Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaomkejeli Mukwala leo watamshangilia kesho

Steven Mukwala SimbSC.jpeg Steven Mukwala

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huko mitaani kwa sasa usajili unaojadiliwa sana vijiweni ni ule wa straika mpya wa Simba, Steven Mukwala aliyetua hivi karibuni akitokea, Asante Kotoko ya Ghana.

Kuanzia vijiwe vya kahawa, vile vya daladala hadi katika mitandao ya kijamii ni ishu nzima ya usajili wa Mukwala ndani ya Yanga kupitia dirisha kubwa lililofungwa katikati ya mwezi huu.

Mashabiki wamegawanyika, kuanzia wale wa Msimbazi hadi kule Jangwani, wanamkejeli kwelikweli staa huyo kutoka Uganda. Wale wa Yanga wanasema watani wao wamsajili Yikpe aliyechangamka na wengine wakimfananisha na Hafiz Konkoni, mmoja ya washambuliaji waliowahi kutua Yanga na kuchemsha.

Wenzao wa Simba wenyewe wanaguna na kuona kama wamepigwa vile katika usajili huo wakishangaa kuachwa kwa Freddy Michael Koublan na kuletwa Mukwala ambaye hadi sasa hajafanya maajabu.

Wengi wanamuona kama ni mchezaji asiye sahihi kutua Simba na hasa baada ya kujaza mzuka na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally aliyedai aliyedai jamaa ni mzee wa kutupia tu 'waaaah!

Hata hivyo, kuna baadhi ya mashabiki wa wanaoishabikia Simba wanaunga mkono usajili huo kwa kuamini Mukwala ni ni mchezaji mahiri na atawasaidia pale atakapozoeana na wenzake, huku wanaompinga wanasema mchezaji mzuri anahitaji mpira na sio muda wakimtolea mfano Aweesu Awesu na wenzake.

Wengine wanamtolea mfano Prince Dube aliyetua Jangwani, kuwa, hajahitaji muda isipokuwa kupewa nafasi na kazi ameshaianza huko, kitu gani kinamkwaza Mukwala kama sio wale wale kina Dan Sserunkuma.

Huo ndio, ukweli ulivyo kinachoendelea sasa ni ushabiki tu wa kisoka ambao kwa Simba na Yanga ni mambo ya kawaida na yananogesha soka la Tanzania.

AKIBA YA MANENO

Ni kweli hajafunga bao lolote la mashindano, lakini Mukwala anaonekana ana kitu mguuni. Ni kama ilivyokuwa ikionekana kwa Freddy na Joseph Guede waliosajiliwa diorisha dogo an kuachwa na Simba na Yanga hivi karibuni.

Ukiondoa utani wa jadi na kukosa subira, ukweli ni kwamba mashabiki wa soka wanapaswa kuweka akiba ya maneno kwa Mukwala.

Kiuhalisia Mukwala ana kazi kubwa. Ni kama amepewa changamoto na wajibu wake ni kuwajibu wote wanaomkejeli sasa. Anapaswa kufanya kile alichokifanya Obrey Chirwa alipotua Yanga kwa mara ya kwanza au Joseph Guede aaliyeitumikia mwishoni mwa msimu uliopita.

Pia anaweza kwenda na upepo wa Freddy Michael aliyeonekana wa kawaida kabla ya kufanya mambo hadi alipopewa 'thank you' hivi karibuni.

Kwenye usajili wa nyota hao niliowataja hapo juu walikejeliwa kwa kuonekana wachezaji wa kawaida sana.

Hata hivyo, wote hao waliziba masikio na kuiacha miguu yao iwajibu kwa vitendo wale waliokuwa wakiwakebehi.

Hivi kwa sasa husikii tena kejeli za kina Guede au Freddy...badala yake wamebadilishwa a.k.a anaondoka Simba akiitwa Freddy Funga funga.

Kwanini? Hii ni kwa sababu, wachezaji hao waliamua kufanya kazi yao uwanjani na mashabiki waliowakejeli ndio waliokuja kuwashangilia baadae.

Guede na Freddy kadri walivyokuwa wakifunga ndivyo walivyowapagawisha mashabiki.

Hivyo, hata Mukwala anayebezwa sasa, anaweza kuwanyamazisha mashabiki wote wanaomponda. Achana na umri alionao. Mukwala soka analijua. Mukwala ana kipaji cha soka ndio maana Kocha Fadlu Davids amekuwa akimtumia mara kwa mara katikia kikosi cha kwanza.

Fadlu ni raia wa Afrika Kusini. Hana muda mrefu katika soka la Tanzania. Huenda amemuona Mukwala vizuri mazoezini kule Misri na hata kwa sasa wakiwa pamoja kambini na kupitia mechi chache na kuona ana kitu.

APEWE MUDA

Ni kweli mchezaji mzuri hatakiwi kupewa muda ila mpira tu aufanyie kazi uwanjani, lakini ni wazi jicho la Fadlu limeweza kukiona kipaji cha Mukwala, lakini hata rekodi alizotoka nazo Ghana zinavutia.

Muhimu kwa straika huyo ni kuweka pamba masikioni kama alivyokiri mwenyewe anaishia kwa presha ya ukubwa wa timu, kisha afanye kazi.

Kwa umri alionao Mukwala, kama ataamua kuiacha miguu yake ifanye kazi uwanjani ni wazi atawafunika wote wanaomkejeli, kwa sababu mshambuliaji huyo ana kipaji cha hali ya juu katika soka na kocha yeyote lazima avutiwe naye.

Naamini wale wanaomkejeli leo, huenda ndio haohao ambao ndani ya muda mfupi baadaye watarejea tena kumsifia kama walivyofanya waliowaponda Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco waliokuwa wakiitwa wahenga, ila wakawazima wote kwa mabao waliyokuwa wakifunga hadi walipoondoka Msimbazi.

Hii ni kwa sababu waliamua miguu yao kuwajibu kwa vitendo uwanjani kitu ambacho hata Mukwala naye anapaswa kufanya hivyo na muhimu ni apewe muda tu.

Mukwala asikubali kuruhusu kejeli za mashabiki zimvuruge, acheze soka kwa sababu kipaji anacho na bado ana uwezo mkubwa wa kuwakimbiza mabeki waliopo katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Apunguze presha na kujua Simba ni timu kubwa na inahitaji matokeo zaidi kuliko maneno na huenda akafanikiwa mbele ya safari kama alivyofanya Freddy aliyeondoka Msimbazi na jumla ya mabao tisa, mawili ya Kombe la Shirikisho (FA), moja la Kombe la Muungano na sita ya Ligi Kuu Bara.

REKODI ZILIVYO

Nyota huyo ametua Simba huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko ya Ghana nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga mabao 16.

Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Ghana Desemba mwaka jana akiwa na kikosi hicho cha Asante Kotoko aliyojiunga nayo Agosti 2022 akitokea URA ya Uganda na katika msimu wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.

Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanziamsimu wa 2019/2020 alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na 2020/2021, akafunga 14 kisha 2021/2022 akatupia tena kambani mabao 13, hii ni kuonyesha kuwa sio mchezaji wa kubezwa kwani namba zinambeba.

TUJIKUMBUSHE

Suala la wachezaji kukejeliwa na mashabiki lilishawahi kumkuta pia Simon Msuva. Mashabiki wa Yanga walikuwa wakimponda mno uwanjani mwanzoni aliposajiliwa msimu wa 2012, lakini hadi anaondoka wale wale waliokuwa wakimkejeli ndio, waliokuwa wakienda viwanjani na viroba vya mchele kumpongeza.

Hilo liliwahi pioa kumtokea, Chirwa alipotua Yanga mwaka 2015 na kukaa kwa miezi 10 bila kufunga bao, lakini alipofungua 'code', Yanga waliishia kumuimba hadi alipoondoka kwenda Misri kisha kuibukia Azam.

Pia iliwahi kuwakuta nyota wengine kadhaa wa kigeni waliosajiliwa kwa mbwembwe lakini iliwachukua muda kukaa vizuri, kitu ambacho Mukwala anatakiwa kuishi huko, la sivyo mambo yatamchachia na huenda akizubaa Krismasi ya mwaka huu ikamkuta kwao, japo bado kuna watu wanaamini atajipata muda si mrefu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live