Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha ameziomba kamati za michezo za mikoa kuwezesha kikamilifu ushiriki wa wanariadha wa mikoa katika mashindano ya siku mbili ya riadha kwa wanawake ya Ladies First yanayoanza Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yanaratibiwa na BMT kwa kushirikiana na Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan [JICA].
Msitha pia amelitaka Shirikisho la riadha Tanzania (RT) kuyasimamia kwa weledi.
Mashindano hayo yanafanyika nchini kwa mara ya nne yakilenga kuibua na kuboresha viwango vya wachezaji wa kike yatashirikisha wanariadha 186 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Tayari baadhi ya timu zimeanza kuwasili ikiwamo ya Arusha, huku zile za Mara na Simiyu zikitarajiwa kuwasili Dar es Salaam wakati wowote kuanzia sasa tayari kwa mashindano hayo.
"Maandalizi yako katika hatua za mwisho, muitikio ni mkubwa na Baraza tunaishukuru JICA kwa mchango wao katika kudhamini mashindano haya kwa msimu wa nne sasa wakigharamia kwa zaidi ya asilimia 80 kwenye malazi, chakula na gharama nyingine zote za uendeshaji wa mashindano hayo," amesema.
Mwakilishi wa JICA nchini, Naofumi Yamamura amesema kuwa, lengo kuu la mashindano hayo ni kuhakikisha jamii inapata uelewa juu ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya michezo na kueleza kuwa, wataendeleza ushirikiano na Tanzania katika kukuza sekta ya michezo.
Awali, baadhi ya washindi wa mashindano hayo waliwahi kuiwakilisha nchi kwenye moja ta mbio nchini Japan, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo zaidi katika nyanja ya kimataifa.