Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu Coastal Union wabadili ratiba Ligi Kuu Bara

Coastala Ratiba Watatu Coastal Union wabadili ratiba Ligi Kuu Bara

Sat, 15 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB) imeondoa mechi mbili za Coastal Union ilizokuwa icheze jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City baada ya kukubali ombi lao la kuahirisha mechi hizo.

Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo leo Jumamosi Octoba 15, imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na sababu za kikanuni waliyoomba Wagosi hao wa Kaya baada ya wachezaji wake watatu kujumuishwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 (U23).

"Mabadiliko hayo yanatokana na sababu za kikanuni na ombi la Coastal Union kwa bodi ya Ligi baada ya wachezaji wake watatu tegemeo kujumuishwa kwenye timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 na michezo hiyo itapangiwa tarehe nyingine" imesema taarifa hiyo.

Timu hiyo ya jijini Tanga ilikuwa ishuke uwanjani kuwavaa Prisons, mechi iliyokuwa ichezwe Jumatatu, Oktoba 17 kisha kuwakabili Mbeya City Oktoba 24 zote zikipigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Coastal Union iliwasilisha maombi yake kusogezwa mechi hizo kutokana na wachezaji wake watatu, beki wa kati, Khatibu Kombo, kiungo Yusuph Jamal na Straika Vicent Aboubakari.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Afisa Habari wa Prisons, Jackson Mwafulango amesema tayari uongozi chini ya Katibu Mkuu wa timu hiyo, Anthony Hau wamepokea barua na kwamba benchi la ufundi linaendelea na program yao kujiandaa na mechi inayofuata dhidi ya Polisi Tanzania itakayopigwa Oktoba 25 kwenye uwanja wa Sokoine.

"Tayari uongozi tumepata taarifa za mabadiliko ya mechi hiyo ambapo benchi la ufundi limetaarifiwa hivyo program na maandalizi yanaendelea kwa ajili ya mchezo wetu na Polisi Tanzania" amesema Mwafulango.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Yusuph Chipo amesema waliwasilisha maombi hayo na walitarajia majibu yoyote lakini wao walikuwa wakiendelea na maandalizi na mechi hizo kuhakikisha wanashinda baada ya kurekebisha makosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Geita iliyomalizika kwa suluhu ya bila kufungana nyumbani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live