Cristiano Ronaldo alipiga mbili Jumanne iliyopita kuinusuru timu yake ya Manchester United kupata kichapo mbele ya Atalanta katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa mabao hayo, Ronaldo, 36, sasa amefikisha mabao 139 kwenye michuano hiyo ya Ulaya - huku mabao yake mawili ya Jumanne yaliifanya Man United kupata sare ya 2-2 dhidi ya miamba hiyo ya Italia.
Ronaldo ndiye kinara wa mabao kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya - na anasimama mbele kwenye fowadi ya Kikosi cha Kwanza cha wakali wenye mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwenye kikosi hicho, golini atakuwa kipa Hans-Jorg Butt, ambaye amefunga mabao matatu katika michuano hiyo ya Ulaya, huku kwenye maisha yake yote ya soka alifunga mabao 32 katika mechi 479.
Kwenye safu ya mabeki, kutakuwa na Gerard Pique mwenye mabao 16 na Sergio Ramos mwenye mabao 15 watasimama kwenye beki ya kati, wakati beki wa kushoto ni Roberto Carlos mwenye mabao 16 na kulia ni Dani Alves mwenye mabao 12.
Kwenye kiungo, gwiji wa Man United, Paul Scholes atapata nafasi baada ya kufunga mabao 24 kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku wengine kwenye eneo hilo ni Thomas Muller, mwenye mabao 49, Cristiano Ronaldo mwenye mabao 139 na Lionel Messi mwenye mabao 123.
Kwenye safu ya ushambuliaji, wakali wawili watakaopangwa hapo ni, Karim Benzema aliyefunga mabao 75 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Robert Lewandowski mwenye mabao 81 kwenye michuano hiyo ya Ulaya.