Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu wa kazi EPL hawa hapa

Chama La Pc Watu wa kazi EPL hawa hapa

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ndo hivyo. Chama cha Wanasoka wa Kulipwa wa Ligi Kuu England kimetaja Kikosi Bora cha Mwaka cha ligi hiyo, huku Arsenal iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita ikiingiza mastaa wengi kuliko timu zote.

Kikosi cha Arsenal chini ya Kocha Mikel Arteta kilizidiwa na Manchester City kwenye mbio za ubingwa siku ya mwisho ya msimu wa 2023/24 na kulikuwa na tofauti ya pointi mbili tu baina ya timu mbili za juu.

Kikosi cha Arsenal kilicheza kwa kiwango bora sana kwa karibu msimu mzima - hivyo ipewa zawadi hiyo ya kuingiza mastaa wengi kwenye kikosi bora cha mwaka na kuna wakali watano wa Emirates wamepata namba.

Wakati huo, mabingwa wa ligi hiyo, Manchester City yenyewe imeingiza wachezaji wanne tu, huku kukiwa hakuna mchezaji yoyote wa kutoka Manchester United, Chelsea wala Tottenham Hotspur.

Kipa, David Raya - aliyekuwa kwa mkopo Arsenal kabla ya kunasa jumla dirisha hili la majira ya kiangazi akitokea Brentford amemwengua Alisson wa Liverpool kwenye goli la timu hiyo bora ya mwaka Ligi Kuu England.

Pacha ya mabeki wawili matata kabisa Ligi Kuu England kwa msimu uliopita, William Saliba na Gabriel wote wamepata nafasi kwenye kikosi hicho wakiunda safu ya mabeki wanne sambamba na Virgil van Dijk wa Liverpool na Kyle Walker wa Man City.

Van Dijk, ambaye aliiongoza Liverpool kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu chini ya kocha Jurgen Klopp msimu uliopita, amewabwaga mabeki wawili wa mabingwa wa Etihad, John Stones na Ruben Dias katika kupata nafasi katika kikosi hicho.

Rodri wa Man City amesimama kwenye kiungo ya kati sambamba na wakali wawili wa Arsenal, Declan Rice na Martin Odegaard. Hiyo ni mara ya kwanza tangu mwaka 2019 kumshuhudia Kevin de Bruyne akishindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha mwaka. Yakijirudia ya mwaka jana ni klabu nne tu ndizo zilizoingiza wachezaji - Arsenal, Man City, Liverpool na Aston Villa.

Ni mara ya kwanza pia kwa Phil Foden na Ollie Watkins kutajwa kwenye kikosi hicho cha PFA, huku kila mmoja akiwa amefunga mabao 19 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.

Straika wa Man City, Erling Haaland ndiye mshambuliaji wa kati kwenye kikosi hicho na  mkali huyo akifanikiwa kuingia kwenye kikosi bora cha mwaka cha PFA kwa msimu wa pili mfululizo.

Staa Foden alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA, huku akiwa tayari alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka miezi mitatu iliyopita.

Staa wa Chelsea, Cole Palmer amechaguliwa kuwa Kinda Bora wa Mwaka, huku Haaland alishinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kufunga mabao 27.

Lakini, kilichoshangaza wengi ni kuona Palmer hayumo kwenye kikosi bora cha mwaka licha ya mkali huyo kufunga mabao 22 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita na jambo hilo limewaibua mashabiki kwenye mitandao ya kijamii.

Shabiki mmoja alisema: “Palmer hayumo. Hii ni hovyo kabisa.”

Mwingine aliuliza: “Inakuwaje Palmer hayumo?” Hivyo pia kwa shabiki wa tatu, aliyesema: “Palmer yuko wapi?” Na shabiki wa nne aliongeza: “Cole Palmer ameporwa.”

Mastaa wengine waliokosa nafasi ni Bukayo Saka, ambaye kiwango chake kilionekana kushuka kidogo mwishoni mwa msimu uliopita. Licha ya kuaminika na wengi kuwa mmoja wa mastaa matata kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England, De Bruyne alikosa mechi za mwanzoni mwa msimu kutokana na kuwa majeruhi. Hata hivyo alifanikiwa kufunga mabao manne na kuasisti mara 10 kwenye mechi 21 alizocheza.

Supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah ni mkali mwingine ambaye amekosa nafasi kwenye kikosi hicho. Mo Salah alifunga mabao 18 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita na kufikisha mabao 155 kabla ya kufunga bao la 156 alipofunga dhidi ya Ipswich Town Jumamosi iliyopita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live