Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaofunga Ramadhani watahadharishwa

Mzizeeeeee Wanaofunga Ramadhani watahadharishwa

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji wa soka wanaoendelea kukinukisha uwanjani huku wakiwa kwenye mfungo mtukufu wa Ramadhani wametahadharishwa na kupewa ushauri wa hatua maalumu za kuchukua ili kulinda afya zao, huku timu nyingine wakizuiwa kufunga kabisa kipindi cha mechi.

Waumini wa dini ya kiislamu duniani kote kwa sasa wapo kwenye mfungo wa mwezi wa Ramadhani ikiwa ni utekelezaji wa nguzo ya nne kati ya tano za dini hiyo, wakiwamo wachezaji wa timu mbalimbali za Ligi Kuu na madaraja mengine wakitimiza nguzo hiyo ya imani na majukumu mengine uwanjani.

Hata hivyo, wataalamu hususani madaktari wametoa maoni na ushauri kwa wachezaji wanaoshuka uwanjani wakiwa na swaumu kwa lengo la kulinda ibada na afya zao kwa jumla.

Wakizungumza na Mwanaspoti baadhi ya madaktari wa timu za Ligi Kuu na Championship walisema mchezaji kucheza mechi ilhali amefunga kiafya si nzuri sana, huku wakitahadharisha na kushauri hatua za kufanya.

Daktari wa Kagera Sugar, Ally Malindi alisema kucheza ukiwa umefunga yapo madhara kiafya ambapo wanashauri ikitokea mchezaji amecheza lazima azingatie vyakula vyenye wanga na sukari ili kurejesha nguvu.

“Japo tunawashauri siku ya mechi wasifunge kwakuwa inatumika nguvu nyingi, ikitokea mtu kwa imani yake akacheza anapaswa kula matunda na tende ili kurejesha nguvu iliyotumika,” alisema Dk Malindi.

Kwa upande daktari wa Mbeya City, Revina Revocatus alisema kutokana na athari kiafya, amewaomba na kushauri wachezaji wake siku ya mechi kutofunga kutokana na nguvu inayotumika.

“Wanapocheza wamefunga, utumbo unaweza kujikunja, kusababisha vidonda vya tumbo, kupoteza kiwango chake uwanjani, hivyo kama akicheza, ale matunda kurejesha maji mwilini,” alisema Dk Revina.

Daktari wa Namungo, Hilal Paul alisema licha kuwa madhara ni madogo lakini wanashauri baada ya mechi mchezaji atumie tende, vyakula au vinywaji vya moto kama chai na uji.

“Wasile chakula kizito kwani mwili utakosa nguvu, wanaweza kutumia vinywaji na ‘bites’ uji au chai ya moto na tende nyingi ili kuongeza sukari kama glukosi ya nguvu ya mwili,” alisema Dk Paul.

Chanzo: Mwanaspoti