Mmesikia? Manchester United imeripotiwa kuweka ubaoni majina ya mastraika watatu wanaotaka kuwasajili kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, akiwamo mkali wa Tottenham Hotspur, Harry Kane.
Man United inafanyia kazi usajili wa straika Wout Weghorst kwenye dirisha hili la Januari ili awafikishe mwisho wa msimu na hapo watakuja na orodha ya washambuliaji wengine ambao wapo kwenye rada ya kocha Erik ten Hag.
Weghorst ambaye pia ni Mdachi kama ilivyo kwa kocha wa Man United, alifunga mabao mawili akiwa na Uholanzi kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2022 huko Qatar dhidi ya Argentina, kwa sasa yupo kwa mkopo Besiktas akitokea Burnley. Man United inahitaji straika mpya dirisha hili baada ya kuachana na Cristiano Ronaldo aliyetimkia Al-Nassr.
Kwa mujibu wa ESPN, Man United ina majina matatu ya mastraika ambao imewaweka kwenye kipaumbele cha kuwasajili kwenye dirisha kubwa la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Straika wa Napoli, Victor Osimhen na Benjamin Sesko - ambaye alijiunga na RB Leipzig akitokea Red Bull Salzburg, ni majina mengine kwenye orodha hiyo ya wanaosakwa na Man United.
Lakini, kuwapo kwa straika wa Spurs na England, Kane kutawafutia zaidi Man United kumweka kwenye mpango wao wa msimu ujao kwa maana ya kunasa saini yake kwenye dirisha lijalo. Mkataba wa Kane, 29, utafika tamati 2024.
Kane alikaribia kujiunga na Manchester City kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2021, wakati kocha Pep Guardiola alipohitaji huduma yake, lakini mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alizuia dili hilo kukamilika.
Man United imesajili mastraika wa maana kwelikweli kwa miaka ya karibuni ikiwamo Radamel Falcao, Zlatan Ibrahimovic, Odion Ighalo, Romelu Lukaku, Edinson Cavani na Cristiano Ronaldo.