Kocha Mkuu wa Kipanga FC, Hassani Kitimbe amewaondoa hofu Yanga kwa kuwaambia wana nafasi ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwafunga wapinzani wao, Club Africain ya nchini Tunisia.
Timu hizo zitavaana katika mchezo wa Play-Off wa Kombe la Shirikisho keshokutwa Jumatano baada ya ule wa awali kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Kipanga ndio waliondolewa na Club Africain katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao walipata suluhu nyumbani kabla ya kwenda kufungwa Tunisia.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kitimbe alisema kuwa Yanga wanatakiwa kuwadhibiti Club Africain kwa dakika 30 za kutoruhusu bao golini kwao.
Kitimbe alisema kuwa Africain kipindi cha kwanza wanakitumia vizuri katika kushambulia ili wapate bao la mapema na kuongeza presha kwa wapinzani wao.
Aliongeza kuwa kama wakifanikiwa hilo, basi watawaongezea presha wapinzani wao na kujikuta wakiliacha goli wazi na kushambulia wote, hiyo itawapa nafasi Yanga kupata bao kwa kumtumia vizuri Fiston Mayele ambaye ataachwa huru muda mwingi.
“Kikubwa Yanga inachotakiwa kukifanya ni kuidhibiti Club Africain katika dakika 30 za kipindi cha kwanza pekee, kwani wao dakika hizo ndio huzitumia vema kushambulia ili wapate bao la mapema.
“Licha ya kupata upinzani kutoka kwa mashabiki wao wana fujo hadi za kurusha chupa uwanjani, lakini Yanga wasizingatie wao wapambane kutafuta matokeo.
“Wao wacheze kwa nidhamu kubwa ya kutoshambulia wote katika goli la wapinzani na badala yake wacheze mipira mirefu kwa mawinga wao, kwani hawana spidi kubwa ya kukimbia na mipira,” alisema Kitimbe.