu isifungwe basi kuna bonasi yako nyingine, hilo lilikuwa kawaida.

Wawa anasema aliwahi kupata pesa ambayo ni kama usajili wa mchezaji katika bonasi ya mechi moja tu ya Ligi ya Mabingwa na yeye mwenyewe hakuamini.

“Iliingia ile bonasi ya timu kama timu halafu ikaingia na bonsai ambayo niliambiwa iwapo tusingefungwa, huwezi amini nilipagawa kwa sababu ela ilikuwa nyingi, nilipiga simu hadi benki ili wanielezee maana kule huwa inaandikwa sababu ya pesa kuingia.”

AZITAJA TIMU ZILIZOMPA UTAJIRI

Wawa anasema katika maisha yake ya soka alishika pesa nyingi sana katika timu ya Al Mereikh (Sudan) pamoja na Azam FC (Tanzania) na ndio sehemu kubwa iliyobadilisha maisha yake.

Beki huyo anasema alianza kucheza Al Mereikh na alisajiliwa kwa pesa nyingi sana ambazo hawezi kuzitaja lakini hata kutoka kwenye timu hiyo na kuja Azam bado alisajiliwa kwa pesa nyingi.

“Ndugu yangu pesa zilikuwa nyingi ambazo zilinibadilisha (Alizitaja lakini hakutaka ziandikwe), Azam ilitoa na hata nilivyorudi kule tena Al Mereikh nilipata pesa nyingi,” anasema Wawa.

“Kiukweli najivunia soka kwa sababu nina viwanja vingi kule nyumbani Ivory Coast na vyote nimepata kupitia pesa yangu ya usajili, vipo vingi na vipo sehemu ambayo ni ya thamani.”

Wawa anasema ;”Nikiwa na Al Mereikh tulishinda ubingwa wa Ligi Kuu kwahiyo yule mwenye timu alinipa ahadi ya kwamba kama tunafanikiwa atanipa saa yake ya thamani na alinipa ipo nyumbani, pia nilijenga nyumba zangu kupitia hizo pesa za usajili.”

SOKA LA SUDANI NGUVU NYINGI

Wawa ambaye ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Sudan na hapa Tanzania, anasema soka la hapa kuna muda halitumii nguvu nyingi tofauti na Sudan.

“Sudan soka lao ni nguvu nyingi, wakisema wanakukaba ni unakaba muda wote lakini hapa ni tofauti kwa sababu mpira unachezwa kabisa tofauti na kule;

“Kule Al Mereikh ikiwa inacheza na timu ndogo asee ni unakabwa mwanzo mwisho, hii nayo hapa nakumbuka nikiwa Azam ilikuwepo lakini kwa sasa imebadilika kidogo.”

SIRI YA YEYE KUDUMU

Wawa anakiri yeye ni mtu mzima kwa sasa lakini kinachomfanya aweze kuendana na presha ya mechi za Ligi Kuu ni kutokana na kulitambua hilo na kujipa muda wa kupumzika.

Anasema ukijijua ni mtu mzima inabidi upate muda mwingi wa kupumzika na kuepuka vitu visivyokuwa na lazima hivyo itakufanya uendelee kucheza muda mwingi.

“Mpira ukiacha mwili upumzike kwa muda mrefu lazima nguvu zirudi ambazo ulizitumkia kwenye mazoezi, kwa hiyo mimi nafanya hivyo kiukweli na pumzika sana;

“Ukiwa mtu mzima kama mimi halafu ukawa unakunywa pombe sana, wanawake wengi kiukweli hautoweza kucheza mpira kwa sababu utakuwa unatoa nguvu nyingi mwilini halafu hupati muda wa kupumzika.”

TATOO ZAKE MAMILIONI, ASIMAMISHA KUCHORA

Mwili wa Wawa umejaa Tatoo kila upande kuanzia kwenye shingo yake hadi kwenye miguu. Muandishi wa Makala hii alimuuliza ni gharama gani ambayo ambayo ametumia kwenye kuchora Tatoo zake alisema ni nyingi kiasi ambacho hakumbuki kwa sasa.

“Hii Tatoo yangu ya mkono wa kushoto nakumbuka nilitumia masaa manne kuichora na nililipa sh 1 milioni, hizi zingine sikumbuki sana kiukweli ila nazo nilitumia pesa;

“Mke wangu na mama wanapenda sana Tatoo kwa hiyo ndio maana nikawa nachora lakini sasa nimeona zimekuwa nyingi mwilini mwangu na nimeamua kuacha.”

ISHU YA KUKAA KAMBI

Wawa hapa nchini amecheza tayari timu tatu na Sudan moja, kwenye upande wa wachezaji kukaa kambini kila timu ina utaratibu wake na yeye mwenyewe anakiri hilo.

Anasema kwa upande wa Singida Big Stars kuingia kambini ni siku mbili kabla ya mchezo, lakini Sudan huwa ni siku moja kabla ya mchezo.

“Hapa hakuna tofauti kubwa sana kati ya Simba na Singida, labda upande wa Azam, nakumbuka tukiwa Simba ni siku tatu kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa lakini kwenye Ligi ni vile vile huwa labda siku mbili;

“Kambi ni nzuri kwa sababu wachezaji mnakuwa pamoja lakini haitakiwi sasa kukaa kwa muda mrefu.”

NJE YA UWANJA

Wawa anasema anapokuwa amemaliza majukumu yake ya uwanjani mfano ligi imeisha huwa hafikirii kabisa masuala ya uwanjani badala yake akili ni kwenye kupumzika.

Beki huyo anasema hayo ni kwa sababu huwa anatumia nguvu nyingi ndani ya uwanja hivyo anapopumzika anapata akili mpya ya kufanya mambo ya maendeleo yake.

“Mimi nikiwa nje ya uwanja kwanza napenda kwenda ufukweni, nasahau kabisa mpira, mpira ujue ni mgumu kwahiyo kuna muda lazima upumzike;

“Pia napenda sana kula vyakula vizuri kwa hiyo nikiwa mwenyewe naenda migahawa mikubwa nakula ninachokitaka na wakati mwingine kuangalia muvi.”

Chanzo: Mwanaspoti