Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanamichezo washiriki warsha ya michezo kitaifa

Swim Pic Data Wanamichezo washiriki warsha ya michezo kitaifa

Fri, 21 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wanamichezo kutoka maeneo mbalimbali nchini wameshiriki warsha ya kitaifa ya mtindo wa maisha kwa mchezaji iliyoendeshwa na Kamisheni ya wachezaji ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Warsha hiyo ya siku mbili imewahusisha wanamichezo wa judo, riadha, kikapu, soka, mieleka, mpira wa wavu, netiboli, magongo na kuogelea.

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Khalid Rushaka amesema hiyo ni warsha ya kwanza kuandaliwa na Kamisheni hiyo.

"Tumekuwa tukifanya makongamano, lakini tukaona kuna haja ya kuwa na warsha hii ambayo itasaidia kuwajenga wanamichezo kuwa na mtindo bora wa maisha katika vipaji vyao," amesema.

Katika warsha hiyo iliyokuwa na mada mbalimbali, Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau amesema inalenga pia kuwaandaa viongozi wa kesho.

Tandau aliyetoa mada ya mambo yanayoweza kuharibu kipaji cha mwanamichezo, alisema matumizi ya vilezi, dawa za kulevya, tumbaku, kutopumzika na mpangilio wa vyakula ni vitu ambavyo vinachangia kwa asilimia kubwa kufifisha ndoto za mchezaji.

Aidha, Tandau aliwashauri wanamichezo kuwa na utaratibu wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya kesho.

"Maisha ya uanamichezo ni mafupi, hivyo pale unapokuwa na nguvu na bado mchezaji ni vema kuweka akiba," amesema Tandau.

Miongoni mwa washiriki katika warsha hiyo ni makocha na wachezaji ambao baadhi yao kwa nyakati tofauti walieleza namna walivyofanikiwa hadi kuwa wanamichezo nguli nchini.

Nyota wa zamani wa riadha, Restituta Joseph amesema nidhamu ndiyo ilikuwa kila kitu kwake hadi kuwa miongoni mwa Olimpian nchini.

"Nimeshiriki Olimpiki mara nne, achilia mbali mashindano ya dunia na mengine ya kimataifa, lakini nilifika levo hiyo kutokana na kuwa na nidhamu ya mazoezi na kila kitu," amesema.

S.John Yuda aliyeshiriki mashindano ya riadha ya dunia mara tatu, Olimpiki mara mbili na kutwaa medali kadhaa za kimataifa ikiwamo ya Madola ni miongoni mwa washiriki, wengine ni mcheza judo, Andrew Thomas na Restituta Joseph. Mwanaspoti. Kata kiu ya michezo na burudani

Chanzo: Mwanaspoti