Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaumee... Wababe wanane wa Afrika hawa hapa!

Simba Yanga WA0007 Wanaumee... Wababe wanane wa Afrika hawa hapa!

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mzizi umekatwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupigwa mechi za mwisho za makundi wikiendi iliyopita na kushuhudiwa Simba na Yanga zikiandika rekodi mpya CAF kupenya zote kwa pamoja hatua ya robo fainali.

Kabla ya hapo haikuwahi kutokea kwa Tanzania kuingiza timu mbili kwa wakati mmoja kwenye hatua hiyo, lakini safari hii vigogo hivyo vimekomaa na kupenya vikishika nafasi ya pili kila moja katika kundi B na D na sasa vinasikilizia timu za kucheza nazo ili kusaka tiketi ya nusu fainali mara baada ya droo kufanyika wiki ijayo.

Yanga iliyokuwa Kundi D ilitangulia mapema wiki iliyopita ilipoifyatua CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 4-0 kabla ya Ijumaa kupoteza ugenini kwa vinara na watetezi wa taji la michuano hiyo Al Ahly kwa bao 1-0 jijini Cairo, Misri.

Watani wao wa jadi, Simba yenyewe ilipenya juzi usiku baada ya kuifumua Jwaneng Galaxy ya Botswana na kulipa kisasi cha misimu miwili iliyopita, kwa kumaliza pia nafasi ya pili nyuma ya Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyokata tiketi mapema licha ya juzi kufungwa bao 1-0 na Wydad Casablanca ikiwa ugenini, huko Morocco.

Kitendo cha Simba na Yanga kumaliza makundi yao zikiwa nafasi ya pili ni dhahiri zitacheza na timu zilizomaliza kinara katika makundi mengine jambo linaloonyesha kazi ipo kwa wawakilishi hao wa Tanzania kutokana na aina ya wapinzani wao.

WABABE WANANE

Mechi hizo za wikiendi zimekamiolisha orodha ya timu nane zilizopenya hatua ya robo fainali na kinachosubiriwa kwa sasa ni kujulikana nani atakutana na nani mara baada ya droo kwa ajili ya kuanza msako wa tiketi ya nusu fainali ambapo wababe wanne tu ndio watakaopenya ili kusaka taji hilo linaloshikiliwa na Al Ahly.

Mbali na Simba na Yanga kutoka Tanzania zilizomaliza kwenye nafasi ya pili ya makundi ya B na D, nyingine zilizopita hatua hiyo ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyoongoza Kundi A ikifuatiwa na TP Mazembe ya DR Congo, huku Asec Mimosas ikiongoza Kundi B ikifuatiwa na Wekundu wa Msimbazi.

Kundi C limeongozwa na Petro Atletico de Luanda ya Angola ambayo imeweka rekodi ya kutoruhusu bao hata moja kwenye hatua hiyo, ikifuatiwa na Esperance ya Tunisia, wakati watetezi na mabingwa wa kihistoria wa taji hilo, Al Ahly ya Misri iliongoza Kundi D lililokuwa pia na Vijana wa Jangwani.

Ukiziondoa Simba, Yanga na Petro Atletico, ambazo hazijawahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya Afrika, timu nyingine tano zilizosalia wamewahi kutwaa ubingwa na kuonyesha namna gani robo fainali ijayo itakuwa ya aina yake kwani kuna uwezekano wa wababe hao kukutana wenyewe kwa wenyewe na kung'oa kabla ya nusu fainali.

HALI KWA YANGA

Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi imeandika rekodi mpya baada ya kutinga hatua hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika histori ya timu hiyo tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika 1997.

Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza hatua ya robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.

Timu hii ilimaliza kundi 'D' ikiwa nafasi ya pili na pointi nane sawa na CR Belouizdad ya Algeria ila Yanga ilinufaika tu na faida ya jinsi zilivyokutana zikiwa nyuma ya mabingwa mara 11 wa michuano hiyo, Al Ahly iliyomaliza na pointi 12.

Katika kundi hilo, Medeama kutoka Ghana ndiyo iliyoburuza mkia baada ya kujikusanyia jumla ya pointi nne katika michezo sita.

Kutokana na hilo ni dhahiri Yanga inaweza kukutana na ASEC Mimosas kutoka Ivory Coast ambayo ndiyo iliyoibuka kinara wa kundi 'B' na pointi zake 11 huku miamba mingine ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Petro de Luanda kutokea Angola.

Mamelodi Sundowns ilimaliza kinara wa kundi 'A' na pointi 13 nyuma ya TP Mazembe ya DR Congo iliyomaliza na pointi 10 huku FC Nouadhibou ya Mauritania na Pyramids anayoichezea nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele zikimaliza na pointi tano.

Petro de Luanda ilikuwa kinara kundi 'C' na pointi 12 nyuma ya Esperance ya Tunisia iliyomaliza ya pili na pointi 11 huku Al Hilal ya Sudan ikishika ya tatu na pointi tano wakati Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia ikiburuza mkia na pointi nne.

Petro imeandika rekodi mpya ya timu ya kwanza kucheza michezo sita ya hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila ya kuruhusu bao ambapo katika mechi hizo kikosi hicho anachochezea nyota wa zamani wa Yanga, Carlinhos kimefunga mabao matano.

SIMBA YENYEWE

Simba iliyotinga hatua ya robo fainali ya CAF kwa mara ya tano katika kipindi cha miaka sita, ilimaliza nafasi ya pili na pointi tisa sawa na Wydad Casablanca ya Morocco huku Jwaneng Galaxy ya Botswana ikiburuza mkiani na pointi nne.

Kinara wa kundi hilo alikuwa ni ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambayo ilikuwa na jumla ya pointi 11 baada ya michezo yake sita.

Kwa mantiki hiyo, Simba katika hatua ya robo fainali inaweza kupangwa na Mamelodi Sundowns na Petro de Luanda ambazo pia ni timu zinazoweza mojawapo kupambana na Yanga huku ikiongezeka tu Al Ahly ambayo hata hivyo zilishakutana mara nyingi.

Kumbukumbu ya haraka kwa Simba na Al Ahly zilikutana Oktoba 20, mwaka jana kwenye michuano mipya ya African Football League ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Dar es Salaam zilifungana mabao 2-2 kisha marudiano Oktoba 24 kufungana 1-1.

Sare ya 1-1 ndiyo iliyowafanya mabingwa hao Al Ahly kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kunufaika na bao la ugenini.

Simba tangu ilipocheza nusu fainali enzi za Klabu Bingwa mwaka 1974, haijawahi kuifikia tena hatua hiyo, kwani mara tano tofauti imeishia robo fainali, ikiwamo ya 1994 kabla ya mfumo kubadilishwa na 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mkuu Mualgeria, Abdelhak Benchikha kimewahi kucheza pia makundi mwaka 2003, mbali na kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwaka 2021-2022 na fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.

Benchikha ana kibarua cha kuifikisha Simba mbali ikiwezekana kuifikia rekodi ya mwaka 1974 na ile ya 1993 ilipocheza fainali ya CAF, michuano iliyokuja kuunganishwa na ile ya Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika kwa sasa.

MSIKIE MAPUNDA

Akizizungumzia Simba na Yanga katika mashindano hayo, kipa wa zamani wa Yanga na Simba, Ivo Mapunda amepongeza uwekezaji wa wachezaji bora waliopo katika timu hizo.

"Hii inaonyesha ni jinsi gani timu za Tanzania kwa sasa zimekuwa tishio kwa sababu ya uwekezaji uliofanyika. Ukiangalia miaka ya nyuma na hapa tulipo unaona wazi tumepiga hatua kubwa ndio maana tunapambana na yoyote bila kujali," amesema.

Mapunda ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Biashara United aliongeza kuwa licha ya kujivunia mafanikio hayo, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika hatua ya robo fainali kutokana na aina ya wapinzani ambao timu hizo zinaenda kukutana nao.

Chanzo: Mwanaspoti