Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapeni Yanga Kombe lao

Aucho Moloko Wapeni Yanga Kombe lao

Sun, 7 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga iko moto uwanjani, imeendelea kulifukuzia taji la 29 baada ya juzi kuwachapa Singida Big Stars kwao kwa mabao 2-0 na kubakiza alama tatu tu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo.

Maneno rahisi ambayo unaweza kuyatumia baada ya mchezo huo ni kwamba Yanga walikuwa bora uwanjani katika muda mwingi wa mchezo wakiwazima Singida kirahisi lakini pia walihitaji makosa yao wenyewe kutofunga mabao zaidi.

Ndani mtiti nje Mtiti

Yanga licha ya kuanza na mabadiliko mengi katika kikosi chake cha kwanza lakini bado walicheza kwa heshima kama timu inayotaka ubingwa, ingawa haikuupiga mwingi kama ilipoichakaza 4-1 timu hiyo katika mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambako, Fiston Mayele alifunga 'hat-trick' yake pekee hadi sasa kwenye ligi.

Kikosi cha kocha Nasreddine Nabi kilianza na Kennedy Musonda, Jesus Moloko, Stephanie Azizi KI na Clement Mzize ambao walianza mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers ya Nigeria, lakini bado wakatengeneza ushindi wao wakitumia dakika 45 za kipindi cha kwanza pekee.

Mapema Yanga walionyesha kuhitaji ushindi walifanya mashambulizi matatu ya nguvu lakini kipa wa Singida, Benedict Haule alikuwa imara kabla ya kujaribu kiwango chake dakika ya 15 kupitia bao la Aziz KI.

Yanga walikamata kiungo

Kazi kubwa kwa Yanga katika kuizima Singida ilifanyika eneo la kiungo kupitia kazi ya Zawadi Mauya na mwenzake Khalid Aucho huku wakipata msaada kutoka kwa mawinga waliocheza pembeni Musonda na Moloko.

Mauya alikuwa na kazi bora kuwafanya Singida wasiwakaribie kwa makali mabeki wao wa kati huku Moloko na Musonda wakirudi mpaka kati na wakati mwingine chini kabisa kupokonya mipira na kuifanya timu kucheza kwa mizania sawa inapokuwa na mipira na wakati haina.

Singida butu mbele

Katika timu za Top 4 ambazo zimejihakikishia kucheza michuano ya Caf msimu ujao, Singida BS ndiyo iliyofunga mabao machache zaidi ikiwa na 32, yaani mabao 12 nyuma ya Azam iliyo katika nafasi ya tatu -- na tatizo hilo lililonekana juzi dhidi ya Yanga kwani washambuliaji wao walipoteza nafasi nyepesi.

Kiungo wao wa Kibrazil, Bruno Gomes ndiye kinara wao wa mabao akiwa na mabao 9, straika wao Meddie Kagere ana mabao 7, lakini straika aliyeibuka mfungaji bora kwenye Kombe la Mapinduzi waliyemsajili katika dirisha dogo, Fancy Kazadi, amepotea kabisa akiwa hana bao hata moja kwenye Ligi Kuu.

Ukuta jiwe Yanga

Baada ya mchezo wa robo fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United, Yanga ilianza tena na ukuta wa wazawa pale nyuma ukiwa na mabeki Dickson Job, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca' ambao wameendelea kuwa na kiwango bora na kuitoa tena timu yao bila kuruhusu bao.

Na Djuma Shabani alipoingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Job, ukuta huo uliendelea kuwa mzito kwa Singida ambao walipata wakati mgumu kukamilisha mashambulizi yao kwa mafanikio.

Mikono salama

Ukiacha ubora wa Diarra katika kudaka vyema na ubora wa umiliki wa mpira kwa kutumia miguu, kitu kingine kwa kipa huyu raia wa Mali ni jicho lake la haraka anapoona nafasi mbele kama alivyokuwa sehemu ya kupika bao la pili la timu yake.

Diara alimuona kwa haraka Moloko na kumpigia pasi ndefu iliyofika ambapo winga huyo alimkimbiza Shafiq Batambuze kisha akapiga krosi iliyomkuta mfungaji Mzize na kufunga kwa umakini na kuifanya Yanga kutumia pasi mbili tu hadi kufunga bao.

Ukitazama kiwango cha Diara na mateso waliyokutana nayo Singida kwa kipa wao kwenye mchezo huo utagundua timu hizo mbili zina makipa wenye utofauti mkubwa wa ubora. Haikushangaza mechi ya juzi kuwa ni 'clean sheet' ya 15 ya Diarra ambayo inamhakikishia kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka kwa msimu wa pili mfululizo. Anayemfuatia ni Aishi Manula wa Simba mwenye 'clean sheet' 11 na zimebaki mechi 3.

Msikie Hans Pluijm

Kocha wa Singida, Hans Pluijm hakumung'unya maneno akiwataja wachezaji kumuangusha kwa kucheza kwa nidhamu ndogo iliyowatengenezea ushindi wapinzani wao.

"Ukifanya makosa kama yale hasa wakati unacheza na timu bora kama Yanga lazima utaadhibiwa, hatukucheza kwa nidhamu tuliwaachia nafasi ya kufanya uamuzi, angalia bao la kwanza lile ni kosa la kipa wetu," alisema Pluijm ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga.

Kaze huyu hapa

Naye kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze licha ya kuwapongeza wachezaji kwa kucheza kwa ubora mkubwa alisema mzunguko wa wachezaji wao katika mchezo mmoja kwenda mwingine umeendelea kuwapa matokeo mazuri.

"Wachezaji wetu walicheza vizuri sana, tulitengeneza nafasi nyingi lakini pia tulizuia kwa hesabu nzuri, tuliwapumzisha baadhi ya wachezaji kutokana na mechi ngumu tulizo nazo mbele lakini bado tukawa bora," alisema Kaze.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live