Shirikisho la riadha la kimataifa la Riadha Duniani limewateua wanariadha watatu wa Afrika kuwania tuzo ya Mwanariadha Bora wa Dunia kwa Wanawake mwaka huu.
Faith Kipyegon wa Kenya na Tigist Assefa na Gudaf Tsegay, wote Muethiopia, ni miongoni mwa wanariadha 11 wa kike walioteuliwa kuwania tuzo za mwaka huu, baada ya kuonyesha utendaji mzuri katika msimu wa riadha wa mwaka huu.
Tigist alishinda mbio za masafa marefu -Berlin marathon mwezi Septemba, na kuweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za marathon za wanawake.
Gudaf pia alishinda mbio za dunia mita 10,000 na Diamond League miya 5,000, ambapo aliweka rekodi ya dunia.
Wachanganuzi wa riadha wanamuunga mkono Bi Kipyegon kama mtu anayepewa nafasi kubwa kushinda tuzo ya mwaka huu baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kuweka rekodi tatu mpya za dunia.
Kulingana na Wanda Diamond League, msimu wa kuvunja rekodi wa Bi Kipyegon umemweka kama "mwanariadha wa kwanza katika historia ya Diamond League kuvunja rekodi ya ulimwengu katika mbio nyingi na wa kwanza kuvunja rekodi zaidi ya moja ya ulimwengu katika msimu mmoja".
Winfred Yavi mzaliwa wa Kenya, ambaye alibadili uraia wake na kuwakilisha Bahrain, pia yuko katika kinyang'anyiro cha tuzo hiyo ya kifahari.
Washindi watatangazwa tarehe 11 Disemba baada ya kujumlisha kura zilizopigwa na mashabiki na maafisa wa Riadha wa Dunia.