Watu wengi nchini Rwanda wamekuwa wakielezea furaha yao kuingia katika uwanja wa michezo wa Amahoro uliofanyiwa ukarabati kwa mara ya kwanza wenye uwezo wa kuwapokea watu 45,000.
Katika hafla iliyoitwa "Peaceful Meeting" kuuwasilisha kwa umma uwanja huo kwa mara ya kwanza, ambao umekarabatiwa kwa miaka miwili, mechi ya mpira wa miguu iliandaliwa mwishoni mwa juma kati ya Rayon Sports na APR FC, timu maarufu zaidi nchini Rwanda, ambayo ilimalizika kwa 0- 0.
Hadi siku moja kabla ya mechi, tikiti za kuingia ambazo ziliuzwa mtandaoni kwa 1,000Frw na 10,000Frw ziliuzwa, na kubakiwa na tikiti za malipo ya 125,000Frw, kulingana na wizara ya michezo.
Shughuli ya leo ilikuwa ni kuukabidhi uwanja huu kabla ya kufunguliwa rasmi na mamlaka katika hafla iliyopangwa kuadhimisha siku ya ukombozi tarehe 4 mwezi wa saba.
Zaidi ya magwiji 150 wa soka wanatarajiwa kuchuana katika uwanja huo mjini Kigali, Rwanda, mwezi Septemba kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya Vilabu vya wachezaji wa zamani(VCWC 2024).
Michael Owen, Jay Jay Okocha, Ronaldinho, Robert Pires, Roger Milla, na Andrew Cole ni baadhi tu ya magwiji mashuhuri wanaotarajiwa kupanda uwanjani, wakileta uzoefu mwingi na mapenzi kwa mchezo huo. Michuano hiyo itatumika kama ufunguzi rasmi wa Uwanja mpya wa Amahoro uliofanyiwa ukarabati, uwanja wa kisasa ambao umefanyiwa mabadiliko.