Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamepishana na mataji Yanga

Pishana Pic Data Wamepishana na mataji Yanga

Thu, 14 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Imeichukua Klabu ya Yanga miaka minne kusotea mataji matatu ambayo Simba ilikuwa ikiyatwaa na kutamba nayo.

Msimu huu Yanga ilikuwa bora na kufanyakua mataji yote matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) huku baadhi ya wachezaji wakipishana na bahati hiyo waliyoipambania.

Hii ni makala ya baadhi ya mastaa waliopambana misimu iliyopita huku msimu huu wakipishana na mataji hayo yaliyosakwa kwa muda mrefu.

HARUNA NIYONZIMA

Kiungo aliyeacha alama katika soka la Tanzania alianza kukipiga Yanga baadae akatimkia Simba na kurejea tena Yanga.

Alikuwa miongoni mwa mastaa waliopambana msimu uliopita kuipatia Yanga taji lakini hali haikuwa hivyo, benchi la ufundi lililazimika kumpunguza kwenye kikosi cha msimu huu.

Kuondoka kwake kumemfanya apishane na makombe aliyoyapambania muda mrefu lakini haikuwa haba alikotimkia timu ya As Kigali ya Rwanda ilitwaa taji la ligi kuu nchini humo.

Niyonzima anasema amefarijika kuona Yanga inatwaa ubingwa wa ligi ambao imekukosa muda mrefu.

"Ilikuwa ndoto zangu kuyapata mataji hayo nikiwa Yanga lakini sio mbaya yamekuja nikiwa nimetoka, nawatakia maandalizi mema kuelekea msimu ujao," anasema Niyonzima.

MICHAEL SARPONG

Mshambuliaji aliyekuwa na wakati mgumu ndani ya Yanga hadi kupelekea kumtema ili kuboresha safu hiyo ambayo msimu huu imekuwa tishio.

Sarpong amepishana na bahati aliyoipambania msimu uliopita baada ya kutemwa na kujiunga na As Kigali iliyomfuta machozi baada ya kutwaa taji la ligi. Sarpong aliitumikia Yanga msimu mmoja pekee ndani ya miaka miwili aliyokuwa amesaini huku akiwa amefunga mabao manne.

FISTON ABDULRAZAQ

Bahati haikuwa kwake alipotua Yanga msimu uliopita, licha ya ubora aliokuwa nao miaka kadhaa iliyopita kusababisha asajiliwe.

Fiston anayekipiga RS Berkane mabingwa wa kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushindwa kufanya vizuri Yanga alibahatika kufutwa machozi katika makazi yake baada ya kupishana na bahati hiyo.

Anasema Yanga ni timu aliyoitumikia kwa mapenzi yake yote lakini mfumo ulimkataa na kulazimika kutafuta maisha mengine nje ya timu hiyo.

"Unapoondoka sehemu vizuri, unafurahia mafanikio yao hata kama sio sehemu ya kikosi kwa wakati huo, niwaambie tu wanatakiwa kujipanga kulinda heshima hiyo msimu ujao," anasema Fiston.

TUISILA KISINDA

Mshambuliaji aliyekuwa na mbio kama mnyama aina ya digidigi alisajiliwa Yanga akitokea As Vita ya DR Congo lakini ubora wake ulipelekea Yanga wamuuze na kuwasajili Yanick Bangala, Fiston Mayele.

Kisinda kwa sasa anakipiga RS Berkane ya Morocco na yeye licha ya mchango wake mkubwa ndani ya muda aliocheza Jangwani lakini hakubahatika kupata taji lolote.

DITRAM NCHIMBI

Mshambuliaji aliyekuwa na wakati mgumu alipokuwa Yanga, katika mapambano ya kuipatia mataji klabu hiyo ilishindikana na hadi kuamua kumtema.

Nchimbi alitua Geita Gold alipewa nafasi kubwa lakini mambo yalikwenda ndivyo sivyo na kujikuta akipishana na bahati ambayo waajili wake wa zamani wameipata msimu huu.

FAROUK SHIKHALO Ni kipa aliyekuwa akitegemewa Yanga msimu uliopita haukuwa bora kwake, uongozi wa Yanga uliamua kumfungashia virago.

Sasa anakipiga KMC moja ya timu yenye ushindani ligi kuu, amejikuta akipishana na bahati hiyo ya makombe waliyoipata mabosi wake wa zamani.

Shikhalo anasema, mafanikio waliyoyapata Yanga msimu huu wameyatafuta kwa muda mrefu tangu akiwa sehemu ya kikosi hicho.

"Mimi nawapongeza wachezaji wote wa Yanga kwa mapambano maana msimu huu haukuwa wa mchezo kila timu ilikuwa na ushindani mkubwa, na wao kutwaa mataji yote ni jambo la kupongezwa, siwezi kuacha kuwapongeza kisa sio mchezaji wao sasa," anasema Shikhalo.

METACHA MNATA

Na yeye ni miongoni mwa mastaa waliotimulia msimu huu kutokana na maboresho makubwa ambayo benchi la ufundi liliamua kuyafanya.

Alitimkia Polisi Tanzania akipishana na makombe aliyoyapambania muda mrefu na msimu ujao anatarajiwa kuwa sehemu ya mastaa wa Singida Big Stars waliomtambulisha hivi karibuni.

Metacha anasema, maisha ya mchezaji ni kambi popote hivyo mafanikio ambayo Yanga imepata ni wakati umefika kwao.

"Wamepambana kupata mafanikio hayo hata sisi tulifanya hivyo lakini wakati haukuwa wakati ule, sasa hivi niko sehemu nyingine na maisha yanaendelea," anasema Metacha.

Chanzo: Mwanaspoti