HALI ndani ya Yanga sio shwari baada ya wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji kutangaza kujiuzulu nafasi zote walizokuwa nazo klabu, huku wengine wawili wakisimamishwa kwa utovu wa nidhamu, ikiwa siku chache tangu Kampuni ya GSM kutishia kusitisha huduma zake klabuni.
Waliotangaza kujiuzulu na maamuzi yao kukubaliwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ni Rodgers Gumbo, Said Kambi na Shija Richard, huku waliosimamishwa kwa muda usiojulikana ni pamoja na vigogo wa Kamati ya Usajili, Frank Kamugisha na Salim Rupia.
Wajumbe hao wamechukua maaamuzi hayo kutokana na kikao kizito klilichofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia jana na leo, ikiwa ni siku chache tangu GSM ambayo ni moja ya wadhamini wa klabu hiyo kuandika barua kusitisha huduma walizokuwa wakizifanya nje ya mkataba wao.
Inaelezwa wajumbe hao hawakuwa wakiiva na kampuni hiyo iliyokuwa ikisimamia ishu za usajili, kuhudumia kambi na kulipa posho na mishahara ya wachezaji kwa kilichoelezwa ni kuingilia majukumu ya kamati hiyo na kuwachefua wanachama wa klabu hiyo wakihofia Yanga kurudi kwenye kutembeza bakuli.
Jioni uongozi wa klabu hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Mshindo Msolla umetoa taarifa rasmi juu ya maamuzi ya kamati hiyo ya utendaji sambamba na kueleza wameijibu barua ya GSM walioandikiwa Machi 24 mwaka huu.
Taarifa hiyo rasmi ya Yanga ilitiwa saini na Dk Mshindo ikifafanua kuwa wameridhia kina Gumbo kujiuzulu.
Pia Soma
- Tshishimbi aeleza mkataba mnono aliopewa na Simba
- Chama afunguka yanayoendelea kati yake na Simba Sc
- Ajibu, Yikpe hesabu zao zimekataa