Polisi nchini Uhispania wamewakamata watu wanne wanaoshukiwa kuning'iniza sanamu ya mchezaji wa Real Madrid, Vinicius Jr, kutoka kwenye daraja la Madrid.
Sanamu hiyo hiyo ilionekana Januari kabla ya mechi kati ya Real na wapinzani wao katika mji mkuu, Atletico.
Ilitundikwa kwa shingo yake chini ya bendera isemayo: "Madrid inachukia Real".
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, ambaye ni mweusi, alikumbana na dhuluma za rangi na mashabiki wa timu pinzani wakati wa mchezo wa La Liga wikendi. Klabu yake iliwasilisha malalamiko ya uhalifu wa chuki.
Mechi ya Real huko Valencia Jumapili ilisitishwa katika kipindi cha pili huku Vinicius aliyekasirishwa akiwaripoti mashabiki wa upinzani kwa mwamuzi.
Kufuatia mechi hiyo, ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 baadaye alitolewa kwa kadi nyekundu kwa kufanya vurugu, alisema: "La Liga ni ya wabaguzi."
Rais wa La Liga, Javier Tebas alijibu kwenye Twitter kwa kusema Vinicius hakufika mara mbili kwa mkutano wa kujadili kile "kinachoweza kufanyika katika kesi za ubaguzi wa rangi", na kuongeza: "Kabla ya kuikosoa na kukashifu La Liga, unahitaji kujijulisha ipasavyo. "
Lakini mkuu wa shirikisho la kandanda Luis Rubiales alisema soka la Uhispania lilikuwa na "tatizo kubwa ambalo pia linatia doa timu nzima, kundi zima la mashabiki, klabu nzima, nchi nzima".
Waendesha mashitaka wa Uhispania sasa wataamua ikiwa watafuatilia uchunguzi wa jinai.
Vinicius amekuwa akilengwa na unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi mara nyingi msimu huu na serikali ya Brazil ilisema tukio hilo ni "kipindi kingine kisichokubalika".