Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu spesho chama la Mourinho

Jose Mourinho Portugal.jpeg Watu spesho chama la Mourinho

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

The Special One, Jose Mourinho ametaja kikosi cha kwanza cha wachezaji wake aliowahi kuwafundisha katika maisha yake ya ukocha.

Unaweza kudhani ni ngumu kiasi gani kutokana na kundi kubwa la wachezaji waliowahi kupita chini ya Mreno huyo, huku wengi wakiwa bora na kumpatia mafanikio makubwa. Lakini, kwenye wakali 11, Mourinho amechora kikosi hicho, chenye huduma ya mastaa wa maana kwelikweli, akiwamo Cristiano Ronaldo na Eden Hazard.

Hata hivyo, mashabiki wa Chelsea, walikasirishwa na Mourinho baada ya kuwaweka kando mastaa wao watatu, ambao wao wanaamini walipaswa kuwamo kikosini.

Mourinho, 60, alitaja kikosi chake hicho wakati alipofanyiwa mahojiano na kiungo wake wa zamani huko Stamford Bridge, John Obi Mikel kwenye kipindi chake cha Obi Wan, huku mahojiano hayo yote yakitarajiwa kuwekwa bayana kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu.

Hata hivyo, kwenye kikosi hicho Mourinho aliwataja wachezaji wanane aliofanya nao kazi Chelsea kwa nyakati mbili tofauti.

Petr Cech, John Terry, Ricardo Carvalho, William Gallas, Claude Makelele, Frank Lampard na Didier Drogba walijumuishwa kwenye kikosi hicho sambamba na Hazard.

Kwenye kikosi cha Inter Milan, Mourinho chaguo lake ni beki wa kulia Javier Zanetti, licha ya kwamba wakati ananyakua mataji matatu makubwa 2010 timu ilikuwa na wakali matata kama Samuel Eto’o, Diego Milito na Wesley Sneijder kwa uchache.

Ronaldo aliungana na Mesut Ozil kwa mastaa ambao Mourinho aliwanoa Real Madrid, huku akiwaweka kando mastaa kibao akiwamo kipa mahiri Iker Casilas. Beki Carvalho na Mourinho ni kama wamekuwa baba na mtoto, ambapo baada ya kushinda pamoja ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya walipokuwa FC Porto walikwenda wote Chelsea na baadaye wawili hao wote walipita Real Madrid. Kwenye kikosi hicho cha Mourinho, hakuna mchezaji yeyote wa Manchester United au Tottenham Hotspur licha ya kuwapo wakali kibao waliocheza chini yake akiwamo Paul Pogba, Zlatan Ibrahimovic, Harry Kane na Heung-min Son kwa kuwaorodhesha kwa uchache.

Mashabiki wa Chelsea walishtushwa na Mourinho kuwaweka wakali wao watatu Ashley Cole, Michael Essien na Mikel ambao wanaamini walikuwa watumishi hodari kabisa wa Mourinho katika kipindi chake alichokuwa Stamford Bridge.

Kwa sasa Mourinho anainoa AS Roma na huko hakumtaja mchezaji yeyote, lakini mashabiki wa Chelsea walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii, ambapo shabiki mmoja alisema: “Unamchagua Gallas mbele ya Ashley Cole ni uchizi.”

Mwingine aliongeza: “Gallas mbele ya Ashley Cole??? Kivipi?” Shabiki wa tatu alisema: “Sikubaliani naye kwenye beki ya kushoto. Naamini Ashley Cole alipaswa kuwa yeye.” Mwingine aliuliza: “Wako wapi Mikel na Essien?” Mourinho alishinda mataji manane kwa vipindi vyake viwili alivyokuwa Chelsea, ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu England mara tatu.

Na huu ni msimu wake wa tatu huko AS Roma, ambako alishinda ubingwa wa Europa Conference League mwaka 2022. Mourinho ni kocha mwenye maneno mengi na hakika kwa wachezaji waliopata nafasi kwenye kikosi chake cha muda wote ni wenye bahati kutokana na idadi kubwa ya wachezaji mahiri aliwahi kuwanoa kocha huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live