Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatushangaa! Rekodi, uzoefu kuzibeba nchi hizi Qatar

Camerron Qatar Wachezaji wa Kikosi cha Cameroon

Fri, 18 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya uwepo wa mataifa makubwa yanayopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Dunia, mwaka huu kuna nchi zingine ambazo hazitajwi sana, lakini huenda zikashangaza kwa aina ya mastaa ambao wapo katika vikosi vyao na uzoefu wao kwenye michuano mikubwa.

 Mataifa hayo yamekuwa yakishiriki mara kwa mara mashindano hayo, lakini mengi yamekuwa hayapati matokeo mazuri ingawa hiyo imekuwa ikiwajengea uzoefu unaoweza kuwa silaha kubwa kwenye michuano mwaka huu. Hapa Mwanaspoti linakuleta baadhi ya nchi ambazo hazitajwi kuelekea michuano ya mwaka huu, lakini zinaweza kushangaza.

SENEGAL

Ni moja kati ya nchi zinazobeba furaha ya nchi za Afrika, kwani mashabiki wengi wa soka kutoka bara hili wanaonekana kuipa imani ya kufanya makubwa.

Mbali ya staa wao Sadio Mane kupata majeraha, mmoja kati ya mastaa ambao wamekuwa wakifanya vizuri sana kwenye eneo la ushambuliaji ni Ismaila Sarr anayecheza Watford inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England.

Msimu huu tayari ameshafunga mabao sita na kutoa asisti tatu kwenye mechi 16 za michuano yote na akiwa na Senegal tangu 2017 amefunga mabao 10 katika mechi 47. Katika mechi za kufuzu amefunga mabao manne kwenye mechi tatu.

Mara kadhaa timu kubwa England zimekuwa zikiiwania huduma yake, lakini mabosi wa Watford wanagoma kumuuza.

Habib Diallo, anayecheza Strasbourg ya ufaransa anaweza kuwa tegemeo kwenye eneo la ushambuliaji kutokana na kiwango ambacho amekionyesha tangu kuanza msimu huu.

Kwa ujumla nyota huyo amecheza mechi 14 za Ligi Kuu Ufaransa na kufunga mabao matano akiwa ndiye mmoja kati ya washambuliaji tegemeo wa timu Strasbourg.

Boulaye Dia, huyu ni fundi mwingine ambaye huenda akaisaidia Senegal katika mashindano hayo. Msimu huu ameonyesha kiwango bora akiwa na Salernitana kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A), ambapo katika mechi 12 amefunga mabao matano na kutoa asisti mbili.

JAPAN

Hii itakuwa ni mara ya nane kushiriki michuano hiyo tangu ianze kushiriki na tangu 1998 haijawahi kukosa kufuzu mashindano hayo hadi leo.

Mafanikio makubwa ya Japan ni kufuzu hatua ya 16 bora mara tatu ambapo michuano hiyo iliyopita pia ilifanikiwa kufanya hivyo na bahati mbaya ilifungwa na Ubelgiji.

Kushiriki kwao mara nyingi kumewajengea uzoefu mkubwa ambao unaweza kuwa silaha kuwafanya wafanye vizuri kwenye mashindano mwaka huu.

Asilimia kubwa ya kikosi ambacho kilikuwepo nchini Russia 2018 ndicho ambacho kitakuwepo nchini Qatar kikiongozwa na nahodha Makoto Hasebe na supastaa Maya Yoshida ambao ni miongoni mwa mastaa wazoefu wa michuano hiyo na watakuwepo.

Pia kikosi kina kipa mkongwe Eiji Kawashima ambaye ana umri wa miaka 39. Mbali na wakongwe Japan pia imejaliwa kuwa na wachezaji vijana wanaofanya vizuri barani Ulaya kama Daichi Kamada ambaye msimu huu amefunga mabao 12 kwenye mechi 22 na msimu uliopita alichukua ubingwa wa Europa League akiwa na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani.

URUGUAY

Timu inaonekana kuwa itaweza kusumbua kwa sababu ya historia na aina ya wachezaji inayokwenda nao kwenye michuano hiyo. Taifa hilo lina historia ya kipekee kwani ndiko ilikofanyika michuano hiyo kwa mara ya kwanza, na sasa likiwa bado na huduma ya straika Luis Suarez ambaye hii itakuwa michuano yake ya mwisho.

Mbali ya Suarez kuna mastaa wengine kama Darwin Nunez na Edinson Cavani ambaye licha ya umri kumtupa linapokuja suala la kufunga hakwepeshi.

Uwepo wa Suarez na Cavani utaisaidia timu kwa sababu wana uzoefu wa kucheza kwenye hatua mbalimbali kubwa za michuano mikubwa duniani.

Mashindano yaliyopita vigogo hao waliishia robo fainali

ambapo walitolewa na mabingwa Ufaransa, hivyo ikiwa watakuwa na moto waliomaliza nao kule Russia 2018 wanaweza kuwa moja kati ya timu zitakazoshangaza dunia.

KOREA KUSINI

Taifa hil limeshiriki michuano hii mara 10 na tisa kati ya hizo limeshiriki mfululizo yaani tangu 1986 halijawahi kushindwa kufuzu.

Mafanikio makubwa ni kufika hatua ya nusu fainali 2002 ambapo lilimaliza kwenye nafasi ya nne.

Vilevile ukiacha hiyo, mwaka mwi-ngine uliokuwa na mafanikio kwao ni 2010 ambapo liliishia hatua 16 bora.

Kwenye michuano ya mwaka huu wenyewe wanaamini wanaenda na kizazi bora zaidi kuwahi kutokea tangu kile kilichocheza nusu fainali 2002.

Wababe hawa wa Bara la Asia ambao wana mastaa kibao ikiwa ni pamoja na Son Heung-min anayekipiga Tottenham Hotspur ambaye ndiye nahodha, nafasi ya kufanya vizuri na kushangaza ulimwengu inaonekana kuwa kubwa kwao kwa sababu wameshiriki mara nyingi mfululizo kwenye michuano hiyo na kwa uzoefu walionao wanaamini kizazi kipya kitawabeba Qatar.

POLAND

Ni nyumbani kwa mmoja kati ya mastraika watano bora barani Ulaya, Robert Lewandowski na haijawahi kuchukua kombe la michuano hiyo, lakini limewahi kumaliza nafasi ya tatu mara mbili 1974 na 1982. Baada ya kushindwa kufuzu 2010 na 2014, lilifuzu 2018 na mwaka huu ni mara ya pili kufanya hivyo.

Michuano iliyopita ilimaliza katika nafasi ya mwisho kwenye kundi baada ya kukusanya alama tatu na kupitwa hadi na Senegal. Mbali ya Lewandowski, hapa pia ni nyumbani kwa Piotr Zielinski anayefanya vizuri katika timu ya Napoli ambapo ubora wake umechangia timu hiyo kuwa tishio kwa sasa barani Ulaya.

Zielinski msimu huu amecheza mechi 21 za michuano yote na kufunga mabao sita. Pia ametoa asisti saba.

MEXICO

Mexico ina historia ya kushiriki fainali nyingi za Kombe la Dunia. Nchi hiyo imeshiriki fainali za Kombe la Dunia mara 15 katika historia ya nchi hiyo ikijumuishwa na michuano ya mwaka huu itakayofanyika Qatar. Licha ya kutopewa nafasi kubwa mwaka huu, Mexico ina kitu cha kujivunia kwani ina uzoefu mkubwa na mashindano hayo licha ya kutobeba ubingwa. Nchi hiyo inashiriki fainali Qatar kwa lengo moja moja tu kuhakikisha inafanya vizuri na kutinga raundi ya 16 bora ya michuano. Katika fainali za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini, Mexico ilitinga 16 bora baada ya kutoboa hatua ya makundi.

Licha ya kufungwa bao 1-0 ilipocheza dhidi ya Uruguay, Mexico ilitinga hatua hiyo baada ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Afrika na Ufaransa. Pia iliichapa Ufaransa mabao 3-1 na sare ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini. Kipindi hicho Mexico ilisheheni mastaa akiwemo Javier Chicharito, nyota wa zamani wa Manchester United.

Hata mwaka huu kikosi kitakachoshiri fainali za Qatar kimesheheni mastaa wenye uzoefu kina Raul Jimenez, Hirving Lozano na Hector Herrera ambao wanakipiga ligi za Ulaya. Mashabiki wanasubiri kuwaona washiriki hao wa kihistoria wa Kombe Dunia baada ya kutoboa raundi ya 16 bora 2018 watafanyaje mwaka huu.

CAMEROON

Cameroon ilikuwa hatari katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka huu ikiwa mwenyeji wa michuano hiyo. Je itafanikiwa Qatar? Licha ya kutopewa nafasi kubwa huenda ikashangaza kutokana na ubora wa kikosi kwani imesheheni wachezaji wakali kama Vincent Aboubakar, Karl Toko Ekambi,Eric Maxim Choupo-Moting, Collins Fai na Andre Onana.

Baada ya kikosi kubadilika miaka ya hivi karibuni Cameroon ina aina ya wachezaji wenye njaa ya mafanikio na wapo tayari kuonyesha maajabu waliyofanya tangu 1990 katika fainali zilizofanyika Italia, kwani walifanikiwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Cameroon imepata nafasi ya kushiriki fainali hizo kuonyesha dunia kwamba hata wao wapo kupeperusha vyema bendera kutoka Bara la Afrika baada ya kukosa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika 2018 kwa kushindwa kufuzu. Cameroon imepangwa kundi moja na Brazil, Serbia na Uswisi.

TUNISIA

Mashabiki wa Tunisia walifurahi baada ya Tunisia kufuzu fainali za Kombe la Dunia, kwani nchi hiyo haikupewa nafasi ya kutoboa, lakini ikashangaza.

Kocha anayeinoa Tunisia, Jalel Kadri na wachezaji 26 wapo tayari kushangaza hatua ya makundi na kuzipa ushindani timu za Denmark, Austria na Ufaransa katika kundi D.

Tunisia ina historia ya kushiriki fainali hizi mara tano katika miaka ya 1978, 1998, 2006, 2014 na 2018. Fainali zitakazofanyika Qatar itakuwa mara ya sita kwa taifa hilo. Nchi hiyo ina wachezaji wakali wakiongozwa na Aissa Laidouni na Ellyes Skhiri wenye uwezo wa kushambulia na kutengeneza nafasi.

Wengine ni Wahbi Khazri, Naim Sliti na Youssef Msakni wenye uzoefu na hatari wanapokuwa eneo la hatari.

Tunisia iliweka historia ya kushinda mechi ya kwanza Kombe la Dunia mwaka 1978 ilipoifunga Mexico kwa mabao 3-1. Nchi hiyo pia imepata kutoboa hatua ya makundi na kutinga raundi ya 16 bora kwani ndani ya miaka mitano tofauti ya michuano waliyoshiriki hawakuwahi kupenya raundi inayofuta.

Chanzo: Mwanaspoti