Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Warithi wa Oppa, Masaka hawa hapa...

Masaka.jpeg Nyota wa Tanzania Aisha Masaka

Sun, 10 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kila zama na kitabu chake! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Ligi Kuu ya Wanawake kuendelea kupata malkia wapya kila msimu kwenye upachikaji wa mabao tangu utawala wa Asha Mwalala, Fatuma Mustapha, Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’ kisha Oppa Clement na Aisha Masaka na sasa msimu huu tutashuhudia majina mapya.

Kuondoka kwa wapinzani wawili wakubwa wa vita ya ufungaji mabao kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, Oppah Clement (Simba Queens) na Aisha Masaka (Yanga Princess) kumetoa rasmi mwanya kwa nyota wengine kubeba kiatu hicho.

Oppa na Aisha wamekuwa na upinzani mkubwa katika misimu miwili ya siku za hivi karibuni ambapo Aisha aliibuka kinara msimu uliopita kwa kufunga mabao 35 Oppah akifuatia na mabao 30, lakini msimu huu Oppah alikuwa anaongoza mbio akiwa na mabao 19 huku Aisha akifunga sita.

Mastaa hao tayari wameaga katika timu zao na hawatokuwepo kwenye duru la pili la ligi hiyo baada ya kupata timu nje ya nchi ambapo Aisha amejiunga na mabingwa wa Sweden, BK Hacken FF huku Oppah akitimkia Yikatel Kayseri ya Uturuki.

Wafumania nyavu wanaopewa nafasi kubwa ya kubeba kiatu cha ufungaji msimu huu kutokana na kasi yao ya kucheka na nyavu ni Zainabu Mohamed (Baobab Queens), Clara Luvanga (Yanga Princess), Asha Djafari (Simba Queens), Hasnath Ubamba na Stumai Abdallah (Fountain Gate Princess) na Winfrida Charles (Alliance Girls).

ZAINABU MOHAMED ‘DUDU’

Japokuwa hakuwa tishio kwa misimu mitatu aliyokuwa Mlandizi Queens ya Pwani lakini tangu ajiunge na Baobab Queens ya Dodoma msimu huu amekuwa miongoni mwa wafumania nyavu wa kuogopwa na wanaotazamwa kwa jicho la ziada.

Zainabu amemaliza mzunguko wa kwanza akitupia mabao 14 katika mechi 11 akizidiwa na Oppah Clement pekee aliyeweka kambani mabao 19.

Zainabu amefunga katika mechi nane ambapo ametupia mabao mawili katika michezo minne mfululizo huku akifunga hat-trick kwenye mchezo mmoja na kupewa nafasi ya kuwa mrithi wa Oppah na Aisha Masaka.

CLARA LUVANGA

Mwanzoni mwa msimu alicheza mechi tano bila bao na kuondoa kabisa uwezekano wa kufikiriwa kuwa kwenye orodha ya wafungaji wa ligi lakini baada ya kutoka kwenye majukumu ya timu za taifa amerudi na moto wa kuotea mbali.

Katika michezo sita ya mwisho ya timu yake kuhitimisha duru la kwanza amefunga mabao 12 na kushtua umma wa wanamichezo na wafuatiliaji wa ligi hiyo akivuka viunzi na kuingia kwenye tatu bora ya vinara wa mabao hadi sasa.

Clara aliyejiunga na Yanga Princess msimu huu akitokea Mapinduzi Queens ya Njombe ameweka pia rekodi ya kipekee hadi sasa kwenye ligi hiyo kuwa mchezaji aliyefunga mabao matano katika mchezo mmoja akifanya hivyo dhidi ya TSC Queens timu yake ilipoibuka na ushindi wa 7-0.

ASHA DJAFARI

Nyota huyu wa Simba Queens raia wa Burundi amekuwa na mwendelezo mzuri wa upachikaji mabao akikamata nafasi ya nne kwenye orodha ya wafumania nyavu kwa duru la kwanza wa ligi hiyo akiwa na mabao 12 katika mechi 11 alizocheza.

Mkali huyo wa mabao amefunga hat-trick mbili akiwa sambamba na Oppah Clement kuwa wachezaji pekee waliofunga hat-trick mbili hadi sasa katika Ligi ya Wanawake msimu huu.

Amefunga katika mechi saba dhidi ya Ruvuma Queens (3), Oysterbay Queens (3), Yanga Princess (2), TSC Queens (1), JKT Queens (1) na Baobab Queens (1).

HASNATH UBAMBA

Mshambuliaji huyu wa Fountain Gate Princess ya jijini Dodoma amekuwa msaada mkubwa kwa timu yake katika mechi za mwisho wa duru la kwanza akiifungia timu yake mabao nane katika mechi 10.

Hasnath anakamata nafasi ya tano kwa orodha ya vinara wa mabao kwenye Ligi hiyo nyuma ya Oppah (19), Zainabu (14), Clara (12) na Asha Djafari (11) pia akiwa kinara wa mabao kwenye kikosi chao na kuwa tegemeo baada ya kukosekana kwa Stumai Abdallah ambaye yuko masomoni.

Amefunga mabao hayo katika michezo minne dhidi ya timu za Oysterbay Girls (2), Baobab Queens (2), JKT Queens (2) na kutupia bao moja moja dhidi ya Alliance Girls na TSC Queens za Mwanza.

WINFRIDA, STUMAI, NEEMA

Nyota Stumai Abdallah na Neema Paul wa Fountain Gate Princess na Winfrida Charles wa Alliance Girls wote wamefunga mabao saba katika mechi 11 za timu zao msimu huu.

Stumai Abdallah amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea JKT Queens ambayo ametamba nayo kwa misimu mitatu akiwa miongoni mwa wafungaji watatu bora wa timu hiyo nyuma ya Aisha Mwalala na Fatuma Mustapha.

Alianza msimu kwa kasi kubwa akifunga mabao hayo katika mechi tatu tu dhidi ya Mlandizi (3), The Tigers (2) na Ilala (2) lakini baadaye aliondoka kikosini na kurudi mafunzoni (JKT) alikokuwa awali ikiitumikia JKT Queens.

Anatazamiwa kurejea kwenye duru la pili la ligi hiyo akitarajiwa kuendeleza makali yake na kuwa miongoni mwa wafumania nyavu matata msimu huu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz