Enzo Fernandez amekuwa mchezaji ghali zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England. Kiungo huyo wa Argentina aliigharimu Chelsea Pauni 107 milioni iliponasa huduma yake kutoka Benfica kwenye dirisha la uhamisho wa Januari mwaka huu.
Hiyo ina maana, Jack Grealish ada yake iliyolipwa na Manchester City ya Pauni 100 milioni ilipomnasa kutoka Aston Villa miezi 18 iliyopita imezidiwa na atakuwa mchezaji namba mbili kugharimu pesa nyingi kwenye historia ya Ligi Kuu England.
Lakini, si wawili hao tu waliokula pesa nyingi za uhamisho kwenye klabu za Ligi Kuu England baada ya kuwapo wengine kibao waliongia kwenye orodha hiyo.
Hata hivyo, hawa hapa mastaa 10 ambao kimsingi ndiyo wanaohesabika kuwa wamekula pesa nyingi za klabu za Ligi Kuu England saini zao ziliponaswa.
1. ENZO FERNANDES
Kutoka: Benfica
Kwenda: Chelsea
Ada: Pauni 107 milioni
Mwaka: 2023
Kushinda taji la Kombe la Dunia 2022 akiwa na kikosi cha Argentina na kucheza kiwango bora kwenye fainali hizo za Qatar kuliwavutia Chelsea na kutoa pesa ndefu kunasa saini yake kutoka Benfica.
Enzo alinaswa na miamba hiyo ya Ureno kwa Pauni 10 milioni tu akitokea River Plate, hivyo kwenye mauzo hayo waliyofanya huko Stamford Bridge wamepata faida kubwa sana. Fernandez tayari ameshaanza kuitumikia The Blues Ligi Kuu England.
2. JACK GREALISH
Kutoka: Aston Villa
Kwenda: Man City
Ada: Pauni 100 milioni
Mwaka: 2021
Pep Guardiola alivunja rekodi ya uhamisho Uingereza wakati alipotoa Pauni 100 milioni kunasa saini ya kiungo mshambuliaji, Jack Grealish kutoka Aston Villa ili kwenda kukiboresha kikosi chake cha Manchester City kiwa tishio ndano ya uwanja.
Tangu atue Etihad, Grealish bado hajaonyesha kiwango kinachoendana na thamani ya pesa iliyolipwa kupata saini yake, lakini tayari amekuwa akienda vyema katika kuelekea mafanikio hayo akichangia vizuri kwenye fowadi yao.
3. ROMELU LUKAKU
Kutoka: Inter Milan
Kwenda: Chelsea
Ada: Pauni 97.5 milioni
Mwaka: 2021
Huu ni usajili wa pesa nyingi ulikuwa na hasara kubwa zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England.
Kwa sababu Chelsea ilitoa pesa nyingi kumrusha straika Lukaku kwenye kikosi chao ikimtoa Inter Milan, lakini baada ya miezi michache tu, mchezaji huyo amerudi tena Serie A kwa mkopo kutokana na kiwango chake kuwa kibovu huko Stamford Bridge.
Lukaku aliigharimu pesa nyingi Chelsea, lakini amewaacha wakihangaika kusaka straika mpya awasaidie uwanjani.
4. PAUL POGBA
Kutoka: Juventus
Kwenda: Man United
Ada: Pauni 89 milioni
Mwaka: 2016
Huu ni usajili wa kwanza uliovunja rekodi ya uhamisho England, hasa ukizingatia Juventus wao awali walimpata bure kabisa Paul Pogba kutoka Manchester United, ambapo walilipa tu fidia ya miamba hiyo ya Old Trafford kumlea.
Hiyo ilikuwa mwaka 2012 na miaka minne baadaye, Man United ilikwenda kumsajili tena Pogba kwa pesa ndefu. Mfaransa hakuna cha maana alichofanya Old Trafford na mwaka jana alirudi zake Juventus kwa uhamisho wa bure.
5. MYKHAILO MUDRYK
Kutoka: Shakhtar Donetsk
Kwenda: Chelsea
Ada: Pauni 88 milioni
Mwaka: 2023
Taratibu Mudryk atakwenda kuwa tishio kwenye kikosi cha Chelsea na amekuwa akiwakumbusha mashabiki wa timu hizo enzi za huduma ya mkali wa Kibelgiji, Eden Hazard, aliyemuuza kwenda Real Madrid kwa mkwanja mrefu. Winga, Mudryk bado hajapata kasi kisawasawa kwenye kituo chake kipya cha kazi, lakini ni moja ya maingizo ya pesa nyingi kwenye Ligi Kuu England, huku mashabiki wa The Blues wakisubiri kuona mambo makubwa kutoka kwake kusaidia kikosi.
6. ANTONY
Kutoka: Ajax
Kwenda: Man United
Ada: Pauni 85.5 milioni
Mwaka: 2022
Mwanzoni lilionekana ni dili la kijanja kutokana na mchezaji huyo alichokuwa akifanya huko Ajax chini ya kocha Erik ten Hag. Mbrazili huyo aliamua kumfuata kocha wake wa zamani, Ten Hag wakati alipotua Old Trafford na taratibu amekuwa akionyesha ubora wake kwenye kikosi hicho cha Manchester United.
Mashabiki kadhaa wamekuwa wakikosoa staili ya uchezaji ya Antony, lakini kimsingi mchezaji huyo amekuwa na umuhimu mkubwa kwenye kikosi hicho.
7. HARRY MAGUIRE
Kutoka: Leicester City
Kwenda; Man United
Ada: Pauni 85 milioni
Mwaka: 2019
Amepita kwenye nyakati tofauti katika maisha yake kwenye kikosi cha Manchester United, kiwango chake kikipanda na kushuka.
Kwa msimu huu, mambo yake yamekuwa magumu tangu kikosi hicho kilipoanza kuwa chini ya kocha Mdachi, Erik ten Hag, lakini alishangaza wengi wakati alipojumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England na Kocha Gareth Southgate alipokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.
8. ROMELU LUKAKU
Kutoka: Everton
Kwenda: Man United
Ada: Pauni 75 milioni
Mwaka: 2017
Jose Mourinho baada ya kubamba ajira huko Manchester United aliamua kwenda kunasa saini ya straika Romelu Lukaku kutoka Everton na hakika alilipa pesa nyingi kumnasa mkali huyo.
Lakini, baada ya Mourinho kufutwa kazi na miamba hiyo ya Old Trafford kuwa chini ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer, mambo yalikwenda kombo kwa Mbelgiji huyo na kufunguliwa mlango wa kutokea, akapigwa bei kwenda Inter Milan kwa Pauni 70 milioni.
9. VIRGIL VAN DIJK
Kutoka: Southampton
Kwenda: Liverpool
Ada: Pauni 75 milioni
Mwaka: 2018
Moja ya mafanikio ghali machache yaliyosaidia Liverpool kushinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu England na kuongeza taji jingine kwenye kabati lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Beki wa kati wa Kidachi, Virgil van Dijk aliikwenda kuwafanya Liverpool ya kocha Jurgen Klopp kuwa bora zaidi ndani ya uwanja na hilo limewasaidia kuwa timu washindani kwenye ligi hiyo wakichuana jino kwa jino na Manchester City kabla ya mambo kwenda kinyume chake msimu huu.
10. JADON SANCHO
Kutoka: Borussia Dortmund
Kwenda: Man United
Ada: Pauni 73 milioni
Mwaka: 2021
Ulionekana kuwa usajili matata wakati Manchester United ilipofanikiwa kunasa saini ya winga Mwingereza, Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.
Lakini, mambo hayakuwa rahisi kwa Sancho, ambapo chini ya Kocha Erik ten Hag alimweka benchi kwa muda mrefu mchezaji huyo, akimfanyisha mazoezi nifasi ili kurejea kwenye kikosi akiwa kwenye viwango bora na siku za karibuni ameoonekana kurudi uwanjani akiwa kwenye moto wa hali ya juu.