Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamepotea mchana kweupee!

Ajib Namba (600 X 718) Ibrahima Ajib

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Zipo sababu mbalimbali zilizowatoa kwenye mstari baadhi ya wachezaji walioonyesha vipaji vikubwa na wakatabiriwa kufika mbali huku wakitarajiwa miguu yao ingewapa utajiri mkubwa.

Ipo hivi: Kinazungumziwa kizazi kilichochipua miaka ya 2000 na kilikuwa gumzo kila kona na kuwavuta wadau kwenda viwanjani kutazama wanachokifanya, ila baada ya muda kila mmoja wao akaanza kupotea kwenye ukubwa ule uliotarajiwa.

Makala hii inakuletea baadhi ya wachezaji hao wanaoendelea kupambana japo sio kwa ubora ule walioonekana mwanzo.

RAMADHAN SINGANO ‘MESSI’

Nyota huyu alijiunga na Simba 2011 na ilipofika 2015 aliondoka na kutimkia Azam FC huku kiwango chake ndicho kilichosababisha wadau kumpachika jina la mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na Paris Saint-Germain (PSG), Lionel Messi.

Kiwango chake kiliwafanya TP Mazembe kuinasa saini yake ingawa tangu ajiunge nao hakuweza kupata nafasi ya kucheza hali iliyomsababishia kutolewa kwa mkopo Nkana FC ya Zambia na sasa hana timu.

Licha ya matarajio makubwa kwa Watanzania wakiamini staa huyu angeendelea kuwika, mambo yamekuwa tofauti kwake kwani kadri siku zinavyozidi kusogea na jina lake linazidi kupotea kwenye mioyo ya mashabiki.

JUMA MAHADHI

Wakati winga, Simon Msuva anaondoka Yanga 2017 na kujiunga na Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, Mahadhi alitabiriwa kufuata nyayo zake lakini ameingia kwenye orodha hii ya mastaa wanaozidi kupotea kila uchao.

Kwa sasa anaichezea Geita Gold ambako hana uhakika wa kucheza mara kwa mara kutokana na ushindani wa namba uliopo kikosini.

PAUL GODFREY ‘BOXER’

Beki huyu yupo Singida Big Stars na alitabiriwa makubwa wakati akiwa Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera.

Akiwa Jangwani alionyesha kiwango kizuri kutokana na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara hali iliyowaaminisha wadau ni mbadala wa Juma Abdul lakini ameshindwa kulionyesha hilo.

ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’

Kiwango bora alichonacho kilisababisha aliyekuwa beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumpa jezi namba 23 aliyokuwa anavaa akiamini ndiye atakayekuwa mbadala wake sahihi pindi alipoondoka.

Ninja aliyewahi kukipiga LA Galaxy ya Marekani ushindani wa namba umemfanya kutokuwa tena tegemeo kwenye kikosi hicho na kutolewa kwa mkopo Dodoma Jiji ili kurejesha makali yake.

SHAABAN CHILUNDA

Chilunda aliwika na Azam FC na kuonyesha kiwango kilichowavutia mabosi wa CD Tenerife ya Hispania na kumchukua wakiamini ataendelea kukiwasha na kufika mbali zaidi ya hapa alipo.

Mbali na Tenerife ila alipata nafasi ya kuichezea Klabu ya CD Izarra ya huko huko nchini Hispania lakini aliondoka akijiunga na Moghreb Tetouan ya Morocco nako alishindwa na kurejea tena Azam.

IBRAHIM AJIBU

Ajibu ni kiungo mshambuliaji mzawa aliyetabiriwa kufanya makubwa kutokana na kipaji alichonacho, akiwahi kuzichezea timu zote kubwa nchini za Yanga, Simba na Azam FC anayoichezea hadi sasa.

Wakati dunia ikisonga mbele kwa kasi, nyota huyu anazidi kurudi nyuma kwani licha ya kuaminiwa angeendeleza ubora wake, ameshindwa kutamba na hata nafasi ya kucheza ni finyu.

MARCEL KAHEZA

Nyota huyu anaichezea Pamba kwa sasa ambayo inashiriki Ligi ya Championship akiwahi pia kuichezea Simba ya vijana chini ya miaka 20 kabla ya baadaye kupandishwa timu ya wakubwa.

Kutokana na ushindani wa namba uliokuwepo viongozi waliamua kumtoa kwa mkopo katika timu ya Majimaji ambako hata hivyo kiwango alichokionyesha msimu wa 2020/2021 kiliwashtua na kumrudisha.

Kaheza alipenda kuvaa jezi namba 10 kutokana na mapenzi yake kwa staa wa zamani wa Brazil, Rivaldo ila licha ya kutembelea nyota hiyo maisha yameenda kasi kwake kwani amejikuta akizidi kuporomoka.

EDWARD CHRISTOPHER ‘EDO’

Mshambuliaji huyu aliyewahi kutamba na timu mbalimbali za Moro Kids, Makongo, Yanga B, Moro United B, Simba, Polisi Morogoro, Toto Africans, Kagera Sugar na Ruvu Shooting ni miongoni mwa mastaa walioaminika watafanya vizuri na kufika mbali katika fani zao kwenye soka.

Edo aliwahi kukiri anajivunia aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Simba Mserbia, Milovan Cirkovic kutokana na kuona kipaji chake na kumpa nafasi ingawa ameshindwa kukiendeleza na kubakia mtaani.

Na ukimsikiliza Edo akisema hili utamuonea huruma alipobainisha: “Najutia baadhi ya mambo yaliyonifikisha hapa, ikiwemo unywaji wa pombe lakini napambana kuachana nayo ili nikitetee kipaji changu.”

YAHYA ZAYD

Kipaji kikubwa alichokionyesha akiwa na Azam kiliwashawishi mabosi wa Ismaily SC, Pharco FC za nchini Misri kunasa saini yake zikiamini nyota huyo atawasaidia.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti kwani alirejea tena nchini na kujiunga na Azam ambapo nako ameshindwa kuonyesha makali kwa sababu ya uwepo wa mastaa wengi wanaopigania namba.

WILLIAM LUCIAN ‘GALLAS’

Safu yote ya mabeki kwenye kikosi cha Simba B, 2012 ikiongozwa na Gallas sawia na mastaa wengine kama, Abuu Hashimu, Omary Salum, Hassan Isihaka na Hassan Hatibu ilipandishwa ili kuitumikia timu ya wakubwa.

Gallas alitabiriwa makubwa sana akiwa na kikosi hicho ila alishindwa kulinda na kupigania kipaji chake hivyo kupotea na sasa yupo mtaani akisubiri madili kupitia usajili wa dirisha dogo, baada ya kuvunja mkataba wake na Geita Gold aliyokuwa nayo msimu uliopita.

ADAM SALAMBA

Alianza kuonyesha imani kwa mashabiki nchini wakati akiitumikia Lipuli FC ya Iringa hali iliyowafanya mabosi wa klabu kubwa nchini kuiwinda saini yake ingawa ni Simba iliyompata 2018.

Salamba aliyeibukia Stand United 2016 alishindwa kutamba akiwa Simba hivyo kutolewa kwa mkopo Al-Jahra SC ya Kuwait 2019 na Namungo FC 2020 kisha kutimkia JS Saoura ambako nako ameshindwa kutamba.

SALUM AIYEE

Aliwika sana akiwa na Mwadui FC msimu wa 2018/19 ambao alimaliza na mabao 19 nyuma ya Meddie Kagere wa Simba aliyeibuka kinara kwa mabao 23, jambo lililomfanya msimu uliofuata asajiliwe KMC ambako hakuendeleza makali yake.

Kwa sasa mchezaji huyo yupo Fountain Gate ya Championship akicheza kwa mkopo akitokea Geita Gold, akiwahi kuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wanatazamwa sana.

MSIKIE RWEYEMAMU

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ambaye amechangia wachezaji wengi kutoka kisoka katika kikosi hicho anasema sababu kubwa ya wengi wao ni kujisahau na kukosa nidhamu ya soka.

“Wanajisahau sana hasa wanapofika kwenye hizi timu kubwa kwani wengi wao wanaendekeza starehe na kusahau maisha ya mpira ni mafupi hivyo kujikuta wanapotea mapema licha ya vipaji vyao.”

Chanzo: Mwanaspoti