Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba leo watakuwa na kazi ngumu mbele ya US Gendarmerie ya Niger katika mechi ya pili ya michuano hiyo.
Simba imetamba kuwa imejipanga vizuri na kuahidi haitarudi mikono mitupu.
Simba iliondoka juzi ikipitia Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kupaa tena kuelekea Niger huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mpaka sasa Simba inashika nafasi ya pili Kundi D katika michuano hiyo ikiwa na pointi tatu sawa na Berkane inayoongoza wakizidiana uwiano wa mabao, Asec ya tatu na ya mwisho ni Gendarmerie.
Gendarmerie ikiwa ugenini nchini Morocco ilipoteza mechi yake ya kwanza kwa mabao 5-3 dhidi ya Berkane.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameliambia HabariLEO kuwa wanafahamu ugumu wa mchezo huo kwa kuwa Gendarmerie itataka kujitengenezea mazingira mazuri katika mchezo wa pili baada ya kupoteza wa kwanza wakiwa ugenini, hivyo wanafahamu namna itakavyokuja uwanjani na wao wameshajipanga kwa hilo.
“Tunafahamu watahitaji matokeo na sisi pia tunahitaji hayo matokeo na kama tutashindwa kupata ushindi wa pointi zote tatu basi tutahakikisha tunaondoka na pointi moja kwa ajili ya kuongeza kitu tukiwa ugenini.
“Inafahamika kwamba tukimalizana na Gendarmerie tutakwenda kumalizana na Berkane kabisa kule Morocco kwa hiyo huko nako hatutahitaji kuondoka mikono mitupu, ni aidha ushindi au sare ili tupate pointi moja,” alisema Ally.
“Unajua hata kama tutapata pointi mbili kwenye mechi hizi mbili, tutakuwa na pointi tano na michezo mitatu mkononi ambayo miwili tutacheza nyumbani kwa hiyo tutahakikisha hii ya nyumbani tunashinda na kuwa na pointi 11 ambazo tayari zitakuwa zimetuweka kwenye mazingira ya hatua inayofuata.”
Wekundu hao baada ya mechi yao na Gendarmerie itakayopigwa Uwanja wa Jenerali Kountche, mjini Niamey wataunganisha Morocco kukipiga na Berkane Februari 27, mwaka huu.
Katika msafara wa mechi hizo, Simba imekwenda na wachezaji 23 huku wengine kama Hassan Dilunga, Kibu Denis na Chris Mugalu wakiwa majeruhi na Rally Bwalya na Mzamiru Yassin wakiwa na udhuru wa masuala ya kifamilia.