Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamiliki wa PSG wanazitaka Man United, Liverpool na Spurs

Wamiliki Wa PSG Wanazitaka Man United, Liverpool Na Spurs.jpeg Wamiliki wa PSG wanazitaka Man United, Liverpool na Spurs

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wanasema pesa hainunui mapenzi. Hivi ni kweli? Kuna ukweli kwenye dunia hii ya sasa? Baki na majibu yako. Lakini, ni pesa iliyowafanya Al-Nassr wanase huduma ya mtu wanayempenda, Cristiano Ronaldo.

Paris Saint-Germain kwenye kikosi chao kuna huduma ya wakali wa mapenzi yao, Kylian Mbappe, Neymar na Lionel Messi - hapo pesa imemaliza utata. Erling Haaland hakupindua kwa Manchester City ilipomhitaji na kuweka ofa ya mshahara mnono mezani. Eden Hazard hakujiuliza mara nyingi wakati Real Madrid ilipohitaji huduma yake na kumpa mshahara wa kibosi.

Pesa ina nguvu. Na pesa hiyo hiyo sasa inataka kutumika kwenye kung’oa vigogo. Mmiliki wa Paris Saint-Germain, kampuni ya Qatar Sports Investments (QSI) imekuwa kwenye mazungumzo ya kuimiliki klabu ya Tottenham Hotspur na sasa wanaripotiwa kuzihitaji pia Manchester United na Liverpool.

Man United na Liverpool zote ziliwekwa sokoni na wamiliki wake wa Kimarekani, Novemba mwaka jana. Familia ya Glazer wanahitaji wawekezaji wengine kwenye klabu ya Man United iwe wa hisa kidogo au mtu wa kuinunua jumla wakati wamiliki wa Liverpool, Fenway Sports Group nao wanahitaji dili la aina hiyo.

Uamuzi huo umekuja baada ya mauzo ya klabu ya Chelsea uliofanywa na bilionea Roman Abramovich - ambaye alimuuzia Todd Boehly na wabia wenzake Mei, mwaka jana. Chelsea iliuzwa kwa Pauni 2.5 bilioni, dili lililowashawishi Glazers na FSG kufikiria kuzipiga bei klabu zao ama kwa kuuza hisa kiasi au kuzipiga bei jumla. CBS Sports iliripoti Jumapili iliyopita mmiliki wa PSG, QSI, inataka kuwa sehemu ya uwekezaji kwenye klabu za Ligi Kuu England.

Mpango huo wa QSI ulimfanya mwenyekiti wake Nasser Al-Khelaifi kukutana na mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy huko London wiki iliyopita kujadili yanayowezekana. QSI wanataka kutanua uwekezaji wa Qatar kwenye soka baada ya fainali za Kombe la Dunia kukamilika. Mpango wao ni kumiliki timu nyingi za soka ili kuchuana na utawala wa Abu Dhabi wenye kampuni ya City Football Group ambao wanamiliki klabu nyingi ikiwamo Manchester City.

Na taarifa mpya kwa mujibu wa Bloomberg ni kwamba Man United na Liverpool nazo zipo kwenye mpango wa QSI, wakitaka ama kuzichukua jumla au kuwa wamiliki wenza. QSI wataendelea kutoa pesa PSG, lakini wanataka kujitanua zaidi kuwekeza kwenye klabu nyingi za soka la Ulaya.

Ukiweka kando PSG, Qatar inamiliki asilimia 23 ya hisa ya klabu ya Braga ya Ureno. Al-Khelaifi ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka za Ulaya ambao wana nguvu kwenye soka barani humo wapo kwenye mazungumzo ya wawekezaji watatu wadogowadogo ambao watamiliki hadi asilimia 15 ya hisa klabu ya PSG.

Mpango wa QSI kuwekeza kwenye Ligi Kuu England utawafanya waingie kwenye upinzani mkali na Abu Dhabi wanaomiliki Manchester City na Saudi Arabia Public Investment Fund inayoimiliki Newcastle United tangu Oktoba 2021.

Jambo hilo litafanya utawala wa wamiliki wa Kiarabu kwenye soka la dunia. City Football Group tayari inamiliki klabu 10 ikiwamo Manchester City, New York City na Melbourne City. Red Bull Group imamiliki RB Leipzig na Red Bull Salzburg, hivyo QSI wanataka wawe wamiliki wa PSG, Braga, Man United, Liverpool na Spurs.

Wamiliki wa sasa wa Man United, familia ya Glazer, Novemba mwaka jana walifichua kwamba wapo tayari kukaribisha wawekezaji wa ubia au kuiuza jumla timu hiyo kama atapatikana mnunuzi na walikuwa na mazungumzo na wawekezaji wa Kiarabu. Liverpool nao wamelenga kupata mnunuzi wa kutoka Mashariki ya Kati.

Chanzo: Mwanaspoti