Kuna usemi usemao ukiona cha nini wenzako wanawaza watakipata lini. Hivyo ndivyo ilivyo kwa baadhi ya mastaa ambao Simba na Yanga ziliwatema msimu uliopita, huku Singida Fountain Gate ikiwasajili.
Vigogo hao wa soka kutema mchezaji haijalishi kiwango chake kushuka au la wanaweza kumuacha kwa kumchoka kutokana na kukaa naye muda mrefu. Mwanaspoti linakuletea mastaa ambao timu hizo zimewaacha na huko ugenini wamegeuka lulu na kupata nafasi kuanza kikosi cha kwanza.
Pazia la Ligi Kuu Bara lilifungwa mwishoni mwa mwezi uliopita. Singida iko katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mashindano ya ndani.
GADIEL MICHAEL Beki huyu alitua Simba kwa mbwembwe akitokea Yanga 2019 wakati huo akiwa na uhakika wa kucheza kushoto kutokana na kikosi hicho wakati huo kuwa na uhaba wa mastaa.
Kutokana na upepo mzuri ambao Simba walikuwa nao hakuna mchezaji ambaye hakutamani kukipiga Msimbazi kwa kuwa mafanikio yalionekana kwao ndani na hata nje.
Gadiel hakuangalia ushindani wa namba uliokuwepo Simba chini ya Mohamed Hussen ‘Tshabalala’ akaona ni vyema kutimiza lengo licha ya kutopata nafasi. Msimu uliopita baada ya kumalizika uongozi wa Simba ulitangaza kumuacha na sasa ndiye nahodha wa Singida Fountain Gate.
Licha unahodha jicho la Mwanaspoti liliangaza katika michezo ya ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Simba na Azam, na kuona kiwango chake kilivyo bora.
Gadiel anaupiga mwingi na kushangaza wengi kutokana na namna ambavyo anasakata kabumbu dakika 90 akiaminiwa na aliyekuwa kocha mkuu Hans Pluijm.
BENO KAKOLANYA Miaka minne ndani ya Simba japokuwa hakuwa anapata nafasi chini ya kipa namba moja Aishi Manula ambaye ameliteka lango la Simba kwa ufanisi mkubwa, wadau walimtaka Kakolanya kuondoka kwenda kuendeleza kipaji na yeye aliziba pamba masikioni kwa kuwa alifahamu kwenda Simba sio kuwa kipa namba moja, bali kumsaidia aliyepo.
Baada ya Simba kumuona wa nini na kushindwa kumuongeza mkataba alipowataka kumlipa kiasi cha pesa (hakutaka kukiweka wazi) na uongozi kukataa, akaona isiwe tabu akatimka zake na huko Mungu kamjaalia ameaminiwa anaanza.
Kakolanya anasema kitendo cha kuaminiwa na Singida kimempa furaha na kujiona mpya, hivyo atapambana kuhakikisha anafanya vizuri na kuiweka timu salama.
JOASH ONYANGO Ubora wake hauwezi kuamini kama ndiye huyo Simba walimuacha bila kugeuka nyuma. Katika mafanikio aliyopata Onyango huko Simba misimu minne mfululizo yalichagiwa na ubora wake katika safu ya ulinzi.
Akaona isiwe tabu kuondoka Msimbazi na msimu huu ameuanza akiwa na walima alizeti Singida Fountain Gate na anapata nafasi ya kuanza katika kikosi hicho.
Ubora wa Onyango wengi hawakutarajia kama angetemwa, lakini wakati Simba wanawaza kumtema wengine walitega macho na masikio kumnasa.
Nyota huyo aliondoka Simba na kuacha alama mpaka kupewa jina la ‘nusu chuma, nusu mtu’ hivyo anasubiriwa kwa hamu katika makazi mapya licha ya mapokezi yake kutokuwa mazuri hasa katika mchezo wa karibuni dhidi ya JKU waliofungwa 2-0.
DICKSON AMBUNDO Winga huyu alitua Yanga 2021 akibahatika kupata nafasi mara chache ndani ya kikosi hicho akitokea Dododoma Jiji.
Ambundo katika mechi tatu ambazo Singida Fountain Gate imecheza - mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na Azam na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya JKU ameanza na kufanya vizuri. Kwa ubora alionao unaweza kushangaa mchezaji kama yeye kutemwa Yanga, lakini ndo hivyo.
Ambundo anasema maisha lazima yaendelee kwa kuwa mpira ndio kazi aliyoichagua na kutoka sehemu moja sio kushindwa kucheza bali ni mifumo na muda mwingine inaweza kumtoa mchezaji katika timu husika.
Anasema ametua Singida na atafanya kadri awezavyo katika timu iliyomuamini ili ipate mafanikio ambayo wamejipangia msimu huu.
HABIBU KYOMBO Mshambuliaji huyu aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita kutua kwake hakukuwakosha Msimbazi na kuujia juu uongozi mara tu alipotangazwa kabla ya ligi kuanza.
Manung’uniko yalikuwa sahihi kwani hakupata nafasi katika kikosi cha Simba na hata alipopata hakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Baada ya msimu kumalizika Simba ilitumia fangio la chuma kufagia wengi ilioona haiwatumii msimu huu na yeye akiwemo.
Mbali na wenzake waliopewa mkono wa kwaheri yeye pekee ndiye hajaanza katika michezo mitatu iliyopita akipata nafasi ya kukaa benchi katika mchezo dhidi ya Azam kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la Shirikisho uliopigwa Tanga.
Akiwazungumzia nyota hao, kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula anasema wachezaji walioachwa na timu hizo sio wabovu, bali namba zimewakosesha kuonyesha uwezo.
Anasema Kakolanya alivyokaa benchi Msimbazi kiwango chake kilipotelea hapo wakati angekuwa timu nyingine ni tegemeo kama alivyokuwa Yanga kabla ya kutimkia Simba.
Anasema wachezaji hao watafanya vizuri na kuwashangaza watu wengi, lakini jambo muhimu wapambane na kujituma ili kutimiza malengo.