Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapigwa faini kwa kumpa pasi mwenzao uwanjani

Adel Taarabt Act 2635592b Adel Taarabt

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Unamkumbuka kocha Neil Warnock? Unamkumbuka kiungo wa mpira, Adel Taarabt?

Wawili hao wana hadithi tamu kwelikweli. Walikuwa pamoja kwenye kikosi cha Queens Park Rangers, mahali ambako Taarabt alicheza soka la kiwango chake bora.

Na kocha Warnock anafichua kitu gani alifanya kumfanya Taarabt kucheza soka la kiwango cha juu uwanjani. Lakini, wakati unajiuliza ni kitu gani hicho, kocha huyo anafichua pia, aliwakataza wachezaji wake wasimpe pasi Taarabt.

Makali ya Taarabt

Taarabt alikuwa mchezaji muhimu sana wakati QPR inakamatia tiketi ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu England mwishoni mwa msimu wa 2010-11, alifunga mabao 19 na kuasisti mara 19 kwa msimu huo na kuwasaidia kushinda ubingwa wa Championship. Akiwa amejaliwa ufundi wa kutosha kwenye miguu yake, staa huyo wa Morocco aliwahi kuwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotpur kabla ya kujiunga jumla Loftus Road mwaka 2010 baada ya msimu mzima wa kucheza kwa mkopo.

Baada ya kushindwa kumshawishi kocha wa Spurs, Harry Redknapp , QPR walikwenda kumnasa Taarabt na kocha Warnock anakumbuka namna alivyovutiwa na kiungo huyo wa ushambuliaji wakati anatua kwenye timu yake msimu wa 2009-10.

Kocha huyo veterani alisema: “Naikumbuka sana siku hii, kulikuwa na kijana mdogo aliyekuwa amevaa glovu nyeusi. Nilimuuliza msaidizi wangu: ‘Nani yule aliyevaa glovu?’. Alinijibu: ‘Kocha wala usitake kumfahamu yule jamaa. Yule ni Taarabt. Kijana wa Morocco amekuja kutoka Tottenham. Amekuja kukufukuzisha kazi. Ameshamfukuzisha kazi kocha huko. Matumizi mabaya ya nafasi’.

“Nilitazama ile mechi na QPR haikufunga bao - hilo lilikuwa tatizo lao. Na nilimtazama yule kijana sikuona chochote kinachoshabiana na nilichoambiwa. Lakini, nilichokiona, alikuwa anakwenda kuchukua mipira kwa mabeki wa kati, anapiga watu matobo, anapoteza mpira, wapinzani wanachukua na kufunga.

“Kama kocha kuna kitu nilikiona. Nilimpenda na zile glovu zake. Japo zile glovu hazikuwa zikinivutia. Nilimwita na kumuuliza: ‘Unahisi baridi Adel? Tunacheza na West Brom Jumamosi, nitakupanga - sawa? Kama utafanya vizuri, nitakupanga mechi ijayo, ukifanya tena vizuri nitakupanga mechi inayofuata, tumeelewana? Kwa babu wewe una kitu kitatusaidia’."

Marufuku kumpa pasi Taarabt

Kocha Warnock alifahamu udhaifu wa Taarabt wa kupenda kupiga chenga bila ya kujali yupo kwenye eneo gani. Jambo hilo lilimfanya apoteze mipira mingi akiwa kwenye eneo la hatari la timu yake na kusababisha wapinzani kufunga mabao.

Kutokana na hilo, Warnock aliibuka na kuwapiga wachezaji marufuku kumpa pasi Taarabt anapokuwa kwenye eneo lao. Kuhakikisha marufuku hiyo inafanya kazi, Warnock alipendekeza faini ya Pauni 50 (zaidi ya Sh150,000) kwa mchezaji atakayempa pasi Taarabt wakiwa kwenye nusu ya uwanja ya upande wao.

Warnock alisema: “Nikawafuata wachezaji wengine, bila ya kumhusisha Taarabt na niliwaambia: ‘Yeyote atakayempa pasi Taarabt tukiwa kwenye nusu yetu, faini Pauni 50’. Kisha nikamfuata Adel na kumwambia: ‘Adel, kama utakuja kwenye nusu yetu na kuchukua mpira, nakupiga faini ya Pauni 50 - sawa?’.

“Nadhani kuna mchezaji mmoja alimpa pasi na tulimpiga faini ya Pauni 50, ni huyo tu. Ukimpa mpira kwenye nusu ya upande wa timu pinzani, utapenda.”

Taarabt akatua jumla QPR

Mwisho wa msimu huo, QPR ilimsajili jumla Taarabt kwa dau dogo, lililoripotiwa kuwa Pauni 1 milioni sambamba na wachezaji wengine kama Paddy Kenny, Shaun Derry na Clint Hill. Wachezaji hao wengine wote walikuwa na vigezo stahiki vya kuwa manahodha wa timu hiyo kumzidi Taarabt, lakini kocha Warnock alifanya kile kilichowashtua wengi kwa kuamua kumpa Taarabt kutambaa cha unahodha wa QPR.

Warnock aliwaambia wachezaji wake: “Sikilizeni, ninakwenda kumfanya Adel kuwa nahodha wetu."

Kulikuwa na wachezaji wengine watano au sita hivi wanaoweza kuwa manahodha. Niliamini kama nitaweza kupata walau asilimia 10 au 20 ya mchango kutoka kwa Taarabt basi tutapanda daraja, huku akiwaambia mastaa wake wakipanda daraja, hata mishahara yao itaboreshwa na kupewa mikataba minono.

Na hakika, Taarabt akawasha moto na kuisaidia QPR kupanda daraja msimu huo.

Peter Crouch, ambaye alicheza na Taarabt walipokuwa Spurs, aliangukia kicheko baada ya Warnock kuthibitisha kwamba aliwapiga faini wachezaji wake waliompasia pasi mwenzao wakiwa kwenye nusu yao.

Akatimkia zake Milan

Baada ya kutamba QPR, Taarabt aliondoka zake kwenda AC Milan kisha Benfica. Baada ya Taarabt kuonyesha kiwango bora kabisa kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha QPR kuna timu kadhaa zilianza kufikiria kumsajili. Tatizo la Taarabt kiwango chake kilikuwa kinapanda na kushuka. Baada ya hapo akapata nafasi ya kwenda kwa mkopo Fulham na AC Milan kabla ya kupata uhamisho wa jumla kwenda kujiunga na miamba ya Ureno, Benfica mwaka 2015. Kwa sasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34 anakipiga kwenye kikosi cha Al-Nasr SC ya Falme za Kiarabu.

Straika wa zamani wa Ligi Kuu England, Crouch alisema wachezaji ambao mitaa haitaweza kuwasahau, Taarabt ni miongoni mwao, alipofichua hilo kupitia kolamu yake kwenye gazeti la Daily Mail mwaka 2020.

"Tulikuwa pamoja Tottenham alipokuwa kijana mdogo na kuonyesha ujuzi na ufundi wake uwanjani, alipenda zaidi kupiga matobo mabeki wa timu pinzani kuliko kupiga pasi ya maana. Alikuwa na uwezo mkubwa, lakini hakujipata," alisema Crouch.

Rekodi zake huko QPR, Taarabt alicheza dakika 11,630 katika mechi 164 akifunga mabao 34 na kuasisti 42 kwa mujibu wa Transfermarkt.

Chanzo: Mwanaspoti