Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi kutikisa Taifa leo

Yanga Bingwa At 17 Wananchi kutikisa Taifa leo

Sat, 25 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Yanga leo inashuka dimbani kucheza na Tabora United katika uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam saa 10:00 alasiri, huku pia ikitarajiwa kukabidhiwa kombe lao la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sherehe za kukabidhiwa kombe hilo zitaanza majira ya saa 4:00 asubuhi kwa burudani mbalimbali kwenye uwanja huo kabla ya kuanza kwa mchezo huo .

Timu hiyo inashuka dimbani ikiwa haina cha kupoteza, lakini itahitaji kulinda heshima yao ya kutopoteza mechi hiyo ambayo wanakabidhiwa kombe la ubingwa.

Muhimu kilichopo mbele yao ni kuona kiungo wao mshambuliaji, Stephane Aziz Ki anaendelea na kasi yake ya kufunga na kutoa pasi za mabao ili mwisho wa siku kuibuka mfungaji bora kwa idadi nyingi ya mabao ambayo kwa sasa amefung 17 na Feisal Salum wa Azam FC akiwa na mabao 16.

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema anahitaji kuona timu yake inacheza vizuri na kupata matokeo chanya na kufanikiwa kuvuna alama tatu muhimu katika mchezo wa leo.

Alisema mashabiki baada ya kumaliza mechi zote watapata muda wa kufurahia, lakini sasa wanaenda kutafuta matokeo chanya katika mchezo huo dhidi ya Tabora United.

“Mchezo huu ni muhimu kama michezo mingine licha ya kutwaa ubingwa, wachezaji wanatambua kuwa tunahitaji matokeo mbele ya Tabora United,” alisema Miguel.

Mwakilishi wa wachezaji wa Yanga, Ibrahim Bacca alisema wamejiandaa vizuri na watapambana kutafuta matokeo mazuri na ushindi dhidi ya Tabora United. 

“Hautakuwa mchezo rahisi lakini tumefanya maandalizi mazuri na tunahitaji kupata pointi baada ya ushindi wa leo ndio tutasheherekea ubingwa tulioupata pomoja na mashabiki wetu uwanja wa Benjamin Mkapa,“ alisema Bacca.

Kocha Msaidizi wa Tabora United, Benard Fabian alisema maandalizi yamekamilika ni mchezo muhimu kwao kutafuta matokeo ili kujiondoa kwenye nafasi ya chini ya msimamo. 

Alisema hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu ubora wa wapinzani wao kila idara, wanaenda kucheza bila presha kwa sababu wanahitaji kupata matokeo ya kutafuta nafasi ya kubaki kwenye ligi kuu msimu ujao. 

“Huu mchezo kwetu ni muhimu kutafuta alama muhimu, tutaingia kwa tahadhari kubwa katika mchezo huu kulingana na ubora wa Yanga, pia ni siku yao ya furaha ya kusherehekea Ubingwa. Tofauti na sisi tuna uhitaji mkubwa wa mchezo huu,” alisema 

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema leo ni siku muhimu kwa Wananchi kushirikiana ubingwa wao na kuanza paredi ya Yanga na kombe litabebwa na Helkopta  litazunguka jijini Dar es Salaam.

Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Azam FC  dhidi ya Kagera Sugar. 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live