Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanasoka wazawa wanamhitaji Khaligraph wao

Duchu Uturuki Wanasoka wazawa wanamhitaji Khaligraph wao

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mitandaoni wiki chache zilizopita jambo lililokuwa ‘linatrendi’ ni wasanii wa muziki wa hip hop Tanzania kuwashiana moto na rapa kutoka Kenya Khaligraph Jones.

Hiyo ni baada ya Kaligraph kuwachana wanahiphop wa Bongo kuwa wamelala na kuwapa saa 24 kuonyesha kuwa hawajalala, na iwapo baada ya muda huo wakishindwa atavamia muziki wa hip hop Tanzania na ndani ya muda mfupi atakuwa mfalme wao Bongo.

Jambo hilo ni kama liliwafika vyema wasanii wa hip hop nchini kwani baadhi yao waliingia studio na kuonyesha umwamba wao kwa kutoa ngoma kali kumjibu Khaligraph na nyingine kumchana jamaa huyo kutoka Kenya ‘Dis tracks’.

Baadhi ya mastaa waliomjibu Khaligraph kwa nyimbo ni Rosa Ree, Songa, Motra the Future, Orbit Makaveli, Young Killer, Fresh Like Uuuh na wengine kibao lakini pia Khaligraph alitoa ngoma iliyozungumza mengi kuhusu kile anachodai ‘kulala’ kwa gemu ya hip hop Bongo.

Achana na hip hop sasa turudi kwenye soka. Huku nako wachezaji wengi wazawa (sio wote) wanamhitaji mtu kama Khaligraph atakayewachana na kuwaamsha kutoka usingizini.

Mastaa wazawa wengi kwenye Ligi Kuu wamelala. Hadi sasa ukiangalaia namba kwenye mechi mbili au tatu za mwanzo utawapata wazawa wachache kwenye namba za juu, hususan katika timu kubwa. Pale kwenye ufungaji bora anaongoza mzawa Feisal Salum mwenye mabao matatu, lakini ukitafuta wachezaji wengine wenye walau mabao mawili wazawa utawapata Matheo Antony wa Mtibwa, Adam Adam wa Mashujaa ilhali wengine ni wageni Stephane Aziz KI, Jean Baleke, Max Nzengeli na Prince Dube. Hali ipo hivyo hata kwenye asisti kwani anayeongoza ni Msenegali Cheikh Tidiane Sidibe, beki wa kushoto wa Azam.

NAMBA SIMBA, YANGA

Licha ya Ligi Kuu kuwa na timu 16, lakini Simba na Yanga ndizo timu zenye mashabiki wengi na ushawishi mkubwa - zikiwa pia ndizo vinara wa kutwaa taji la ligi, Yanga ikibeba mara 29 ikifuatiwa na Simba iliyochukua mara 22.

Pamoja na kuwa kila timu inaruhusiwa kusajili wachezaji 12 wa kigeni huku wazawa wakiwa hawana idadi, lakini bado wengi wameshindwa kupenya kwenye vikosi vya timu hizo licha ya wingi wao. Tangu kuanza kwa msimu huu, Yanga kwenye mechi zote za mashindano ilizocheza hadi sasa hakuna siku wameanza wachezaji wazawa zaidi ya sita kwa mpigo. Mara nyingi wamekuwa wakianza wanne, watatu au watano.

Mudathir Yahya, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto na Nickson Kibabage ndio wazawa wenye uhakika wa kucheza dakika nyingi kwenye kikosi cha Yanga wengine ‘kazini kwao kuna kazi’, kama asemavyo Kibwana Shomary beki wa pembeni kwa Wanajangwani hao ambaye kwa sasa anasota benchi baada ya ujio wa Muivory Coast, Attohoula Yao.

Upande wa Simba hali iko hivyo pia katika mechi za mashindano msimu huu hakuna hata moja ambayo wazawa wameanza zaidi ya sita kwenye kikosi cha kwanza. Wengi ni wageni na hata mabadiliko yakifanyika, wanaopata zaidi nafasi ni ‘wakuja’.

Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Ally Salim ndio wazawa wenye uhakika wa kucheza dakika nyingi ndani ya kikosi cha Simba, wengine bado hakijaeleweka.

Hata hivyo sio Simba na Yanga tu, bado wazawa wengi wameshindwa kutoa ushindani wa kutosha kwa wageni walio katika timu tofauti za Ligi Kuu Bara.

Singida Big Stars, Azam na Tabora United ni miongoni mwa timu za Ligi Kuu ambazo vikosi vyao vya kwanza vinatawaliwa na wachezaji wa kigeni wengi ilhali wazawa wapo wengi.

Mwamko mkubwa unahitajika kwa wazawa wengi wao kwa sasa wameishia kuishi kwa lawama bila kukumbuka mpira ni mchezo wa wazi na ukifanya vizuri lazima uonekane.

Hata hivyo lililo dhahiri ni kwamba, wageni wapo ili kuwaamsha wazawa na wazawa wanapaswa kuamka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live