Dar es Salaam. Timu itakayocheza na Yanga ya Tanzania katika mechi ya mchujo ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu itajulikana rasmi Oktoba 9 itakapopangwa droo Cairo, Misri.
Yanga ambayo imeondolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia kwa matokeo ya jumla ya kufungwa mabao 3-2 kwenye raundi ya kwanza, imeangukia upande wa pili ambako itapangwa na moja kati ya timu 16 zilizopenya kuingia hatua hiyo baada ya kufanya vizuri kwenye raundi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) mapema leo, droo hiyo ya mechi za mchujo za Kombe la Shirikisho Afrika hafla yake imepangwa kufanyika kwenye Hoteli ya Hilton Pyramids Resort iliyopo jijini Cairo, Misri kuanzia saa 12 jioni.
Katika droo hiyo, Yanga itakuwa kwenye chungu kimoja sambamba na timu nyingine 15 ziliztolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku chungu kingine kikiwa na timu 16 zilizotinga hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho ambapo zitakutanishwa pamoja kusaka klabu 16 zitakazotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho msimu huu.
Timu 16 za upande wa Kombe la Shirikisho ambazo zimetinga hatua ya mchujo ya mashindano hayo ni RS Berkane (Morocco), Al-Masry (Misri), Hassania Agadir (Morocco), Zanaco (Zambia), Enugu Rangers (Nigeria ), Djoliba (Mali), Paradou AC (Algeria), ESAE (Benin), DC Motema Pembe (DR Congo), FC San Pedro (Ivory Coast), Pyramids (Misri), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).
Mbali na Yanga, timu nyingine 15 zilizoondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ni UD Songo (Msumbiji), Côte d'Or (Shelisheli), Green Eagles (Zambia), Fosa Juniors (Madagascar), Elect-Sport (Chad), KCCA (Uganda), Asante Kotoko (Ghana), FC Nouadhibou (Mauritania), Generation Foot (Senegal), Cano Sport (Guinea ya Ikweta), Gor Mahia (Kenya), ASC Kara (Togo), Horoya (Guinea) na Al Nasr (Libya).
Pia Soma
- Vita ya Kane, Lewandowski yatikisa Ulaya
- Kocha Arsenal achekelea sare Old Trafford, Keane aponda kiwango
- De Gea awaonya wachezaji Manchester United kwa sare Arsenal