Historia ya mastaa watatu wa Simba inawapa fursa nzuri ya kuwemo katika kundi la nyota watano wenye nafasi kubwa ya kuendelea kusalia kikosi cha kwanza cha timu hiyo, licha ya ujio wa kocha mpya Pablo Franco.
Licha ya ujio wa makocha wapya kila mara, kuwaathiri baadhi ya wachezaji kupoteza nafasi na kunufaisha wengine kikosini, nyota hao watatu ukiongeza na wengine wawili wana nafasi kubwa kupeta mbele ya Pablo aliyetua Msimbazi Novemba 6.
Wachezaji hao ni mabeki wawili wa pembeni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe na na kipa Aishi Manula.
Katika kundi la wachezaji waliodumu kwa muda mrefu kikosini, watatu hao ndio pekee wamekuwa na historia ya nafasi zao kutoathirika na ujio wa makocha wapya..
Manula aliyejiunga na Simba akitokea Azam mwaka 2017, amekuwa chaguo la kwanza katika nafasi hiyo chini ya makocha wanne tofauti ambao ni Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck na Didier Gomes.
Katika kipindi cha miaka mitano Manula amekuwa chaguo la kwanza katika ukipa, huku wengine akiwamo ni Deogratias Munishi ‘Dida’, Beno Kakolanya, Ally Salim na Jeremiah Kisubi kushindwa kumpiku.
Hata chini ya Pablo, Manula ana nafasi kubwa ya kuanza kwa kiwango bora alichonacho pia anabebwa na kitendo cha kuwa kipa namba moja kwenye Taifa Stars.
Mwingine mwenye hadithi inayofanana na Manula ni Kapombe aliyesajiliwa sambamba na kipa huyo wakitokea Azam.
Licha ya usajili wa mabeki wengine wa kulia kama Haruna Shamte, Zana Coulibaly, Ally Shomary, David Kameta na Israel Patrick, Kapombe ameonekana hana mpinzani na ameendelea kuwa chaguo la kwanza.
Tshabalala naye amekuwa chaguo la kwanza tangu Simba ikiwa chini ya Lechantre, Aussems, Sven na Gomes na hapo kabla wakati Simba ilipokuwa ikinolewa na Dyran Kerr, Jackson Mayanja, Joseph Omog, Patrick Phiri, Zdravko Logalusic na Goran Kopunovic.
Msimu wa 2018/19, Asante Kwasi alionekana kuanza kushinda vita ya namba dhidi ya Tshabalala kwa kupangwa mechi za mwanzoni za Simba, ila ghafla alipoteza nafasi hiyo na Aussems kumrudisha Tshabalala.
Ukiondoa watatu hao, wachezaji wengine wawili ambao wana nafasi ya kujihakikishia nafasi ya kuanza kikosi cha Simba chini ya Pablo ni Rally Bwalya na beki wa kati Enock Inonga ‘Varane’.
Kukosekana kwa kiungo mshambuliaji anayeweza kucheza vyema namba nane au nyuma ya mshambuliaji wa kupambana na Bwalya ni wazi kwamba kunamuweka katika mazingira mazuri kiungo huyo Mzambia kuendelea kutamba kikosi cha kwanza.
Kutetereka kwa viwango vya mabeki wawili wa kati waliokuwa mhimili wa timu hiyo msimu uliomalizika, Pascal Wawa na Joash Onyango kunatoa nafasi kubwa kwa Varane kujihakikishia nafasi kikosi cha kwanza.
Kiwango bora kilichoonyeshwa na Varane tangu ajiunge Simba kimemfanya awe lulu na kipenzi ndani ya timu huyo na kusababisha Wawa, Onyango na Kennedy Juma wawanie nafasi moja tu ya kucheza kabla ya beki huyo kufungiwa kwa kosa la kumpiga kichwa Issah Abushehe wa Coastal Union.
Kocha wa Tunduru Korosho, Amani Josiah alisema hadhani kama kundi kubwa la wachezaji litapoteza nafasi siku za mwanzoni za Pablo.