Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawa: Huyu Bwalya ni mtu na nusu

Wawa Picdf George Wawa

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale akiyataja majeraha kama adui mkubwa wa wanasoka duniani, hali iko hivyo pia kwa beki wa Geita Gold, George Wawa (24), ambaye anasema kuna kipindi alitaka kuachana na soka kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Wawa ni kati ya mabeki ambao wamekuwa wakionyesha kiwango cha juu kwenye Ligi Kuu Bara na Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalumu na kufunguka kila kitu kuhusu maisha yake ndani ya soka na nje, na kusema kitu pekee ambacho kimemrudisha nyuma kwenye mafanikio ya soka ni kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara.

ALITOKEA WAPI?

Wawa, mzaliwa wa Singida, kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Geita Gold na ameliambia Mwanaspoti kwamba alianza maisha ya soka huko Babati akiwa shuleni na baadaye kujiunga na moja ya timu ya mtaani, baada ya kumaliza shule kisha alijiunga na Akademi ya Ruvu Shooting baada ya kuona uwezo wake na hapo ndipo safari yake Ligi Kuu ikaanza rasmi.

“Nilivyokuwa Babati nilipata nafasi ya kwenda U-20 ya Ruvu Shooting na pale nilikutana na wachezaji wengi, lakini nilipambana na ndani ya msimu mmoja nilipandishwa timu kubwa na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2018/2019.

“Nilicheza Ruvu na baadaye nikahamia Singida United. Kote huko nilikuwa nikicheza na baadaye nilisajiliwa na Dodoma Jiji na msimu uliopita nikajiunga na Geita Gold ambayo nipo hadi sasa,” anasema nyota huyo ambaye huu ni msimu wake wa tano akiwa Ligi Kuu.

AMERITHI KWA BABA

Akizungumzia zaidi kuhudu soka, anasema: “Binafsi napenda. Nilianza kucheza nikiwa mdogo. Nilikulia kwenye familia ya soka. Baba yangu alipata ajira kwa ajili ya mchezo huu na alikuwa anaupenda na aliamini nina kipaji kwa hayo yote yalichangiwa na upenzi wa soka,” anasema Wawa.

“Hata hivyo, kama unavyojua kuna baadhi ya watu kwenye familia walikuwa hawaamini kama soka litanilipa, lakini baba yangu alinipambania na namshukuru sana kwa hilo.”

SOKA LINALIPA KINOMA

Mchezaji huyo anasema mchezo huo unawalipa sana wanaouheshimu kama kazi na hapa anasema: “Vijana wengi wa sasa wanaamini soka ni ajira inayoweza kuwalipa vizuri na kutimiza mahitaji na ndoto zao.

“Nashukuru Mungu kwa ninachopata kupitia kazi ya miguu yangu maana sio haba kwa soka letu na inanipa moyo wa kupambana zaidi nikiamini ipo siku nitapata kikubwa zaidi. Hata sasa bado naona mafanikio makubwa.”

HATAISAHAU 2020/2021

Nyota huyo anayesifika kwa kumwaga maji, anasema pamoja na kuwa na kiwango bora, lakini hatausahau msimu wa 2020/2021 akiwa Dodoma Jiji kwani alitoa asisti saba na kufunga bao moja.

“Msimu wa 2020-21 ulikuwa poa sana kwangu na sitausahau kwani nilikuwa na nafasi kubwa kikosi cha kwanza na niliisaidia timu kwa kutoa pasi za mwisho saba na kufunga bao moja.

“Unaweza kuona ni kitu cha kawaida, ila kwangu ni kikubwa zaidi kwani sio rahisi kwa beki kutoa pasi nyingi za mabao namna hiyo,” anasema Wawa mwenye asisti mbili hadi sasa msimu huu akiwa ni miongoni mwa mabeki watano wa Ligi Kuu wenye asisti kuanzia mbili na kuendelea.

BILA SOKA MAMBO YANGEKUWA MAGUMU

Wakati mastaa wengi wakiwa na mipango mingine nje ya soka, Wawa anasema hadi sasa haelewi iwapo bila soka maisha yake yangekuwaje kwani alianza kuwa na matumaini na mchezo huo tangu akiwa mdogo.

“Isingekuwa soka sijui ningekuwa nani maana kwenye maisha mambo yanatokea bila wewe kujua. Nadhani na kwangu ingekuwa hivyo kwani nilikwa mdogo, lakini nashukuru nipo hapa,” anasema.

BWALYA BALAA

Wawa yupo tofauti na baadhi ya wachezaji wengine ambao mara nyingi ukiwauliza mchezaji gani umnamkubali watakuambia staa anayecheza eneo sawa na lake, lakini beki huyu wa kulia anamkubali kiungo wa zamani wa Simba, Rally Bwalya anayekipiga kwa sasa Amazulu ya Afrika Kusini.

“Wapo wengi ninaowapenda na kuwakubali namna wanavyocheza, lakini Bwalya nafurahia zaidi anavyocheza kwa sababu anajua na anafanya soka kuonekana mchezo rahisi yaani anacheza kama hachezi kumbe ndio anacheza, kiujumla ni mtaalamu haswa,” anasema.

ALIA WABONGO NJE

Soka la Bongo limekua na wachezaji wa kigeni wamekuwa wengi na wanafanya vizuri zaidi, lakini kwa upande wa wachezaji wa ndani sio wengi ambao wameenda kucheza nje.

Beki huyo anaeleza namna ugumu ulivyo wa wachezaji kwenda nje kwani mipango ya kutengeneza wachezaji bora watakaowakilisha soka nje bado haijakaa sawa.

“Sioni kama tumekwama ila ni mipango ya soka letu ilivyo. Sioni kama kuna mipango mingi ya kwenda kucheza kimataifa kama wenzetu. Sisi mifumo yetu bado haiko vizuri na ni ngumu kwenda nje kama mipango haijanyooka. Inawezekana wachezaji kwenda nje kwa wingi, lakini kwanza tuweke sawa miongozo na mipango kwenye soka la Tanzania,” anasema Wawa.

MAJERAHA YANAMKWAMISHA

Nyota huyo anateswa na tatizo ambalo kila mchezaji ni nadra kulikwepa, nalo ni lile la majeraha. “Binafsi majeraha yalishawahi kunipa changamoto mpaka nikahisi soka tena basi na matokeo yake huwa ni mabaya kwa mchezaji, “ anasema.

“Hadi sasa naogopa sana kuumia kwa sababu najua msoto wake, ukikaa nje unapoteza vitu vingi na ni kazi kurudi uwanjani kwa kiwango bora kama uliumia sana.

“Kila nikiwa na majeraha napata sana mawazo ya hovyo, kuna muda najikatia tamaa kabisa lakini nashukuru watu wa karibu wananipa moyo na kunisapoti kwa kila kitu na baadaye nakuwa sawa.”

NDOTO KIBAO

Kila mtu katika maisha ana ndoto zake ambazo anataka kuzitimiza na kufurahia, vivyo hivyo kwa Wawa na hapa ameliambia Mwanaspoti ndoto zake ni kubwa na bado anazipambania.

Wawa anasema anaiona nafasi yake ni kupambania ndoto kubwa alizonazo na ndiyo maana anaendelea kupambana ili aweze kuzifikia, ila kwa wakati kwani safari bado ni ndefu na anatamani kucheza kwa mafanikio timu ya taifa na kufika mbali ngazi ya klabu.

“Naendelea kupambana hadi mwisho bila kuchoka. Ndoto zangu ni kufika mbele zaidi ya hapa kwa ngazi ya taifa na klabu. Bado sijafika kabisa lakini naamini katika safari yangu na ipo siku nitakuwa pale ninapopataka,” anasema mchezaji huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live