Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watani matokeo makundi yawape adabu

Yanga X Simba Balaa Watani matokeo makundi yawape adabu

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ghafla tu nimezikumbuka zile hesabu zilizokuwa zinapigwa baada ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kupangwa, Simba ikidondokea Kundi B pamoja na Wydad, Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy huku Yanga ikipangwa Kundi D na Al Ahly, CR Belouizdad na Medeama.

Kundi kubwa la watu wa Simba likaanza hesabu ambazo zitaipeleka timu robo fainali kwamba watashinda mechi tatu nyumbani halafu katika mechi tatu za ugenini watachukua pointi nne dhidi ya Asec na Jwaneng Galaxy jambo litakalofanya imalize na pointi 13.

Walituaminisha timu tishio kwao ni Wydad ila Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy zitakuwa daraja lao la kuwapeleka kirahisi katika robo fainali.

Watani wao Yanga nao wakawa na hesabu zinazofanana na hizo kwamba katika lile kundi lao, wana pointi sita za Medeama, wanachukua pointi nne kwa Belouizdad na kisha kwa Al Ahly uhakika nyumbani wanavuna tatu.

Kwa maana hiyo hapo kimahesabu wanakuwa na pointi 13 ambazo sio tu zinawapeleka robo fainali bali hata kufanya waongoze kundi.

Lakini raundi mbili za mwanzo zikaonyesha mipango sio matumizi. Simba wakapata pointi mbili kwa kutoka sare dhidi ya Jwaneng Galaxy na Asec Mimosas, huku Yanga wakipata pointi moja kwa kutoka sare na Ahly huku wakipoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Belouizdad.

Nilitegemea kuona baada ya matokeo hayo wawakilishi wetu wangeshtuka na kuanza kuzipa heshima timu hizo kwenye makundi yao, kisha kujikita zaidi na maandalizi ya uwanjani na kuacha matokeo ya mechi zilizobakia yatoe majibu.

Mambo yamekuwa tofauti na jamaa bado hawaonekani kuzipa heshima timu hizo maana, licha ya kwamba wao ndio wana pointi chache kwenye makundi yao, wanatamba kuzipita kirahisi zile ambazo tayari zipo juu yao kwa pointi.

Kwa Simba, Jwaneng Galaxy na Asec Mimosas sio aina ya wapinzani wa kuwadharau kiasi hicho, kwani matokeo waliyopata kwenye mechi za mwanzo ni mazuri kuliko wao kama ilivyo kwa Yanga na Belouizdad na Medeama. Waheshimuni tu hamtoonekana wajinga.

Chanzo: Mwanaspoti