Kocha Mkuu wa Azam, Dani Cadena amesema sababu kubwa za kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kwenye kikosi hicho ni kutokana na mpinzani wake kuwa tofauti.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Cadena alisema jambo kubwa analojivunia kwenye timu hiyo ni uwepo wa wachezaji bora hivyo kutocheza kwa mmoja wao kati ya wale waliopo haina maana kwamba kiwango chao kimeshuka kama ambavyo inazungumzwa.
"Tuna michezo mingi ndani ya msimu na kila mchezaji ni lazima acheze, sisi kama benchi la ufundi tunapenda kuona utayari wao na wakiwa na utimamu wa mwili hivyo tunachagua kutokana na umuhimu na ugumu wa mchezo uliopo mbele yetu," alisema.
Aidha Cadena aliongeza huenda kukawa na mabadiliko madogo kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Ihefu utakaochezwa Jumatatu ya Machi 13.
"Kulikuwa na wachezaji majeruhi ambao wameanza kurudi kikosini hivyo ni matumaini yetu hadi kufikia siku ya mchezo tutakuwa na wigo mpana wa machaguzi hususani ikichangiwa na ubora wa mpinzani wetu tunayeenda kupambana naye," alisema.
Azam inakutana na Ihefu katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Highland Estate Mbarali mkoani Mbeya huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi ya kwanza zilipokutana kwa bao 1-0 Oktoba 31, mwaka jana Azam Complex.