Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi mmejiandaaje na maisha bila Mayele

Bye Mayele Fiston Mayele

Sun, 16 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabao 16 ya Ligi Kuu msimu wa kwanza. Mabao 17 ya Ligi Kuu msimu wa pili. Achilia mbali Vikombe alivyoshinda msimu wa kwanza. Achilia mbali vikombe alivyoshinda msimu wa pili. Kama wewe ni nwananchi ukisikia Fiston Mayele anaondoka Yanga, lazima tumbo la uzazi likukate! Lazima pozi zikuishe.

Ni kama kuna kisu kinapasua moyo wako. Ni kama unahisi kuzimia. Ndiyo maisha ya soka yalivyo. Ndiyo utamaduni wake. Ziko tetesi kuwa mshambuliaji wa Yanga, Mayele hatokuwa na mabingwa hao kwa msimu ujao.

Ni tetesi tu. Bado hazijathibitishwa na upande wowote lakini, lisemwalo lipo. Kama sio msimu ujao, basi ipo siku tu. Tetesi zinasema kuna timu moja kutoka Afrika Kusini, na nyingine zinasema kuna timu kutoka Uarabuni. Huku kwa waarabu ndiyo kabaya zaidi. Waarabu wameanza kutingisha soka la Ulaya. Waarabu hawana mkono wa birika. Kwa jicho la kawaida, huwezi kumuona mbadala wa Mayele kirahisi. Ukitazama ligi yetu, unamuona Mayele tu.

Ukitazama ukanda wetu wa CECAFA, bado kuna Mayele mmoja. Kama Mayele anaondoka, Yanga itayumba kuelekea msimu ujao? Jibu ni NDIYO. Kama Mayele ataondoka msimu ujao, YANGA itaanguka? Jibu ni HAPANA. Yanga imepitia mengi.

Imepitia misukosuko mingi sana ya wachezaji na siku zote wanavuka salama. Wananchi, mmejiandaa kwa maisha bila Mayele? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Mayele ni mshambuliaji mzuri sana lakini, hawezi kuingia hata kwenye orodha ya washambuliaji 10 Bora kuwahi kucheza Yanga. Hawezi kufika hata kwenye washambuliaji 20 wa muda wote. Ni kweli zama zinabadilika. Ni kweli kila kizazi na wachezaji wake.

Mayele ni mchezaji muhimu sana kwa Yanga lakini, iko haja ya Yanga kuanza kujipanga na maisha baada ya Mayele. Mayele amekuja Tanzania kwa kuchelewa, ni mtu mzima ambaye huu ndio muda wake wa kutengeneza maisha. Vita ya mpira akishaingia Mwarabu, hakuna anayeiweza. Yule Earling Haaland yuko pale Manchester City, nyuma yake kuna Mwarabu. Yule Kylian Mbappe yuko pale PSG, ni kwa sababu nyuma yake kuna Mwarabu.

Ukisikia Mwarabu hapa unaelewa nini? Ni rahisi tu. Ni watu wenye pesa ndefu za mafuta. Ni watu ambao hawataki faida ya mpira, wao furaha tu inawatosha. Kushindana na mtu anayetumia mabilioni ya pesa kujipa furaha, wakati wewe unataka faida, ni kazi ngumu. Yanga ni lazima waanze kufikiria nje ya boksi.

Yanga ni lazima waanze kujiandaa kisaikolojia. Ukiachana na mabao, Mayele bado ni mtu mwenye nidhamu sana. Kwa msimu wa pili sasa, hakuna ripoti yoyote ya utovu wa nidhamu kutoka kwake. Maisha yake ya kazi yamejaa nidhamu. Maisha yake binafsi, ni mtu anayejilinda na kujiheshimu sana. Ni mara chache sana kumpa mtu wa aina hii. Wananchi, mmejiandaa kwa maisha bila Mayele? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Yanga imewahi kuwa na washambuliaji wengi tu bora kuliko Mayele kwa nyakati zao. Ben Mwalala, Boniface Ambani, Amissi Tambwe, Simon Msuva wote kwa nyakati tofauti wamewahi kufunga mabao mengi sana lakini, kuna namna Mayele amekuwa muungwana sana kwa viongozi, wachezaji wenzie na hata mashabiki. Baada ya kuanza kusikia taarifa za waarabu kuingia rada za Mayele, nimeogopa. Hawa watu wakija, Yanga hawatotoboa kwa Mayele. Mayele ataondoka. Ni muda wa kaunza kujiandaa kisaikolojia. Wachezaji wengi hasa wa kigeni wanapokuwa na ushawishi mkubwa na kuwa tegemeo kwa timu, wengi huanza jeuri. Wengi huanza kiburi na migomo ya hapa na pale.

Huwezi kusikia habari hizo kwa Mayele. Siku zote yuko kazini kupiga kazi. Wananchi, mmejiandaa kwa maisha bila Mayele? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Kuna kila dalili kwamba Mayele hatokuwa na Yanga kuelekea msimu ujao. Inaweza ikawa ngumu kupata mbadala wake wa moja kwa moja lakini, ukapata viungo kama wanne wenye uwezo hata wakufikisha mabao 10 ya Ligi kwa msimu, tayari una mabao 40. Hakuna mtu anaweza kumkumbuka Mayele.

Anapoondoka kocha mkuu aliyefanikiwa. Anapoondoka msaidizi wake aliyefanikiwa. Anapoondoka mshambuajili bora na mfungaji bora, timu haiwezi kubaki salama. Kocha mpya wa Yanga, Miguel Gamondi ana kazi kubwa ya kufanya.

Mshambuliaji mpya anayekuja kama Yanga wataachana kweli na Mayele, ana kazi kubwa kweli kweli. Kila michuano watakayoshiriki Yanga, mashabiki wa Yanga watataka kuone kombe. Kila mpira atakaogusa mshambuliaji mpya, mashabiki watataka kuona bao linaingia! Hii ndio kazi kubwa ambayo kocha na mshambuliaji mpya wanakabiliwa nayo.

Kibaya zaidi, ni mfumo mpya wa Ngao ya Jamii msimu mpya. Kama Yanga anafika fainali, ni wazi kuwa atakutana na timu bora mbili kati ya nne kwenye ligi yetu. Hapa pole pole tutaanza kuona uelekeo wa Yanga mpya. Ni muda wa kujiandaa Kisaikolojia kwa mashabiki wa Yanga.

Ni muda wa Wananchi kujiandaa na maisha mapya bila Mayele. Unadhani Yanga watakuwa Bora msimu ujao? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: