Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanne wawekwa pembeni, Mbeya City, Lule acharuka

Mbeya Cityy.jpeg Wanne wawekwa pembeni, Mbeya City, Lule acharuka

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mbeya. Baada ya kuambulia kipigo katika mchezo uliopita, leo Alhamisi kikosi cha Mbeya City kimeendelea na mazoezi yake kujiandaa dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo utakaopigwa Jumapili katika uwanja wa Sokoine jijini hapa, huku wachezaji wanne wakipewa programu maalumu.

Katika mchezo uliopita City ilichezea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Namungo, ambapo Jumapili hii watakuwa tena uwanjani kuwavaa ndugu zao, Prisons walio mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa alama 11.

Hata hivyo mchezo huo unatarajia kuwa wa visasi na heshima kwani City watahitaji kuendeleza rekodi ya ushindi, huku Wajelajela wakisaka alama tatu ili kufuta uteja na kujikwamua mkiani na kufanya timu hizo kuwa na maandalizi ya ukweli ili kufikia malengo.

Prisons chini ya Kocha wake, Patrick Odhiambo haijapata ushindi wala sare katika mechi nne za Ligi Kuu wakicheza vichapo tu, hivyo kufanya mpambano huo kuwa wa kufa na kupona kusaka ushindi wa kwanza ili kurejesha matumaini kwa mashabiki na mabosi lakini zaidi kulinda kibarua chake.

Katika mazoezi ya leo kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga, timu hiyo ilionekana kuelekeza nguvu kwenye pumzi, pasi na kufunga mabao, huku Kocha wa timu hiyo, Mathias Lule akiwafokea nyota wake walioonekana kutofuata maelekezo yake.

Pia Lule aliwatenga wachezaji wanne, mabeki David Mwasa aliyerejea baada ya kukaa nje muda mrefu akiuguza majeraha, Hamad Waziri na Seleman Boban pamoja na Straika Juma Luizio ambao walikuwa na programu yao maalumu walijikita kukimbia kuuzunguka uwanja.

Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Lule amesema anafahamu mchezo huo kuwa na ushindani lakini matarajio yao ni kusahihisha makosa yao na kupata alama tatu na kurudi nafasi yao ya nne huku akifafanua kuwa anaamini vijana wake watafanya vizuri.

"Kipigo cha juzi dhidi ya Namungo kimetuamsha, tunaendelea na maandalizi kuhakikisha mchezo ujao na Prisons tunapata matokeo mazuri, tulifanya makosa ambayo yalitugharimu hivyo hatutarajii kuyarudia" amesema Lule.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz