Majimaji iliwahi kushiriki ligi kuu na sasa imeshushwa daraja hadi ngazi ya Mkoa na itakosekana uwanjani kwa misimu miwili kutokana na adhabu hiyo.
Majimaji FC imeshushwa daraja na kufungiwa kucheza ligi kwa misimu miwili baada ya kushindwa kufika katika mchezo wake wa hatua ya mtoano ‘play off’ dhidi ya Kasulu United.
Timu hiyo ya mkoani Ruvuma ilikuwa inashiriki first league ambapo ilikuwa imalize mchezo wa marudiano kwenye hatua ya mtoano ‘play off’ dhidi ya Kasulu United ya mkoani Kigoma lakini haikuweza kusafiri kwa madai ya ukata.
Awali mechi hiyo ambayo ilikuwa ipigwe kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Aprili 18, kisha kusogezwa siku tatu mbele, lakini viongozi kupitia chama cha soka Wilaya ya Songea (Sorefa) iliomba kupelekwa tena hadi Aprili 29 lakini hata hivyo haikuweza kufika.
Awali katibu wa chama hicho, Godi Mvula aliliambia Mwanaspoti kuwa kutokana na ukata walionao hadi kushindwa kusafiri, wanasubiri uamuzi wowote kutoka kwenye mamlaka za soka kitakachoamuliwa.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Mei 4 na bodi ya ligi kuu nchini (TPLB) imefafanua kuwa kwa sababu mchezo huo ulikuwa wa play off, jambo hilo linatafsiriwa kikanuni kuwa ni kujitoa kwenye ligi.
“Baada ya Majimaji kujitoa na kwa mujibu wa kanuni ya 31;4(4.1) klabu hiyo inakabiliwa na adhabu ya kushushwa daraja na kufungiwa kucheza ligi kwa misimu miwili” imeeleza taarifa hiyo.