Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanasoka hawa wanapeta na umri wa miaka 30+

Cristiano Ronaldo Madrid Career Wanasoka hawa wanapeta na umri wa miaka 30+

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Yanga inamnyakua kiungo wa Simba, Jonas Mkude, katika msimu huu baadhi ya wadau wa soka walinyoosha kidole kuonya usajili huo wakisema ni mchezaji mzee yaani umri wa 30+.

Haishangazi kwani ni kawaida kwa wachezaji wa soka duniani wanapofikisha umri miaka 30 kuanza kuitwa wazee hii ni kutokana na sababu za kitaalam kuwa mwili nao unakuwa umegota ukuaji.

Katika michezo ya UEFA ya wiki hii tumeona katika vikosi mbalimbali vya timu za taifa za Ulaya bado zikiwa na wanasoka wenye umri wa miaka zaidi ya 30+ ambao bado wako timamu kuzibeba timu zao za taifa.

Klabu mbalimbali zinazojiendesha kibiashara kama zile za Ligi Kuu barani Ulaya ambazo huwalipa mishahara mikubwa wachezaji wao katika mikataba wanayowapa huwa na kipengele cha umri ambacho wengi hutoa mkataba wa muda mfupi kwa wenye umri wa zaidi ya miaka 30.

Tumeona kwa mastaa wa soka wa klabu ya Inter Miami, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo wa Al Nassr, Robert Liwandoski wa Barcelona, Thomas Muller wa Bayern Munich na Luca Modrid wa Real Madrid kuwa umri wa 30+ si kikwazo cha wao kushindwa kucheza kwa kiwango bora.

Ukiacha Muller, wachezaji hawa ambao kila mmoja ana makombe kadhaa na huku pia wote wakifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanaendelea kutamaniwa na klabu zao za zamani.

Mfano klabu ya Barcelona imekuwa ikitupa ndoana kumnasa mchezaji wake wa zamani Lionel Messi ambaye anaonekana kutamani kujiunga klabu yake hiyo aliyoitumikia tangu akiwa kinda.

Umri wa miaka 30+ unaonekana kufumbiwa macho hii ni kutokana na mafanikio wanayoyapata baadhi ya mastaa ambao wanacheza ligi za Ulaya.

Ukitazama baadhi ya timu za taifa za Ulaya zilizochezwa wiki hii utaona mastaa wenye umri wa miaka 30+ wakiendelea kutumika na klabu na timu za taifa ikiwamo Ronaldo, Lewandowski, Modric na Muller.

Ingawa ni kawaida kwa klabu za Ulaya kujihami na umri kwa kuweka utaratibu wa kuwapa mkataba wa muda mfupi wa mwaka mmoja mmoja kwa wachezaji ambao tayari umri wao umeishavuka miaka 30.

Ni kweli kabisa kwa tafiti za soka zinaonyesha wachezaji walio wengi wanapofikisha umri wa miaka 30+ viwango vya uchezaji huanza kuporomoka.

Wachezaji wa kulipwa waliofikia umri huu walianza kucheza katika ligi hizo za kulipwa wakiwa na umri wa miaka miaka 18 na huku wengine wakianza katika shule za soka za klabu hizo wakiwa makinda.

Hii inatoa picha kwa mchezaji kama Ronaldo, Messi, Muller, Modric na Lewandowski walianza kuwa na makali soka wakiwa vijana wa umri wa miaka 17 na wamedumu kwa miaka zaidi ya miaka 10 mpaka kufikia 30+.

Katika miaka hiyo waliyotumikia klabu zaidi ya mbili miili ya wachezaji hawa inakuwa umetumika sana na huku pia wakikumbana na majeraha mbalimbali ambayo huwaweka nje kwa siku kadhaa.

Lakini uimara na kudumu kwa wachezaji hawa wakiwa na kiwango kile kile hutofautiana mchezaji na mchezaji ikiwamo asili ya mwili, aina ya mazoezi au mfumo wa mafunzo, majeraha anayopata, lishe, kuugua magonjwa mengine na mienendo na mitindo ya kimaisha anayoishi.

Vile vile kudumu huko kunaweza kuchangiwa na ligi wanazocheza, mazingira ya kijiografia ya nchi au ligi anayocheza na huduma za matibabu wanazopata pale anapokuwa mgonjwa au majeruhi.

Wachezaji hawa wamekuwa mfano bora wa wanasoka ambao umri wa miaka 30+ umeonekana kuwa umri si kikwazo cha kutimiza majukumu yao ya uwanjani.

Mfano Lionel Messi aliipata mafanikio makubwa katika Kombe la Dunia la FIFA 2022 lililofanyika Qatar akiwa na umri wa miaka 35 alipotwaa Kombe la Dunia na kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.

MIAKA 30+ NA KUCHEZA KUKO HIVI

Kwa kawaida viungo vya mwili wa binadamu ikiwamo maungio, misuli, mifupa, mishipa ya fahamu na damu hupungua uimara kadiri umri unavyosonga.

Kitabibu viungo vya mwili kama vile mifupa ukuaji wake kwa wanadamu wengi huishia pale mtu anapofika umri wa miaka 25. Umri ukishapiga hatua hata mfumo wa usagaji chakula nao unakuwa dhaifu kiutendaji.

Pia ipo tofauti kubwa kwa mchezaji aliye majeruhi mwenye umri wa chini ya miaka 30 na yule mwenye zaidi ya miaka 30, hapa anayepona majeraha mapema ni mwenye umri mdogo.

Moja ya vitu ambavyo vinachangia kutopona majeraha kwa wakati ni umri wa mchezaji majeruhi hii ni kutokana viungo hivyo vinakuwa vimetumika sana na kuchakaa.

Pamoja ya kwamba tishu za mwili wa binadamu hufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa sana lakini pale zinapofanyishwa kazi kupita kiasi huweza kuwa chanzo cha wanasoka wa aina hii kupata majeraha.

Kadiri mwili unavyotumikishwa ndivyo pia unakuwa katika hatari zaidi ya kupata majeraha mbalimbali ikiwamo ya misuli, mifupa na nyuzi ngumu yaani ligamenti na tendoni.

Ili mchezaji kuweza kumudu jambo hili umri alionao una maana kubwa, wanasoka wanapofikisha umri zaidi ya miaka 30 tayari mwili unakosa uimara ukilinganisha wanapokuwa na umri wa miaka 17-30.

Wachezaji wanapotumika sana miili yao huweza kuambatana na majeraha wakati wanashiriki mazoezi na mashindano mbalimbali. Messi ni mmoja wa wachezaji umri umesogea na pia ametumika kucheza katika mashindano mengi na klabu yake.

Lakini imekuwa bahati hata majeraha wanayopata huwa si makubwa na huwa yanapona kwa wakati, lakini wapo wachezaji wengine wa aina yao ambao waliandamwa na mara kwa mara kwa na majeraha kiasi cha kuamua kuachana na soka ikiwamo Eden Hazard wa Real Madrid.

Kiwango cha uchezaji na uimara wa wanasoka hawa kutoka chini wakiwa na umri huo kumechangia kuendelea kuwa wchezaji wa kutegemewa katika klabu zao na huku wakiendelea kuwindwa na klabu nyingine.

CHUKUA HII

Mchezaji ambaye ana umri wa miaka 30+ anatakiwa kujihami na majeraha yatokanayo na mchezo kwani umri huo tayari ni kihatarishi cha kupata majeraha kirahisi.

Anatakiwa kushikamana na mazoezi ya viungo kabla na baada ya kucheza ili kupunguza hatari ya kupata majeraha. Vile kuzingatia ratiba ya mlo na kupumzika kama kanuni za afya inavyoelekeza.

Mfano Messi na Ronaldo kwenda kucheza ligi isiyo na ushindani ni mbinu nzuri kwa umri huo kupunguza hatari ya kupata majeraha na kulinda viwango vyao.

Ili kudumu na kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu pasipo majeraha mchezaji mwenye umri wa miaka 30+ ashikamane na ushauri wa benchi la ufundi na wataalam wa afya za wanamichezo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live