Ugonjwa ule ule ambao unawasumbua wakubwa wetu wa soka nchini, Simba na Yanga uliendelea juzi katika jiji la Bamako baada ya Yanga kuruhusu bao la kizembe la kusawazisha kutoka kwa wapinzani wao, Real Bamako na pambano kumalizika kwa sare.
Wakati Fiston Kalala Mayele alipogeuka katika ukingo wa boksi la wapinzani na kisha kupiga shuti zuri la mguu wa kushoto lililokwenda katika nyavu za ndani za lango la Real Bamako ilionekana kama vile Yanga walikuwa wanaondoka na pointi tatu ugenini.
Isingeshangaza sana. Juzi Simba waliichapa Vipers ugenini. Yanga pia waliichapa Club Africain kwake. Simba pia walitembeza kichapo kwa Primeira de Agosto kwake Luanda. Inaonekana kama vile klabu zetu zimeanza kuzoea kushinda nje. Usijali sana wapinzani wetu wana uzito kiasi gani, ukweli ni kwamba zamani hatukuzoea hivyo.
Juzi Yanga walikuwa karibu kabisa kuendeleza tabia hiyo kama si uzembe ule ule ambao waliufanya kwa bao la pili dhidi ya Monastir au kama sio kwa uzembe ule ule ambao Simba waliufanya dhidi ya Horoya pale Conakry Guinea wiki mbili zilizopita.
Kwanini wachezaji wetu wanashindwa kushughulika na mipira ya kona au friikiki? Majuzi nikiwa Tunisia niliongea na mwalimu msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze kumueleza namna ambavyo siridhishwi na ukabaji wa mipira wa kona kutoka kwa timu zetu.
Kwa mfano, pale Yanga wanatumia mfumo wa kukaba nafasi (zonal markinga) badala ya kucheza mtu na mtu (man to Man).
Ni kama ambavyo mfungaji wa bao la Real Bamako aliwakuta wachezaji wa Yanga wakiwa wamekaa katika nafasi huku yeye akiwa huru. Mpaka leo makocha wamekuwa wakibishana kuhusu mfumo sahihi wa kuzuia mipira ya kona. Ni wachezaji kuwakaba wapinzani, au kukaa katika nafasi ambazo mpira unaweza kupita?
Tukiachana na hilo ilikuwa ni mechi ambayo Yanga waliitawala wa kiasi kikubwa. Kama ile ni timu ambayo inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ya Mali unaweza kujua ni kwa namna gani Ligi yetu ipo mbele kwa baadhi ya Ligi nyingi za Afrika Magharibi.
Yanga walifanya kila kitu sahihi katika pambano lao la juzi kasoro kuzuia mpira mmoja wa kona katika dakika za majeruhi. Basi. Vinginevyo wangefuata nyayo za Simba katika kushinda ugenini. Walicheza vema katika kila idara.
Na sasa wanaturudisha tena katika hesabu zetu za vidole. Jana tulifanya hesabu zetu za vidole kwa Simba na tukaona kuna uwezekano Simba wakapita na Mwarabu wao Raja Casablanca kama wakizichanganya hesabu zao kwa usahihi.
Na kwa hesabu za vidole inaonekana kuna uwezekano mkubwa na Yanga nao wakapita katika hatua hii wakiwa na Mwarabu wao Monastir ya Tunisia. Kuna kila sababu. Nafasi yao ipo wazi licha ya kukosa pointi tatu juzi pale Mali.
Kitu ambacho kimewasaidia Yanga ni kwa Monastir kumchapa TP Mazembe mabao 2-0 pale Lubumbashi. Inakatisha tamaa kuona timu ambayo iliwahi kutamba katika michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa na kutwaa taji hilo mara tano, ikishindwa kufurukuta katika michuano kama hii ya Shirikisho.
Wiki moja iliyopita walichapwa na Yanga na sasa wamechapwa na Monastir. Hii inawaacha wakiwa na pointi tatu wakati Yanga wana pointi nne. Kitu kibaya zaidi kwao ni kwamba wiki ijayo wanalazimika kufunga safari mpaka Tunis kucheza tena na Monastir.
Katika soka lolote linaweza kutokea lakini kuna asilimia kubwa wakapoteza pambano hilo. Kuna asilimia kubwa pia Yanga wakashinda katika pambano la uwanja wa taifa dhidi ya Real Bamako. Hii itawapeleka Yanga kuwa na pointi saba wakati Mazembe watabakia na pointi tatu tu. Kama Mazembe akijitahidi kadri anavyoweza na kutoa walau sare katika pambano hilo basi atafikisha pointi nne tu huku Yanga wakiwa na pointi saba.
Yanga bado wataendelea kubakia nyumbani kucheza na Monastir na kuna uwezekano mkubwa wakaambulia pointi tatu au moja. Bado watakuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu. Kifupi ni kwamba kama Yanga akishinda mechi zote mbili akiwa nyumbani basi atafikisha pointi kumi. Ni ngumu kwao kutofuzu wakiwa na pointi hizo.
Nilichogundua kutoka kwao ni kwamba wana kila sababu ya kufuzu. Wana timu ya kufuzu. Katika mechi zote tatu ambazo wamecheza mpaka sasa Yanga wamemiliki mpira kwa kiasi kikubwa kuliko wapinzani wao.
Katika pambano dhidi ya Monastir walifungwa mabao mawili ya haraka haraka tena ya mipira ya kutengwa tu, lakini kuanzia hapo mizani yao ilisimama na mwisho wa mechi waandishi wa habari wa Tunisia walimshutumu kocha wa Monastir kwa kuruhusu Yanga kutawala pambano.
Sitazamii kitu tofauti katika pambano la marudiano Kwa Mkapa. kitu cha zaidi ambacho Yanga watakuwa nacho ni idadi kubwa ya mashabiki wa nyumbani. Ni faida ambayo Yanga wamekuwa nayo katika mechi mbili walizocheza ugenini. Mashabiki wa wenzetu hawaji uwanjani na zimewafanya Yanga wafurahie mechi vizuri tu.
Ni sehemu moja tu ambayo Yanga watakumbana na wakati mgumu. Ni pale ambapo watacheza na TP Mazembe ugenini. Bahati nzuri ambayo watakutana nayo katika pambano hili la mwisho ni kwamba Mazembe wana mashabiki wazuri lakini hawana timu nzuri.
Sioni sababu yoyote ya msingi ya Yanga kupoteza na Mazembe katika pambano la mwisho. Haijulikani itakuwa ni mechi yenye umuhimu kiasi gani kwa sababu kwa kadri ninavyopiga hesabu kuna uwezekano mkubwa Yanga wakaenda Lubumbashi wakiwa wamepita. Tunashuhudia kuanguka kwa moja kati ya timu kubwa barani Afrika.
Mazembe ya sasa sio ile ya kina Reinford Kalaba, Mbwana Samatta, Andrew Sinkala, Jean Kasusura, Tresor Mputu na wengineo.
Upande wa pili pia hesabu zinaonyesha hivi hivi. Huenda Simba wakaenda Casablanca wakiwa wamepita. Inategemea tu ni namna gani watacheza vizuri katika mechi zao mbili zijazo Kwa Mkapa. Lakini pia inategemea ni namna gani watasaidiwa kazi na Raja katika mechi dhidi ya Horoya.
Vyovyote ilivyo inafurahisha kuona timu za Tanzania zikitanua mbawa na zikienda kucheza ugenini huku akilini wakiamini kwamba wanakwenda kushinda mechi. Kama sio kosa la Yanga katika ukabaji wa kona ya juzi nadhani ingekuwa mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kwenda ugenini na kushinda mechi zao katika wikiendi moja.