Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapo, wanasubiri Ten Hag afukuzwe

Makocha Foleni Wapo, wanasubiri Ten Hag afukuzwe

Sun, 5 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Erik ten Hag hana tena pa kujificha huko Manchester United kutokana na matokeo ya hovyo inayovuna timu hiyo uwanjani msimu huu.

Usiku wa Jumatano iliyopita, timu yake ya Man United ilikumbana na kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Newcastle United kwenye Kombe la Ligi, jambo linaloifanya timu hiyo kuanza na mwanzo wa hovyo zaidi wa msimu katika kipindi cha miaka 61.

Presha imezidi kupanda kwa kocha huyo Mdachi na gwiji wa Man United, Gary Neville anadhani kwamba Ten Hag amejiweka kwenye nafasi kubwa ya kufutwa kazi. Man United inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na mbaya zaidi imechapwa mara tano katika mechi 10 za ligi, huku mechi zote hizo ilizochapwa, imepigwa uwanjani Old Trafford.

Na mambo yalivyo mabaya zaidi, huenda ikatupwa nje pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuvuna pointi tatu tu kwenye mechi hatu za makundi ilizocheza, huku ikichapwa mbili dhidi ya Galatasaray na Bayern Munich.

Mechi zijazo za Man United itacheza dhidi ya Fulham, Copenhagen na Luton na matokeo yoyote yasiyokuwa ya ushindi kwenye mechi hizo, yanaweza kutengeneza mwisho za zama za Ten Hag huko Old Trafford.

Hivyo basi, kama Ten Hag ataonyeshwa mlango wa kutokea, hii hapa orodha ya makocha ambao huduma zao zinaweza kunaswa ili wakapige mzigo Man United.

Joachim Low

Mjerumani huyo ni mmoja kati ya makocha 21 pekee walioshinda Kombe la Dunia. Lakini hajapata timu ya kufundisha kwa ngazi ya klabu tangu alipojiuzulu ukocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani mwaka 2021 baada ya kudumu kwa muda wa miaka 15.

Low alisikilizia ofa moja au mbili na alihusishwa na Fenerbahce, pamoja na kurejea kufundisha timu za kimataifa kama Uturuki, Brazil na Ubelgiji lakini nafasi yake ya mwisho ngazi ya klabu aliwahi kuifundisha Austria Vienna ambayo aliitema miaka 20 iliyopita.

Zinedine Zidane

Kocha huyo hana timu tangu alipoondoka Real Madrid kwa mara ya pili mwaka 2021. Mkongwe huyo alishinda mataji mawili ya LaLiga na matatu ya Ligi Mabingwa Ulaya, alihusishwa na kazi ya ukocha Manchester United na bila shaka anaongoza kwenye mbio za kuchukua mikoba ya Erik ten Hag. Pia, mkongwe huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ufaransa alihusishwa na klabu ya Marseille lakini taarifa hizo zikapingwa vikali.

Hansi Flick

Bado anaugulia machungu ya kufukuzwa kazi ya ukocha kwenye Timu ya Taifa ya Ujerumani, Septemba mwaka huu baada ya kuiongoza mechi 25 na kushinda mara 12 u tangu alipochukua nafasi ya Joachim Low mwaka 2021. Rekodi yake Bayern Munich ilikuwa bora zaidi kwani alishinda mara 70 katika michezo 86 Uwanja wa Allianza Arena. Aliisaidia miamba hiyo kubeba makombe mawili msimu wa 2019-2020. Endapo Flick atarudi mzigoni anaweza kupata kazi Bundesliga na Ulaya kwa ujumla.

Roberto De Zerbi

Kocha huyo anayeinoa Brighton kwa sasa amehusishwa na timu nyingi ikiwemo Manchester United baada ya kuonyesha soka safi kutokana na aina ufundishaji wake. Ameipeleka Brighton kushiriki michuano ya Europa kwa mara kwanza msimu huu. Brighton ilikiwasha msimu uliopita tangu De Zebri, alipochukua mikoba ya Graham Potter. Man United inatakiwa kutoa mkwanja mrefu ili imng’oe De Zerbi.

Diego Simeone

Simeone yupo Atletico Madrid kwa muda wa miaka 12 na imeripotiwa hana mpango wa kuondoka kusaka changamoto sehemu nyingine. Ingawa mkataba wake utamalizika mwishoni mwa msimu na kocha huyo anayelipwa pesa ndefu, anatakiwa kukubali kupunguziwa mshahara wa asilimia 20 ili aongeze mkataba mpya. Man United inaweza kuchukua nafasi hiyo na kujaribu kumshawishi aondoke Hispania. Aina yake ya ufundishaji wa kutumia mabeki wanne nyuma inaweza kutatua matatizo ya Man United.

Julian Nagelsmann

Nagelsmann alitimuliwa na Bayern Munich tangu Machi mwaka huu, licha ya kubeba ubingwa wa Bundesliga pia ilishiriki michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya na kufanya vizuri hatua ya makundi. Baada ya kuondoka Bayern aliteuliwa kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani akichukua nafasi ya Flick. Kocha huyo mwenye mbinu anaweza kufanya uamuzi wa kurejea kwenye ngazi ya klabu baada ya michuano ya Euro mwakani.

Antonio Conte

Ndio aliondoka vibaya Tottenham mwisho wa siku lakini alibadilisha kikosi chini ya utawala wake kwa kiwango kikubwa. Kwa kuongezea aliwahi kubeba ndoo ya Ligi Kuu England wakati akiinoa Chelsea na anabaki kuwa mmoja kati ya makocha sita bora wa Ligi Kuu England wa muda wote. Conte aliweka rekodi ya kubeba mataji manne ya Serie A na kujingenezea sifa nyingi Italia, pia anapenda siku moja arudi nyumbani huku akijihusisha na timu kama Napoli na Roma. Kabla ya Kocha Erik ten Hag kutua Old Trafford alihusishwa na Man United lakini dili likabuma badala yake akajiunga na Spurs.

Graham Potter

Potter alishindwa kuhimili presha ya klabu kubwa (Chelsea) ambayo ilipitia mabadiliko, baada ya mmiliki mpya kununua timu na alifukuzwa kazi baada ya kudumu kwa muda wa miezi saba tu. Hajapata kazi tangu alipoondoka Stamford Bridge huku Gazeti la Sun likiripoti Potter yumo kwenye orodha ya makocha wanaowindwa Man United endapo Erik ten Hag atafukuzwa. Potter ana nafasi nzuri kwani bilionea Sir Jim Ratcliffe anamkubali na anaweza kupewa shavu endapo atafanikiwa kuinunua Man United kwa asilimia 25.

Chanzo: Mwanaspoti