Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania tunapombagua Mtanzania mwezetu

FCuBIRhX0AQI6G Kibu Dennis akijarubu kumtoka mchezaji wa Polisi Tanzania

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sio utani. Nilikuwepo mahala nikitazama mechi nilipomsikia shabiki mmoja akiropoka na kuungwa mkono na wenzake. “Afadhali tungewapa uraia hawa kina Aucho, lakini sio huyu rasta”. Alikuwa akimaanisha Kibu Dennis.

Mara nyingi tumekuwa tukijadili uraia wa Kibu. Hata alipocheza pambano dhidi ya Benin kuna watu walimshambulia katika suala la uraia pindi alipokosea kitu uwanjani. Uraia wa Kibu unaonekana kama vile ni kitu cha ajabu.

Nadhani kwa sababu hatujichanganyi. Nadhani pia ni kwa sababu ya Watanzania kuwa wagumu kutoa uraia kwa watu wengine au kutokuwa na uraia pacha. Mtu ambaye sio Mtanzania anapokuwa Mtanzania huwa tunaona kitu cha ajabu. Haya ni maisha ya kawaida kabisa kwa wenzetu.

Haijalishi kama m-chezaji ana kiwango gani cha mpira lakini anaweza kupewa uraia kutokana na taratibu alizofuata. Haijalishi kama mtu ni raia wa kawaida anaweza kupewa uraia tu kutokana na taratibu alizofuata.

Simba kumuombea uraia Kibu au kibali maalumu cha kucheza katika klabu haimaanishi kwamba ghafla angegeuka kuwa ‘Mbwana Samatta’. Tusimhukumu kwa uraia wake, tumhukumu kwa kiwango chake zaidi.

Kumhukumu kwa uraia ni unyanyasaji na ubaguzi. Kuna Watanzania wengi wamepewa uraia katika nchi za watu na wala hawabaguliwi. Lakini kama wangekuwa wanaambiwa maneno haya ambayo tunamwambia tungejisikiaje?

Tumuache acheze mpira na akosee au kupatia kama mchezaji mwingine yeyote yule. Uraia wake haumuongezei kipaji wala haumpunguzii kipaji. Tumuache tu afurahie soka lake. Hata sisi tuna wachezaji wengi wazawa ambao wanafanya makosa kila siku.

Awali nilikuwa nadhani utani lakini sisi tumeelekea kuwa wabaguzi. Ubaguzi ni kitu kibaya ambacho tusingependa kina Samatta na Msuva wafanyiwe katika nchi za watu. Kwa sasa Kibu ni Mtanzania na anapaswa kuangaliwa kwa kipaji chake tu na si mengineyo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz