Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watunisia wa Yanga watua na mchecheto

Watunisia Pic Watunisia wa Yanga watua na mchecheto

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga kimerejea jijini Dar tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Club Africain ya Tunisia ambayo imetua jijini kimyakimya, huku ikiwa na mchecheto, lakini Kocha Nasreddine Nabi na Fiston Mayele wakiicheza kijanja mechi hiyo.

Yanga itakuwa wenyeji wa Watunisia hao ambao waliamua kutua kimyakimya kwa kile kilichoelezwa hofu waliyonayo dhidi ya Yanga, kabla ya mechi hiyo ya kwanza wa play -off ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa kesho Uwanja wa Benjamini Mkapa kabla ya kurudiana wiki ijayo.

Inaelezwa mabosi wa Yanga walishtukizwa juu ya ujio wa wageni wao hao, huku wakitafuta chimbo la pekee yao kuisubiri mechi ya Jumatano ambayo mastaa wa Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kung’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan wamedai wanajua presha iliyopo mbele yao na wameshajipanga mapema.

Nabi alisema maandalizi ya mchezo huo wa kwanza nyumbani yalianza mapema mara baada ya kucheza mechi ya Dabi dhidi ya Simba, hivyo hana presha na mchezo huo.

Nabi alisema baada ya kumalizana na mchezo huo mkubwa nchini alitenga muda wa kutosha kuiangalia Club African inacheza kwa mbinu za aina gani inapokuwa ugenini ili kuwa bora zaidi yao.

Alisema hawana muda wa kutosha kufanya maandalizi kwa mechi hiyo ila kwenye kuifuatilia Africain kuna vitu vya kiufundi wameviona wanavifanyia kazi ili kuhakikisha wanashinda ushindi mnene.

“Ligi ya Mabingwa Afrika tulishindwa kufanya vizuri kwa kukosa matokeo bora nyumbani safari hii tumejipanga kupata matokeo bora mchezo huu wa kwanza ili kujihakikishia nafasi ya kumaliza kazi ugenini,” alisema Nabi na kuongeza;

“Baada ya kucheza na Simba tuliwapumzisha baadhi ya wachezaji kwenye michezo dhidi ya KMC na Geita Gold ndio maana kuna wakati tulishindwa kucheza kwa ubora.”

“Malengo yetu ni kwenda hatua ya makundi na hilo naamini linawezekana kutokana na hamu kubwa iliyopo kwa wachezaji wangu huku kila mmoja akitamani kufanya vizuri ili kutimiza hitaji letu.”

Yanga mechi mbili zilizopita baada dhidi ya Simba, ilipangua kikosi cha kwanza kwa kufanya mabadiliko kwa baadhi ya nyota wakianzia benchi kama, Fiston Mayele, Djuma Shaban, Yannick Bangala, Stephane Aziz KI, Feisal Salum na Tuisila Kisinda.

MAYELE AKOLEZA MOTO

Juu ya mechi hiyo Mayele kwa upande wake alisema wanajua wanacheza na timu ya aina gani na tayari wameshaanza kuisoma ili kuimaliza nyumbani kabla ya kumalizia kazi ugenini.

Mayele alisema faida kubwa ambayo Yanga inayo ni kwamba timu yao imeshacheza mechi nyingi za ushindani hususan ligi kitu ambacho kitawatofautisha na Africain ambao ligi ya kwao bado haijaanza.

“Tunatakiwa kufunga mabao ya kutosha, pia tusiwaruhusu kupata bao hapa, hii inahitaji umakini mkubwa, lakini tutahakikisha tunafanikisha hayo yote katika mechi ya hapa nyumbani,” alisema Mayele na kuongeza;

“Tunajua makocha wetu wanawajua vizuri kwa kuwa wametoka huko Tunisia, kitu ambacho kinaweza kututofauitisha sisi na wao ni kwamba timu yetu imeshacheza mechi kubwa za ushindani kuanzia ligi na kimataifa, wao tumeona ligi yao haijaanza kwa maana hiyo tunatakiwa kutumia nafasi hii vizuri.”

“Hii ni nafasi kubwa iliyosalia kwetu kulinda heshima yetu baada ya kutolewa na Al Hilal, tunatakiwa kuhakikisha tunashinda vizuri hapa nyumbani,”alisema Mayele aliyefunga bao pekee dhidi ya Al Hilal.

“Tunatambua itakuwa mechi ngumu kwa kuwa hii ni klabu kongwe, kila kitu kwetu kinawezekana kama tukijipanga sawasawa nawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi siku ya mechi.

Wakati Mayele akiyasema hayo beki wa timu hiyo Dickson Job alisema timu yao sio rahisi kufanya makosa mengine katika mechi dhidi ya Club Africain na kwamba watakabiliana nao kikubwa.

Job alisema kila mchezaji aliumia kwa hatua ya kutolewa na Al Hilal na kwamba tayari wameshasahau hayo na sasa wanataka kuhakikisha wanashinda vizuri nyumbani.

“Tunatakiwa kuwa makini katika mchezo huu, watu hawajui jinsi kila mchezaji alivyoumia katika zile mechi mbili, matokeo yale yametupa uzoefu mkubwa zaidi, hatutarudia makosa kama yale,”alisema Job.

Chanzo: Mwanaspoti