Wanasema usipojipanga, utapangwa. Hicho ndicho kilichotokea kwenye dirisha la usajili baada ya timu kupigwa mkwanja mrefu tofauti na thamani halisi ya wachezaji, wakati ilipofanya usajili kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Kuna wachezaji hao wameuzwa kwa pesa nyingi sana, tofauti na thamani zao na klabu zimepigwa parefu.
Kampuni ya Spin Genie ya Uingereza imefanya utafiti wa kutambua klabu zilizopigwa pesa ndefu kwenye usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi kwenye Ligi Kuu England na ligi nyingine duniani kutokana na kuuziwa wachezaji pesa ndefu tofauti na thamani zao halisi.
Kilichofanyika ni kulinganisha pesa iliyolipwa kunasa saini zao dhidi ya thamani zao halisi sokoni kwa kipindi wanasajiliwa.
Chelsea ilimsajili staa wa Brighton, Moises Caicedo kwa mkwanja wa Pauni 115 milioni, pesa ambayo ilivunja rekodi ya uhamisho huko Uingereza.
Chelsea iliizidi ujanja Liverpool na kumnasa kiungo huyo ambaye imemsainisha mkataba wa miaka minane huko Stamford Bridge.
Hata hivyo, utafiti huo unafichua Chelsea imelipa Pauni 50 milioni zaidi kwenye usajili huo wa Caicedo kulingana na thamani yake sokoni. Chelsea ilipaswa kulipa Pauni 65milioni tu kunasa saini ya mkali huyo wa Ecuador.
Klabu za soka za Saudi Arabia zilitumia pesa nyingi sana kusajili kwenye dirisha hili, hasa Al-Hilal, ambayo ililipa ziada ya Pauni 26 milioni kwenye usajili wa Malcolm na Neymar.
Kwenye orodha ya timu zilizotumia pesa nyingi ni pamoja na Manchester United, hasa kwenye dili za mastaa straika Rasmus Hojlund na kipa Andre Onana.
Man United inayonolewa na kocha Erik ten Hag ilimnasa straika Hojlund kwa Pauni 72 milioni kutoka Atalanta ya Italia licha ya kutokuwa na uzoefu sana, akiwa amefunga mabao 27 tu katika historia ya soka lake kwa ngazi za klabu.
Kampuni hiyo ya masuala ya takwimu inaamini Man United imelipa Pauni 26 milioni zaidi kwenye usajili wa Hojlund na Pauni 15 milioni ilipomnasa kipa Onana.
Arsenal walifanya maboresho kwenye kikosi chao wakitumia zaidi ya Pauni 210 milioni kwenye usajili wa mastaa Declan Rice, Kai Havertz na Jurrien Timber.
Miamba hiyo ya Emirates ililipa Pauni 105 milioni kumchukua nahodha wa zamani wa West Ham United, Rice – na kwamba Arsenal ililipa ziada ya Pauni 23 milioni kwenye usajili wa mchezaji huyo kulingana na thamani yake sokoni, huku Chelsea iliweka kibindoni ziada ya Pauni 17 milioni kwenye mauzo ya staa wa Kijerumani, Havertz.
RB Leipzig walipiga mkwanja mrefu kwenye dirisha la usajili, licha ya kwamba iliwapoteza mastaa wake makini kama Dominik Szoboszlai na Josko Gvardiol waliotimkia Liverpool na Manchester City mtawalia.
Klabu hiyo ya Ujerumani ilipokea jumla ya ziada ya Pauni 30 milioni kwenye mauzo ya wachezaji hao tofauti na thamani zao sokoni zilivyokuwa zinasoma wakati wananaswa.
Uhamisho mwingine uliokuzwa sana thamani yake ni ule wa Matheus Cunha ambao awali ulikuwa wa mkopo kutoka Atletico Madrid kwenda Wolves kabla ya kufanywa kuwa wa jumla.